November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yakunwa na TIRA, yatoa maelekezo Sekta ya Bima

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online


SERIKALI imepongeza kazi kubwa
inayofanywa na Mamlaka ya Usimamizi
wa Bima Tanzania (TIRA) na imetoa
maelekezo manne kwa mamlaka hiyo
na wadau wengine kuimarisha mikakati
ya uendelezaji sekta ndogo ya Bima
kwa mfumo wa utoaji huduma kwa njia
ya kidigitali.

Pongezi na maelekezo hayo yametolewa
juzi jijini Dar es Salaam na Waziri wa
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt.
Damas Ndumbaro, alipomwakilisha
Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu
Nchemba, kwenye uzinduzi wa Taarifa
wa Taarifa za Utendaji wa Soko la Bima
kwa mwaka 2022.

Pili, Dkt. Ndumbaro ameagiza watoa
huduma za Bima waendelee kuimarisha
matumizi ya teknolojia ili kusimamia na
kuuza bidhaa za bima kwa lengo la kufikia
wananchi kwa urahisi.

Tatu, Dkt. Ndumbaro ameitaka TIRA
kuendelea kusimamia miongozo iliyopo
kuhakikisha wananchi wanapata huduma
zilizokusudiwa kwa haki,usawa na kwa
uharaka uliokusudiwa.

Nne, ametaka wadau wote wa sekta
ndogo ya bima wajiepushe na vitendo vya
ubadhirifu ikiwepo matumizi ya bima feki,
ambayo yanarudisha nyuma maendeleo
ya Taifa.

Kwa mujibu wa Dkt. Ndumbaro vitendo
hivyo ni jinai na ameelekeza mamlaka
zinazohusika kuchukua hatua kali kwa
wanaohusika na kushiriki katika utoaji na
utumiaji wa huduma feki.

Amesema katika kipindi cha uongozi wa
Rais Samia Suluhu Hassan, wanaona
sekta ya Bina inakua kwa kasi, hivyo ana
kila sababu ya kumpongeza’
Aidha, alimpongeza Rais wa Zanzibar,
Dkt. Hussein Ali Mwanyi kwa kazi
kubwa anayoifanya kuleta maendeleo ya
kiuchumi Zanzibar hususani katika sekta
ya umma.

Dkt. Ndumbaro ameendelea kupongeza
uongozi wa TIRA kwa kazi nzuri ambayo
wanaifanya, kwani taarifa iliyozinduliwa
imeonesha takwimu nyingi ambazo ni
nzuri.

Lakini pia amewataka kuendelea kuimarisha mikakati ya uendelezaji sekta ndogo ya bima kwa mfumo wa utoaji huduma kwa njia ya kidigitali.

“Nawapongeza kwa uzinduzi huu,
ripoti hii mngekaa nayo ofisini kwenu
wadau wengi wasingeijua, uzinduzi huu
ni jambo muhimu kwa sisi tulioko hapa
kuweza kujua mambo mazuri ambayo
mnayafanya, yamesheheni kwenye ripoti
hii, lakini kupitia hadhara hii Watanzania
wote na dunia nzima wanaweza kujua
mambo mazuri ambayo mnayafanya,”
amesema Dkt. Ndumaro.


Amefafanua kwamba ripoti hiyo
imezinduliwa ili waweze kuipata na kuitumia vizuri.

Amesema katika kutimiza majukumu yake, TIRA inaongozwa mambo mbalimbali. Kwanza, alisema inaongozwa na mpango mkuu wa maendeleo ya sekta ya fedha ambao unatekelezwa kwa mwaka 2019-2020 mpaka 2026.

Pia amesema kuna mpango wa maendeleo wa miaka mitano wa mwaka 2021-2022 mpaka 2025/ 2026.

“Lakini ni muhimu zaidi inaogozwa na ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025 na moja kati ya maeneo ambayo tunajivunia kwamba tumefanya vizuri sana ni eneo la Bima,” amesema Dkt. Ndumbaro na kuongeza; “Ni muhimu zaidi katika suala la Bima kuna maeneo matatu lazima yazingatiwe, kwanza ni kujenga ufahamu na umuhimu wa bidhaa za bima, kwani bado ufahamu na uelewa wa watu kwenye bima na bidhaa zake na umuhimu wake ni mdogo sana.”

Amesema watu wanadhani bima ni kwa ajili ya magari na sio kwamba wanapenda kwa ajili ya gari, bali ni kwa sababu sheria inamlazimisha na anajua asipokuwa na bima atakamatwa na askari. Alisema kama pasingekuwepo askari barabarani hata bima za kwenye magari zisingekatwa.

“Maana yake ni kwamba uelewa wetu, ufahamu wa watu wa bima na bidhaa za bima na maslahi ya bima bado ni mdogo sana,” amesema Dkt. Ndumbaro.

Hivyo, amewataka wadau wote wachukue hiyo kama changamoto, waifanyie kazi zaidi ili kuelimisha Watanzania umuhimu wa Bima hasa kipindi hiki, ambacho Serikali imepitisha na kutunga Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote. Alisema Watanzania wanahitaji elimu zaidi ili watu wengi waweze kunufaika na Bima. Akifafanua zaidi, alisema kazi ya bima ni kulinda mali na maisha ya watu.

Amesema kwenye suala la Bima, inahitajika mifumo ambayo itaondoa urasmu, makosa ya kiufundi na itaweza kutoa matokeo ndani ya muda mfupi, kwa sababu mtu ambaye amekata bima halafu akalalamika, wale wote wanaosikia malalamikio hayo wanakuwa na mtazamo hasi dhidi ya bima. Alisema ili kupunguza mtazamo hasi ni vizuri malalamiko yashughulikiwe haraka. Dkt. Ndumbaro alisema takwimu za miaka mitano zinaonesha Sekta ya Bima inakuwa na ukiona inakua, lazima ujiulize sababu ambazo zinakufanya ukue.

“Kwa hiyo wakati nawapongeza kwa sekta kukua ndani ya miaka mitano katika kila eneo , hivyo natoa rai tuendelee kuhakikisha kwamba tunakua zaidi ili tuchangie pato la nchi na kuwaweka Watanzania wawe salama zaidi,” amesema Dkt. Ndumbaro na kuongeza; “Tupambane na kuwapa Watanzania kilicho bora zaidi.

***BIMA YA AFYA

Kwa upande wa Bima ya Afya kwa Wote, Dkt. Ndumbaro amesema safari ya kuwa na Bima ya afya ni ya muda mrefu sana, imechukua miaka 21.

Amesema kitu ambacho wamekisubiri kwa miaka 21, lazima wahakikishe wanakitumia vizuri, kwa sababu bima ya afya kwa wote ni haki za binadamu. Dkt. Ndumbaro alisema kila mtu apate huduma sawa.

“Tukishakuwa na bima ya afya, uwe tajiri, uwe maskini wote mpo sawa, kwa hiyo utekelezaji wa hii sio tu utekelezaji wa Malengo ya Milenia, lakini kwetu ni utekelezaji wa Ibara ya 13 ya katiba ambayo inasisitiza usawa kwa wote.”

Amewataka wadau wa bima wajitaidi washirikiane na TIRA ili Watanzania wengi waweza kumudu hivyo vifurushi, wakiwemo wananchi wa chini kabisa ili waweze kuzimudu.

Kwa upande wake Kamishna wa TIRA, Dkt. Baghayo Saqware, alipongeza Rais Samia kutokana na miongozo yake ambayo anatoa, kwani imekuwa ikisaidia sekta ya bima.

“Kama ambavyo mnafahamu Rais Samia amesaini muswada wa Bima ya Afya kwa Wote na sisi kama TIRA tuko tayari kuendesha na kusimamia biashara ya bima nchini,” amesema Dkt. Saqware.