November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samia kutua Katesh na maelekezo mazito


*Ni baada ya kufupisha ziara yake nchini Dubai, wengi wakunwa alivyoshuhulikia maafa hayo, misaada yaendelea kumiminika Hanang

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

RAIS Samia Suluhu Hassan, leo anatarajia kufanya ziara Katesh, mkoani Manyara kwa lengo la kuwapa pole wananchi waliopata maafa ya mafuriko ya maporomoke ya tope yaliyotokea Jumapili pamoja na kutoa maelekezo mengine ya kazi inayoendelea.

Rais Samia anawasili Katesh baada ya kufupisha ziara yake nchini Dubai, alipokuwa akihudhuria Mkutano wa 28 wa Umoja wa Mataifa wa nchi wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28).

Ziara hiyo ya Rais Samia inafanyika, huku maelekezo yote aliyoyatoa akiwa nje yakiwa yametekelezwa kwa ufanisi mkubwa ikiwemo la kutaka nguvu zote za Serikali kuelekezwa Hanang’ kwa ajili ya uokoaji.

Aidha, Rais Samia alielekeza waliopata na maafa na kupoteza makazi wastiriwe vizuri, pamoja na Serikali kugharamia mazishi na matibabu ya waliojeruhiwa kwenye maafa hayo.

Maelekezo mengi yalikuwa ni pamoja na Wizara ya Madini kufanya utafiti kwenye Mlima Hanang’ ili kujua sababu zilizosababisha maporomoko hayo, ambapo tayari taarifa ya awali imetolewa.

Kinachoongeza uzito na ziara ya Rais Samia na kusubiriwa kwa hamu na wananchi wa Hanang’ ni kwa jinsi ambavyo amekuwa karibu na wananchi hao, ikiwemo kutuma akasri kutoka kwenye majeshi yetu wakiongozaskari na askari Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wapatao 1,285.

Aidha, madaktari bingwa wamepiga kambi wilayani Hanang’ wakiendelea kutoa matibabu kwa majeruhi.

Wakati Rais Samia akisubiriwa kwa hamu Katesh, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi, imeeleza kuwa Serikali inaendelea kuyashughulikia maafa haya kwa kutumia wizara za kisekta na vyombo vya dola.

Amesema hadi sasa Serikali imegharamia mazishi ya watu wote waliopoteza maisha, kutoa matibabu ya bure kwa majeruhi wote, kuweka na kuhudumia kwa kila kitu kambi za waathirika wa maafa na kuondoa tope lililojaa mitaani na barabarani katika mji mdogo wa Katesh.

Aidha, amesema kazi ya utafutaji miili kwenye tope inaendelea ambapo kuna jumla ya askari 1,285 vikosi vya majeshi mbalimbali nchini wanaofanya kazi hiyo.

***Kuchimba visima
Matinyi, amesema Serikali imeanza kuchimba visima vya maji katika maeneo yaliyoathirika kwa kukosa maji kufuatia banio la maji yatokayo mlima Hanang kubomoka.

Pia, anasema inafanya utambuzi wa nyumba zilizobomoka na kaya zilizoathirika kwa kutumia picha za satelaiti za kabla na baada ya tukio na kulinganisha na taarifa za sensa ya Agosti 2022 pamoja na taarifa za serikali za mitaa.

“Serikali pia imeleta wataalamu wa ushauri nasaha kutoka Wizara ya
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ili
kuwasaidia wananchi waliopatwa na mshituko wa maafa haya ikiwa ni
pamoja na kujeruhiwa na kupotelewa na ndugu na jamaa,” amesema Matinyi.

***Misaada ya Serikali

Matinyi amesema Serikali imeendelea kupokea misaada mbalimbali kutoka kwenye taasisi za umma na binafsi likiwemo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, umoja wa watoa huduma za mawasiliano ya Simu Tanzania (TAMNOA) pamoja na klabu mbili za mpira wa miguu nchini za Simba na Yanga.

Amesema jana Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson, alifanya ziara Katesh jana kuangalia madhara yaliyotokea, kukagua huduma za uokoaji na misaada inayotolewa, kuwatembelea waathirika waliolazwa hospitalini pamoja na waliopo kwenye kambi na kuwapa pole wananchi wa Hanang.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, leo anatarajiwa kufanya ziara Katesh kwa ajili ya kuwafariji wananchi waliopata maafa.