Na Mwandishi Wetu,TimasmajiraOnline,Dar
RAIS Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwepo Dubai kwa ajili ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28), ameamua kufupisha safari hiyo na kurejea nchini haraka ili kushughulikia kwa karibu janga mafuriko wilayani Hanang, mkoani Manyara.
Rais Samia amefupisha kuendelea na mkutano huo, huku vifo vilivyotokana na mafuriko hayo yaliyoambatana na maporomoko ya tope vikifikia zaidi ya 63 na wengine zaidi ya majeruhi 116 kujeruhiwa.
Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu jana, ilieleza kwamba mbali na Rais Samia kufupisha safari yake hiyo, ametoa maelekezo kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuwa Serikali igharamie mazishi ya wote waliopoteza maisha.
Kugharamia matibabu
Aidha, Rais Samia pia ametaka majeruhi wote ambao wapo kwenye hospitali mbalimbali wapate matibabu yote yanayostahili kwa gharama za Serikali. Avielekeza vyombo vya ulinzi
Aidha, Rais Samia ameelekeza vyombo vya ulinzi na usalama kutoa msaada wa dharura na uokoaji.
Ataka waliopoteza makazi wastiriwe
Aidha, Rais Samia ameelekeza Serikali ya Mkoa na Kitengo cha Maafa cha Ofisi ya Waziri Mkuu kuhakikisha wananchi wote ambao makazi yao yamesombwa na maji wapate makazi ya muda kwa ajili ya kuwastiri wananchi hao.
Maafa haya yameathiri mji wa Katesh hususan vijiji vya Jorodom, Ganana, Katesh na Dumbeta na pia vijiji vya Gendabi, Sarijandu, Arukushay, na Sebasi. Kwa taarifa za awali nyumba na mifugo imeathirika sana huku idadi za kaya zilizoathirika ni 1,150, idadi ya watu walioathirika hadi sasa ni 5,600 na pia ikikadiriwa takriban ekari 750 za mashamba zimeharibika.
Licha ya changamoto kadhaa zilizokuwepo uokoaji unavyoendelea ikiwemo barabara kuharibika, huku tope na magogo kujaa yaliyojaa barabara kuu na mitaani na kusababisha mawasiliano kukatika, yakiondolewa.
Aagiza tathimini
Wakati huo huo Rais Samia ameelekeza tathmini ya kina ifanyike juu ya maafa hayo na vitengo na taasisi zote za Serikali zinazohusika kuwepo eneo la tukio na kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha hali inarejea kawaida.
Majaliwa hatua Hanag
Wakati huo huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewasili wilaya ya Hanang mkoani Manyara na kukutana viongozi wa mkoa huo na wa Serikali na kupokea taarifa ya hali halisi ya tukio la maafa lililotokea jana na kusababisha vifo na majeruhi.
Waziri Mkuu alitoa pole kwa viongozi na wananchi wa Hanang kwenye kikao kilichofanyika jana kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, vyombo vua ulinzi na usalama na Watendaji wa taasisi za Serikali.
Afananisha tukio nwa mwala 1990 Ndanda
Waziri Mkuu alisema tukio la jana linafanana na tukio jingine lililowahi kutokea mwaka 1990 katika eneo la Ndanda ambako mlima uliporomoka na kusomba nyumba na barabara, hali ambayo ilisababisha vifo na majeruhi.
Alizishukuru Kamati za Maafa za Wilaya na Mkoa ambazo zilianza kuchukua hatua za uokoaji tangu jana, lakini pia mawaziri na watendaji wao ambao walikwenda kutoa msaada kwa kuungana na viongozi wa mkoa wa Manyara.
Madaktari bingwa wawasili
Alisema matibabu yanaendelea kutolewa kwa majeruhi ambapo timu ya madaktari bingwa kutoka Dodoma, Singida na Arusha imeungana na kuanza kutoa huduma za upasuaji kwa wagonjwa watatu waliovunjika mifupa.
Alisema majeneza yameagizwa kutoka Babati na Singida ili ndugu waliotambuliwa waweze kuhifadhiwa kwenye nyumba zao za milele.
Ajionea madhara akitumia helikopta
Waziri Mkuu na baadhi ya mawaziri walikagua eneo la Mlima Hanang kwa kutumia helikopta. Eneo hilo ndiko maporomoko ya udongo yalianzia. Baadaye alishiriki kuaga miili ya marehemu.
Makampuni ya simu yatoa milioni 240/-
Wakati huo huo, Umoja wa makampuni ya simu umetoa sh. milioni 240 kwa ajili ya kusaidia kukabiliana na athari za mafuriko hayo. Mbali na kutoa fedha tasilimu, umoja huo umetoa misaada mingine ya kibinadamu kusaidia waathirika wa mafuriko hayo.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa