November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TANESCO wakatieni umeme wanaodaiwa – Biteko

Na Mwandishi Wetu

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kukata umeme kwa wadaiwa wote wasiolipa gharama za kutumia umeme ambapo Shirika hilo linadai jumla  ya Shilingi Bilioni 224 kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali, Binafsi na waliohama na madeni kutoka mita za zamani za umeme kwenda za kisasa hali inayopelekea changamoto katika utekelezaji wa majukumu ya TANESCO.

Amesema hayo tarehe 26 Novemba 2023, wilayani Arumeru mkoani Arusha, wakati alipokagua kituo cha umeme cha Lemuguru mkoani Arusha ambacho ujenzi wake ni sehemu ya mradi  wa ujenzi  wa njia  kuu ya umeme  ya msongo wa kV 400 kutoka Singida mpaka Namanga kuelekea Kenya ( Kenya- Tanzania Power Interconnection Project (KTPIP).

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akitembelea na kukagua Kituo cha Lemuguru ambacho ujenzi wake ni sehemu ya mradi wa ujenzi wa njia kuu ya umeme wenye msongo wa kV 400 kutoka Singida mpaka Namanga kuelekea kenya Kupoza leo Novemba 26, 2023 wilaya ya Arumeru mkoani Arusha

“Hapa Arusha tu, TANESCO anadai wateja wake shilingi Bilioni 7.7, na mara nyingi wanaodaiwa si wanachi wadogowadogo bali Taasisi za Serikali na Wawekezaji wanaojiita wawekezaji wakubwa ambao ukiwakatia umeme wanakwambia unaua ajira,  wepesi wa kujificha kwenye kisingizio cha kulipa kodi na ajira; TANESCO anahitahi fedha ili awekeze na kisha awapelekee umeme wananchi, TANESCO nawaambia kateni umeme kwa mtu yeyote mnayemdai ili mradi unamdai kwa haki.” Amesema Dkt. Biteko

Dkt. Biteko pia ameagiza wadaiwa wote wa madeni ya bili za umeme wakalipe madeni hayo ili zipatikane fedha za kuwahudumia wananchi na ameongeza kuwa, Serikali itaendelea kushughulikia changamoto za umeme nchini kwa aina mbalimbali ikiwemo kuendelea kutekeleza miradi ya uzalishaji umeme ukiwepo wa Julius Nyerere (MW 2115), ambao umefikia asilimia 94 ambapo amesema kuwa, Mkandarasi ameshafunga mashine mbili tayari kwa kuanza majaribio ya kuzalisha umeme.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amekemea vikali watu wote wanaohujumu miundombinu ya umeme akitolea mfano wizi wa shaba na mafuta ambapo kati ya tarehe 25 Novemba, 2023 na 26 Novemba, 2024 kuna matukio 14 katika Ukanda wa Pwani ya kuharibu au kuhujumu miundombinu ya umeme, ambapo ameeleza kuwa, Serikali itawashughulikia kwa kuendesha msako na watakapopatikana sheria itachukua mkondo wake.

Aidha, Dkt. Biteko ameitaka TANESCO kuwasikiliza na kuwapatia majibu kwa haraka wananchi wanaopiga simu kwenye Shirika hilo ili kupata huduma za umeme na mahali penye matatizo waambiwe, “huu utaratibu wa watu kupiga simu anaambiwa subiri, hii tumekubaliana kuwa haiwezekani ikaendelea na ndio maana nimewaambia kituo cha Huduma kwa Mteja tukiimarishe kutoka miito 65 na ziongezwe kufika 100 na zaidi.”

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko akipata maelezo kutoka wa Waratibu wa mradi wa Kituo cha Lemuguru ambacho ujenzi wake ni sehemu ya mradi wa ujenzi wa njia kuu ya umeme wenye msongo wa kV 400 kutoka Singida mpaka Namanga kuelekea kenya Kupoza leo Novemba 26, 2023 wilaya ya Arumeru mkoani Arusha

Dkt. Biteko ametaka Watanzania  kulinda vyanzo vya maji ambavyo vinazalisha umeme, amesema vyanzo hivyo visipolindwa vitapelekea athari mbalimbali zikiwemo kwenye uzalishaji umeme, na pia ameitaka TANESCO kutokukaa nyuma  katika masuala ya utunzaji wa mazingira bali washirikiane na Wizara inayoshughulika na suala la mazingira na NEMC ili wote kwa pamoja washirikiane kusimamia mazingira.

Kuhusu utekelezaji wa kituo hicho cha umeme cha Lemuguru kilichopo wilayani Arumeru Mkoa wa Arusha, Dkt. Biteko amesema kuwa mradi huo ni mkubwa na unagharimu Dola za Marekani milioni 258.8 na kina faida mbalimbali ikiwemo kupelekea wananchi umeme usiokatika mara kwa mara na kituo kitaimarisha hali ya umeme mkoani Kilimanjaro na Arusha.

Dkt.Biteko vilevile ameipongeza TANESCO kwa hatua mbalimbali inazochukua ili kupunguza makali ya mgawo wa umeme pamoja na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa kuongeza kiwango cha Gesi Asilia kinachozalisha umeme.

Sehemu ya mitambo ya umeme katika Kituo cha Lemuguru ambacho ujenzi wake ni sehemu ya mradi wa ujenzi wa njia kuu ya umeme wenye msongo wa kV 400 kutoka Singida mpaka Namanga kuelekea kenya Kupoza leo Novemba 26, 2023 wilaya ya Arumeru mkoani Arusha.

Awali, akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa njia Kuu ya kusafirisha umeme wenye msongo wa Kilovoti 400 kutoka Singida hadi Namanga kuelekea Kenya, Msimamizi wa Mradi huo Mhandisi Peter Kigadye, amesema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuongeza uwezo wa kusafirisha umeme kwenda mikoani na migodi ya uchimbaji madini na hivyo kuwezesha kufikia uwezo wa juu wa megawati 2000 katika kusafirisha umeme.

Amesema, utekelezaji wa mradi unahusisha vipengele Sita  ikiwemo ujenzi wa njia 8 za laini ya kV 400/33 kutoka Kituo kipya cha kupoza umeme, ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kV 400 kutoka Singida hadi Namanga kupitia Arusha yenye urefu wa kilomita 414.3, Babati -Arusha kilomita 150, Arush –Namanga, Kilomita 114.3 ambao umefikia asilimia 96.

Ameeleza mradi huo pia unahusisha, upanuzi wa vituo vya kupoza umeme ambao umefikia asilimia 98.72, mradi wa usambazaji umeme kwa vijiji vilivyopitiwa na mradi vijiji na ujenzi wa vituo vyq kupoza umeme vya Dodoma, Singida, ambavyo vimekamilika.