Na Julius Konala, Timesmajira Online Ruvuma
ASASI isiyo ya kiserikali ya Hoja Project Tanzania yenye makao yake makuu mjini Songea Mkoani Ruvuma, ipo mbioni kuanzisha mashindano ya soka yatakayoshirikisha timu zaidi ya 15 kutoka Wilaya ya Nyasa lengo likiwa ni kuibua vijana wenye vipaji ili waweze kusajiliwa na timu ya Hoja FC.
Awali mashindano hayo yalipangwa kufanyika mapema lakini kutokana na Taifa kukumbwa na mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu Covid-19 na Serikali kusimamisha shughuli zote za michezo nao walisitisha kila kitu hadi pale Rais John Magufuli aliporuhusu shughuli hizo kuendelea kama kawaida lakini wakitakiwa kufuata Muongozo wa Afya Michezoni uliotolewa na Wizara ya Afya pamoja na Michezo kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
Mkurugenzi wa asasi hiyo, Oswin Mahundi ameuambia mtandao wa Timesmajira katika mahojiano maalum kuwa, katika mashindano yatakayoanza mwezi huu Wilayani Nyasa zawadi zitakuwa Sh. 500,000 kwa mshindi wa kwanza, Sh. 300,000 kwa mshindi wa pili na shilingi Sh. 200,000 kwa mshindi wa tatu.
Shindano hilo pia litakwenda sanjari na utoaji wa elimu juu ya kupambana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu Covid-19, malaria pamoja na ugonjwa wa upungufu wa kinga mwilini wa Ukimwi(HIV)
“Sababu nyingine ya kuanzisha mashindano hayo ni kutaka kuwajenga kiafya na kiakili vijana lakini pia yatawasaidia kuepukana na mambo yasiyofaa ndani ya jamii ikiwemo kujiingiza kwenye vitendo vya matumizi ya dawa za kulevya pamoja na ngono zembe, ” amesema Mahundi.
Hata hivyo kiongozi huyo amesema, asasi yao imekuwa ikishindanisha timu mbalimbali kwa ajili ya kusaka vijana wenye vipaji ambao watasaidia kukiongezea nguvu kikosi chao katika mashindano mbalimbali ndani ya Mkoa.
Kwa sasa timu hiyo ya Hoja FC inashiriki Ligi daraja la tatu lakini mipango yao ni kujiimarisha zaidi ili kuwa na kikosi bora kitakachoweza kupambana na kuipandisha timu hizo hadi kufikia kucheza Ligi Kuu.
More Stories
Watumishi wa Fahari wafanya Bonanza
Rais Samia atia mkono mchezo wa masumbwi Tanzania
Chino bingwa mpya wa IBA Intercontinental Championship