December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Madiwani watakiwa kusaidia ukusanyaji mapato

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Lushoto

MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga Mathew Mbaruku amewataka Madiwani kuhakikisha wanawaelimisha wananchi juu ya ulipaji kodi na ushuru, kwani makusanyo hayo ndiyo yatawasaidia kupata fedha za miradi ya maendeleo kwenye vijiji vyao.

Ameyasema hayo kwenye Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo kikiwa ni kikao cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/2024.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga Mathew Mbaruku akizungumza kwenye Baraza la Madiwani. Wengine ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Lushoto Ali Daffa (kushoto), na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Ikupa Mwasyoge

Mbaruku amesema mapato ya ndani ni kipaumbele cha kwanza cha halmashauri hiyo na madiwani wamekuwa wanalalamika kuwa miradi yao hasa maboma ya zahanati na madarasa yaliyojengwa na wananchi yameshindwa kukamilika

Lakini kama mapato hayo yatakusanywa, halmashauri inaweza kukamilisha maboma hayo na miradi ya afya na elimu,

“Diwani ukiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kata (WDC) unatakiwa usimamie mapato ili kuweza kufikia malengo na ikibidi kuvuka lengo,kata zote zina POS (Mashine za kielektroniki za kukusanya mapato), hivyo diwani yeyote akiona POS iliyopo kwenye kata yake haifanyi kazi, awasiliane na mimi,”amesema Mbaruku.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Ikupa Mwasyoge akizungumza kwenye Baraza la Madiwani.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Lushoto Ali Daffa, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto na Serikali kwa kukamilisha jengo la mama na mtoto lililojengwa kwenye hospitali ya Wilaya ya Lushoto ambalo ni jengo hilo ni mkombozi kwa wanawake na watoto wa Wilaya hiyo na maeneo mengine.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mara baada ya kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Ikupa Mwasyoge amesema wamevuka lengo la ukusanyaji mapato ya ndani kwa kuweza kukusanya kiasi cha zaidi ya milioni 976.2sawa na asilimia 34.65 kwa miezi mitatu ya Julai hadi Septemba kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

” Kwenye bajeti yetu ya mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha 2023/2024 tulipanga kukusanya zaidi ya bilioni 2.8 lakini kuanzia Julai hadi Septemba, 2023 tumeweza kukusanya zaidi ya milioni 976.2 sawa na asilimia 34.65. Niwaombe madiwani, watendaji na wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwenye ukusanyaji wa mapato ya halmashauri ili tuendelee kutoa huduma,” amesema Mwasyoge.

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto wakiwa kwenye kikao

Mwasyoge amewataka watendaji watumie mifumo ya malipo ya serikali kwenye ukusanyaji mapato, na ndani ya saa 24 wawe wamepeleka fedha hizo benki.

Wakuu wa Idara na Vitengo, vyama vya siasa na Maofisa Tarafa wakiwa kwenye Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto