November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kyela Ibasa kutoa zaidi ya kadi 600 bima ya afya

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

Umoja wa wazawa wa Kyela waishio ndani na nje ya nchi umejipanga kugusa maisha ya wananchi wa wilaya hiyo iliyopo mkoani Mbeya kwa kutoa bima za afya kwa zaidi ya wananchi 600, kupitia tamasha la Kyela Ibasa (Ibasa Festival).

Sambamba na kutoa madawati kwa shule zenye uhaba, kuenzi utamaduni, kutembelea vivutio vya utalii pamoja na burudani mbalimbali ikiwa ni sehemu ya kurudisha fadhila kwa jamii yao ambayo imewasaidia kupigia hatua mbalimbali ya maisha.

Katibu wa Ibasa Festival, Nicholaus Mwangomo, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari amesema ni msimu wa tano sasa tangu kuanzishwa kwa tamasha hilo ambalo limekuwa likiwakutanisha wanaKyela wanaoishi maeneo mbalimbali kurudi wilayani humo kila mwisho wa mwaka kusherehekea na kujumuika pamoja na ndugu na jamaa zao.

“Tumekuwa tukiyagusa makundi mbalimbali wakiwemo wanaoishi kwenye mazingira magumu kwa kuwapatia bima za afya ili wawe na uhakika wa kupata huduma za matibabu, utoaji wa madawati ili kusaidia watoto kusoma kwa utulivu pamoja na kuinua uchumi wa Kyela kupitia shughuli za utalii, burudani na michezo tunayoandaa,” amesema Mwangomo.

Mtunza Hazina wa Ibasa Festival, Lufingo Mwakilasa, amesema katika michango waliyoitoa wanachama asilimia 40 itaenda kwa jamii ili kusaidia uboreshaji wa huduma za afya na elimu.

Mratibu wa Tamasha hilo, Pablo Kais, amesema furaha yao ni kuwa sehemu ya kuisaidia jamii na kwamba wataendelea kufanya hivyo kama sehemu ya kurudisha fadhila.

Kyela Ibasa Festival iliasisiwa mwaka 2019 likiwa na maono ya kuisaidia jamii ya Kyela katika nyanja ya elimu, afya, uchumi na utamaduni.