Na Heri Shaaban, TimesMajira Online
Wakazi 1865 wanaopisha upanuzi wa Uwanja Ndege wa Julius Nyerere wameangua kilio na kumuomba Rais Samia Suluhu Hassan walipwe fidia zao wapishe eneo hilo.
Wananchi hao walitoa vilio vyao jana huku wakinyeshewa na mvua mbele ya Mbunge wao wa Jimbo la Segerea, Bonah Ladslaus Kamoli, wakiitaka Wizara ya Fedha kuwalipa fidia zao waweze kupisha eneo hilo .
Mkutano huo wa adhara Kipunguni uliandaliwa na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kipunguni, Mwinjuma Seke kujadili mustakabali wa malipo yao.
Akizungumza katika mkutano huo mmoja wa wananchi wa Mtaa wa Kipunguni, Beatrice Kimanga, alisema tathmini mpya ya Serikali ilifanyika Julai 2022 lakini mpaka sasa Wizara ya fedha haijawalipa na wao wako tayari kuondoka.
Beatrice alisema masikitiko yao mpaka sasa hawajui kinachoendelea huku haki zao zikicheleweshwa na kusisitiza hakuna mtu anayekataa kulipwa wapo tayari kulipwa kuondoka eneo hilo.
“Tunakuomba Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mbunge wetu wa jimbo la Segerea kutupigania, tunaomba mpokee kilio chetu wananchi wa Kipunguni Kata ya Kipawa tumekubali kuondoka tupewe fedha zetu tukajenge maeneo mengine.
“Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Mchemba alifanya ziara kuja kuongea na sisi mpaka leo utekelezaji bado, Serikali yetu sikivu mtutazame kwa jicho la karibu, usalama wetu ni mdogo wezi wamekuwa wengi,” alisema Beatrice.
Mkazi mwingibe Aseri Simon Anael, alisema tathmini ya mwaka 1997 ilikuwa ya ubabaishaji lakini Rais Samia alielekeza ifanyike upya kwa kutumia sheria ya sasa lakini tangu ilipofanyika mwaka jana mpaka sasa zoezi linasuasua na kumuomba kuingilia kati.
Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Ladslaus Kamoli, alisema kuna watu walipewa viwanja ndio walichelewesha zoezi hilo ambao walipewa Majohe na Msongola.
Aliwataka wananchi wanaotaka viwanja waandike majina kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa na wasiotaka pia waandike pamoja na wale walioendeleza maeneo yao.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Kipunguni, Mwijuma Seke, alisema wanaohitaji viwanja vya Serikali watachukua na wasiohitaji watarejesha na kwamba hawana mgogoro tena na wala hakuna mwananchi aliyepinga malipo.
Alisema Mtaa wa Kipunguni wapo tayari kwa malipo na watu waliozika makaburi ya eneo hilo waende kujiandikisha walipwe waweze kuyahamisha.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa