November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bilioni 1.4 yajenga ofisi ya RPC

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online,Mara

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Jumanne Sagini amefanya ziara ya kutembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa jengo la ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara katika eneo la Manispaa ya Musoma wenye thamani ya bilioni 1.4.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini (Kushoto), akikagua mradi wa ujenzi wa jengo la ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara linalojengwa katika eneo la Manispaa ya Musoma wenye thamani ya shilingi Bilioni 1.4

Akizungumza baada ya kukagua mradi huo Sagini amesema kuwa, ukikamilika utaipa heshima na hadhi ofisi ya Kamanda wa Polisi kwani kila Kitengo kitakuwa na ofisi yake tofauti na ilivyo kuwa sasa.

“Serikali ni sikivu na nimearifiwa kuwa, fedha za awamu ya pili na tatu tayari zimetoka hivyo basi nimuombe mkandarasi kukamilisha ujenzi kama inavyoelekeza ili ofisi ianze kutumika,” amesema.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini (wa pili kushoto), Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara ACP Salim Morcase (wa pili kulia), pamoja na Maofisa wengine wa Jeshi hilo kwenye picha ya pamoja baada ya kukagua Mradi wa jenzi wa jengo la ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara ACP.Salim Morcase, amemshukuru Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Wizara kwa ufuatiliaji wa karibu wa mradi wa ujenzi

“Sisi kama Jeshi la Polisi kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchi tunatoa shukurani zetu za dhati kwa Serikali, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na kwako kwa ufuatiliaji wa karibu wa mradi wa ujenzi wa jengo letu,”amesema ACP. Morcase.

Aidha, amebainisha kuwa, utekelezaji wa mradi huo mpaka sasa umefikia asilimia 92 na ulianza kutekelezwa Novemba 18, 2021 unakadiriwa kumalizika mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka 2023.

Muonekano wa Jengo la Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara linalojengwa katika eneo la Manispaa ya Musoma lenye thamani ya bilioni 1.4.