-Ni kwa kufanikisha Miswada ya Sheria ya Tume ya Uchaguzi na Muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa kutua Bungeni,watoa ya moyoni
Na Penina Maulundo, TimesMajira Online
WASHIRIKI wa Kongamano la Mjadala wa Kitaifa la lililojadili Muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi pamoja na Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa ambayo imewasilishwa Bungeni kwa mara ya kwanza Novemba 10, mwaka huu wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha hatua hiyo, ambayo ilishindikana kwa miaka mingi.
Wameenda mbali zaidi wakisema muswada huo umeleta matumaini mapya katika mchakato mzima wa uchaguzi na vyama vya siasa hapa nchini.
Pia wamepongeza mapendekezo yaliyomo kwenye muswada huo wa sheria, huku wakishauri kundelea kufanyika kwa maboresho kwenye baadhi ya maeneo ikiwemo suala la Tume ya Uchaguzi kusimama peke yake na sheria yake.
Maeneo mengine ni Ushiriki wa Viti Maalum kwa wanawake, Usawa wa Kijinsia katika vyama vya siasa.
Washiriki hao wametoa pongezi na ushauri wao jana jijini Dar es Salaam wakati Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye kongamano hilo lililofanyika kwa njia ya mtandao (Zoom).
Majadiliano hayo yamehusisha viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa ,wanasheria wabobezi, viongozi wa dini, wawakilishi viongozi, makundi ya vijana pamoja na waandishi wa habari.
Wamesema Rais Samia ameweza kuhakikisha demokrasia inasimamiwa kikamilifu nchini na kwa kuonesha ni namna gani vyama vya siasa vitakuwa huru kufanya kazi zake.
Mwenyekiti Taifa wa Chama cha ADC Alliance, Hamad Rashid, amemshukuru Rais Samia kwa utashi wake wa kisiasa kuweza kufikia hatua ya kupatikana kwa muswada huo kwa kutumia Kamati aliyoiteua.
Amesema kwa mara ya kwanza Tanzania inaelekea kupata fursa ya kuona Tume ya uchaguzi inatoa fursa kwa wajumbe wake kupitia utaratibu angalau wa kuchujwa kabla ya kupelekwa kutangazwa.
Amesema hii ni hatua muhimu ambayo haikutegemewa na hata miaka ya nyuma haikuwepo, lakini kwa namna ambavyo Rais Samia amekuwa na utashi wa jambo hilo, ameweza kufanya jambo jema.
“Mimi niliyebahatika kuwepo katika awamu zote za Serikali na kwnye vyama vya siasa nimeshuhudia chaguzi mbalimbali kwenye mfumo wa chama kimoja au vyama viwili, lakini kwa hatua hii nimeona namna nzuri ambazo zimeanza kuchukuliwa kuhakikisha demokrasia ya siasa inapatikana,”amesema na kuongeza;
“Tanzania inapiga hatua kubwa katika suala la demokrasia ukizingatia suala zima la Katiba, usalama, amani na utulivu katika nchi yetu, pia nampongeza Rais Samia kwa kuunda kikosi kazi ambacho kimepokea mawazo mbalimbali na michango ya wadau na hatimaye kuyafanyia kazi,”
Kwa upande wake Mbunge wa Viti maalum, Neema Lungangilwa amempongeza Rais Samia kwa kuunda Kamati ya Kufanya Tathimini ya Vyama vya Siasa nchini na kupokea mapendekezo, ambapo tayari matunda yake yameanza kuonekana.
Amesema Watanzania wanapaswa kutambua kuwa Serikali chini ya Rais Samia imefanyia kazi mapendekezo ya kikosi kazi kwa kiwango kikubwa, ikiwemo katika eneo la usawa wa kijinsia, kuwekwa kwa kifungu kipya ambacho kinasema kila chama cha siasa katika shughuli zake zote kinapaswa kuzingatia usawa wa kijinsia, ikiwemo ujumuishaji wa makundi maalum, vijana, wanawake na watu wenye uhitaji maalum.
Kwa upande wake Joseph Selasini amesema angependa sheria itamke Tume ya Uchaguzi iwe huru. “Na sio tume ya uchaguzi pekee, Sheria itambue kabisa kuwa ni tume huru na kwa sababu hiyo wajumbe wa tume hiyo watambulike kisheria na sheria iwalinde nje na ndani ya tume,”amesema.
Kuhusu viti maalum, amesema visiwe vya akina mama fulani ambao wamekuwa wakijimilikisha nafasi hizo kama mali zao, kwani mara nyingi kunakuwa na upendeleo mwingi.
“Lazma viti maalum vijulikane, wanapoingia wanakaa muda gani, kwani inaonekana watu hao hawafanyi kazi majimboni,
hivyo ni vema kuweka utaratibu wa akinamama hao kuwa wanachaguliwa kwa mtindo fulani,” amesema Selasini na kuongeza;
“Nampongeza Rais Samia kwa hatua hii amedhubutu, tusilalamike tu, lazima tuunge mkono na kutoa mapendekezo ya kusaidia tusione upande hasi tu, hiki kitu kimeletwa ili kuleta manufaa
kwa nchi yetu, hivyo ni vema kuchangia mawazo yetu,”amesema.
Naye Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Haji Duni alisema, amesema kwa sasa kuna mazuri yaliyorekebishwa katika sheria.
“Nampongeza Rais Samia kuchukua hatua ingawa tuna safari ndefu kwenye sheria ya vyama vingi, pia tuhakikishe kuna udhibiti fedha za uchaguzi,”amesema na kuongeza;
“Tatizo lisilokuwa wazi juu ya sheria ya Polisi ndio tulitegemea sheria ifanyiwa marekebisho, wanachama na wanasiana kufanya mikutano yao kwa amani kwani Jeshi la Polisi linatumia sheria ya Mwaka 1973 ambayo ilikuwa inatazamia chama kimoja”amesema.
Pia amesema kwa ujumla mambo sio mabaya katika sheria hiyo, lakini linapokuja suala la kushinda, Rais ashinde kwa asilimia zaidi ya 50 na sio 38 hakuna sababu ya kuogopa.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa