Na Mwandishi wetu, Dodoma.
TANZANIA imefungua milango ya uwekezaji katika Sekta ya Madini kwa nchi ya Korea ya Kusini ikiwemo kuendeleza ushirikiano wa kikazi ili kufanikisha utekelezaji wa mikakati ya malengo (Vision) 2030 yenye kauli mbiu ya Madini Maisha na Utajiri.
Hayo yamesemwa Novemba 8, 2023 na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde wakati wa mazungumzo ya ushirikiano wa kisekta baina ya Tanzania na Jamhuri ya Watu wa Korea Kusini yaliyofanyika jijini Dodoma.
Wakati akizungumza na ujumbe huo kuhusu uwepo wa madini, Mavunde amesema kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na madini ya aina mbalimbali, yakiwemo madini mkakati kama vile madini ya kinywe, lithium,nibioum na makaa ya mawe ambayo kwa sasa mataifa mengi yanatafuta kuwekeza huko kutokana na mabadiliko ya tabianchi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Mavunde amezikaribisha kampuni mbalimbali kutoka Korea ya Kusini kuja kuwekeza nchini hapa na kuwaeleza kuwa kwa sasa sekta ya madini nchini Tanzania ipo na malengo 2030, ambayo lengo lake ni kupata taarifa za utafiti ambazo zitatoa dira ya uwekezaji na uendelezaji kwa kufungamanisha sekta za kiuchumi.
Akielezea kuhusu kufungua kiwanda cha uchakataji madini ya kinywe na uongezaji thamani madini nchini hapa Mkurugenzi wa Kampuni ya POSCO ya nchini Korea, Ji Ki Chun amesema, baada ya kukamilisha uchimbaji wa madini ya kinywe wilayani Mahenge watafungua kiwanda cha kuchakata madini ghafi ya Kinywe na uongezaji thamani kabla ya kusafirisha nje ya nchi.
Chun amefafanua kuwa menejimenti ya POSCO imeridhika na hali ya miundombinu nchini ikiwemo reli ya kati pamoja ujenzi wa SGR.
Naye, Balozi wa Korea ya Kusini nchini Tanzania, Kim Sumpyo ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuimarisha uhusiano mzuri wa kiuchumi na serikali ya Korea Kusini amebainisha kuwa nchi hiyo ina mkataba wa hiyari katika ushirikiano wa kikazi ndani ya sekta ya madini hivyo itaendelea kutoa ushirikiano katika uwekezaji.
Balozi Sumpyo ameongeza kuwa mazingira salama na sera nzuri zinavutia wawekezaji wetu na kuahidi kuendelea kuwaleta wawekezaji wengi kutoka nchini Korea Kusini kuja kuwekeza nchini hapa.
Awali, akifungua mazungumzo hayo ya ushirikiano Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali ameimshukuru Balozi wa Korea Kusini nchini Tanzania kwa uwekezaji mzuri katika sekta ya madini akitolea mfano uwekezaji katika madini ya Kinywe wilayani Mahenge.
Mahimbali amemuomba Balozi Sumpyo kuendeleza ushirikiana na kubadilishana uzoefu wa kisekta baina ya wataalam wa Korea kusini na wataalam wa sekta ya madini Tanzania.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi