November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof. Kitila Mkumbo afunguka utendaji wa Rais Samia

Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOnline, Dodoma

WAZIRI wa Nchi katika Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amewasilisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2024/25, huku akichambua utendaji wa Rais Samia Suluhu Hassan, akisema kama nchi tunaye kiongozi mkuu wa nchi makini aliyeonesha weledi na kuthibitisha uadilifu na uzalendo wa hali ya juu kwa nchi yake

“Zaidi ya yote amethibitisha kuwa kiongozi muungwana na mpenda haki. Kupitia falsafa yake ya 4R, amejenga maridhiano mapana ya kijamii na kisiasa na kuweka mazingira sawia ya kufanya siasa kwa vyama vyote nchini (R1 =Reconciliation).”

Profesa Kitila ametoa kauli hiyo Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2024/25 ikiwa ni mara yake ya kwanza.

“Kiongozi wetu ameleta mageuzi makubwa katika kuweka mazingira bora ya biashara na uwekezaji (R3 = Reform). Amefufua sekta za kilimo, mifugo, uvuvi na madini na kuwapa matumaini mapya mamilioni ya wakulima, wafugaji, wavuvi na wachimbaji wadogo wa madini.

Hakika anaijenga upya nchi yetu (R4 =Rebuilding) na kupitia uongozi wake, Serikali na nchi yetu ipo salama. Naam, hapa ninamzungumzia Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesema Profesa Mkumbo na kuongeza;

“Ni wazi kuwa sisi kama nchi tuna mahitaji mengi lakini raslimali tulizo nazo zina kikomo. Kwa sababu hii tunawajibika kuchagua tufanye lipi leo na lipi tulifanye baadaye.

Hii ndiyo maana ya kupanga. Kupanga ni kuchagua. Katika kupanga tutazingatia vipaumbele vya kimkakati kwa kuzingatia dunia inataka nini na sisi tunaweza kutoa nini.” Prof. Kitila.

Aidha, Prof Kitila ameainisha hatua saba zitakazochukuliwa na Serikali ya Rais Samia kuchochea na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii vijijini, ambapo asilimia 65.1 wanaishi kwenye maeneo hayo nchini.

Profesa Mkumbo ameanisha hatua hizo Bungeni jana jijini Dodoma wakari akiwasilisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2024/25.

Ametaja baadhi ya hatua hizo kuwa ni kuendelea kuwawezesha wakulima kuongeza uzalishaji, ikiwa ni pamoja na kuendelea kuwapatia wakulima wadogo mbegu bora na mbolea kwa bei ya ruzuku na kuendelea kupanua na kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji.

Profesa Kitila ametaja hatua nyingine ni Serikali kutumia sera za kifedha na kikodi ili kuvutia wawekezaji katika maeneo ya vijijini ili mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na misitu yatoke vijijini yakiwa yameanza kufanyiwa uchakataji wa awali.

Amesema viwanda vya vijijini vitabakisha thamani kubwa kijijini na kutoa nafasi ya ajira kwa vijana na wanawake ambao wengi wao sasa wana elimu ya sekondari.

Kwa mujibu wa profesa Mkumbo katika hatua hii, watahitaji kulipanga upya shirika la Viwanda Vidogo nchini (SIDO).

Ametaja hatua kuendelea kupanua na kuboresha miundombinu ya huduma za afya, elimu, maji na umeme na kuhakikisha kuwa angalau asilimia 30 ya wananchi vijijini wanakuwa na bima ya afya ifikapo mwaka 2025.

“Kuweka mkazo wa pekee katika kuimarisha ubora wa elimu, hususani katika kuhakikisha kuwa shule za vijijini zina walimu wa kutosha na kuunganishwa katika miundombinu ya kidigitali,”alisema.

Ametaja hatua nyingine ni kuzingatia umuhimu wa dijitali katika kuleta mapinduzi ya uchumi vijijini, ninapendekeza kujenga mfumo wa dijitali vijijini ili kuwaunganisha wananchi vijijini katika uchumi wa taifa na kuongeza matumizi ya Tehama katika shughuli za kiuchumi na kijamii.

Amesema hatua hiyo itaiwezesha Serikali kuwa karibu zaidi na wananchi, kusaidia katika mapambano ya rushwa, kuimarisha demokrasia na utawala bora.

Alisema kupitia upya sera za fedha, sheria na kanuni zinazosimamia mikopo kwa lengo la kuzisukuma taasisi za kifedha kuelekeza mikopo katika sekta ya kilimo, ufugaji, uvuvi na wachimbaji wadogo wa madini.

Ajira zilizotokana na miradi Profesa Mkumbo alisema jumla ya ajira 160,107 zimezalishwa kutokana na miradi 883 iliyowekezwa nchini katika kipindi cha kati ya Juni 2021 na Septemba 2023.

Amesema katika kukuza biashara na uwekezaji pamoja na hatua zingine, Serikali iliendelea kuweka mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji ambapo miradi hiyo ilikuwa na thamani ya Dola za Marekani yenye milioni 12,154 ilisajiliwa katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).