Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Korogwe
MAMENEJA wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wa mikoa na Wilaya watapimwa utendaji kazi wao siyo kwa kuwa na miradi mingi kwenye maeneo yao bali kwa kufikisha maji ya bomba kwa wananchi.
Angalizo hilo limetolewa na Mkurugenzi wa Huduma ya Usambazaji Maji Vijijini kutoka RUWASA Makao Makuu, Mkama Bwire wakati akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa maji na vyombo vya watoa huduma ya maji ngazi ya jamii (CBWSO’s) Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga uliofanyika mjini Korogwe.
“Kipimo cha utendaji kazi kwa Meneja wa RUWASA Wilaya au Mkoa ni maji kutoka bombani,hivyo hatuangalii Meneja ameweka au anatekeleza miradi mingapi kwenye wilaya yake au mkoa wake, bali ni kuona maji bombani, na wananchi wanayapata,”amesema Bwire.
Bwire amesema adhima ya serikali ni kuona ifikapo mwaka 2025, asilimia 85 ya wananchi vijijini wanapata maji na mwaka 2030, wananchi wote wanapata maji huku RUWASA imefanikiwa kuongeza vijiji vinavyopata huduma ya maji.Ambapo tangu mwaka 2019, wananchi vijijini wanapata maji kwa asilimia 68.4 huku nia ikiwa ni kufikia asilimia 77 ifikapo Desemba, mwaka huu.
“Kuongezeka kwa idadi ya vijiji vinavyopata huduma ya maji kutoka 7,082 mwaka 2019/2020 hadi kufikia vijiji 9,670 sawa na asilimia 78 kati ya vijiji 12,318 nchini,kuongezeka kwa vituo vya kuchotea maji kutoka 86,780 Juni 2019 hadi kufika vituo 144,010 Desemba 2022,kupungua kwa vituo vya kuchotea maji visivyofanya kazi kutoka asilimia 23 Julai 2019 hadi kufikia asilimia 14 Juni 2023,” amesema Bwire na kuongeza kuwa
“Kukwamuliwa kwa miradi 159 sawa na asilimia 89 kati ya miradi 177 iliyorithiwa kutoka LGAs iliyokuwa na changamoto ya utoaji wa huduma ya maji,kuongeza maunganisho ya nyumbani kutoka 157,201 Julai 2019 kufikia 184,360 kufikia Juni 2023,mbauti 68 zimejengwa kuhudumia mifugo,”.
Bwire amesema ili wawe na mfumo imara wa kitaasisi ni lazima kiwepo chombo cha Kamati ya Maji ambacho kitasimamia wataalamu ili kufanya kazi kwa weledi na ukamilifu.
Kwani kamati hizo zitasimamia miradi iliyokamilika na kutoa huduma ya maji na kuiacha RUWASA ikiendelea kujenga miradi mipya kwa maeneo mapya yasiyokuwa na miradi.
“Huduma ya maji endelevu RUWASA ilifanikiwa kuunda jumla ya CBWSOs 2,328 ambazo zimeajiri wataalam 6,051 kati yao mafundi 2,102, wahasibu 1,743,walinzi na wasaidizi wa ofisi 2,206 katika mwaka 2022/23, RUWASA imefanikiwa kutengeneza ajira 5,209 kupitia miradi ya maji inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali vijijini,”amesema Bwire.
Bwire amesema moja ya changamoto ni wananchi waliopo vijijini kujenga nyumba kwa mtawanyiko, jambo hilo ni changamoto kwa wao kupata huduma za jamii ikiwemo maji. Hivyo wanakwenda kujenga miradi ya maji wakielewa changamoto kama hizo pia wanaelewa vijiji vinakuwa, hivyo miradi yao inajengwa kwa kuangalia miaka mitano hadi 20 ijayo.
Mratibu wa CBWSO’s Mkoa wa Tanga Hans Mwiyola amesema RUWASA Wilaya ya Korogwe hadi sasa ina jumla ya CBWSO’s 11 huku Wilaya hiyo ikiwa na vijiji 122, ambapo kati ya hivyo, vijiji vinavyopata huduma ya maji kutoka RUWASA ni 92.
Huku vijiji ambavyo havipati huduma ya maji ni 30, wakati idadi ya wakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe ni 272,976 na waliofikiwa na huduma ya maji ni asilimia 64.
Mwiyola amesema CBWSO’s Wilaya ya Korogwe zimepata mafanikio kwani jumla ya makusanyo kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/2024 ni zaidi ya milioni 61 huku matumizi yakiwa ni zaidi ya milioni 51 huku kiasi cha zaidi ya milioni 18 kimebaki.
Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini Timotheo Mnzava amesema jamii ijengewe utamaduni wa kuviona vyombo vya watumia maji ni vya kwao, hivyo wataweza kuchangia na miradi hiyo kuwa endelevu.
Akifunga mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Korogwe William Mwakilema aliwataka watendaji wa kata, na viongozi wengine kwenye ngazi ya vijiji na kata kulinda vyanzo vya maji, miradi ya maji na mapato yatokanayo na maji.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mkutano huo, Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo amesema CBWSO’s kwenye mkoa huo zimeonesha mafanikio makubwa katika kutoa huduma kwa wananchi,matumaini yake wananchi wameanza kuelewa namna ya kulipa huduma ya maji ili iwe endelevu.
Hata hivyo Meneja wa RUWASA Wilaya ya Korogwe Mhandisi William Tupa amesema wanafanya mikutano kama hiyo ili kuwasaidia viongozi wa Serikali kuanzia ngazi ya wilaya hadi vijiji waweze kujua muundo mpya wa uundaji vyombo vya watumia maji, kwani itasaidia kuelimisha wananchi ili waelewe adhima ya Serikali kwenye huduma ya maji.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â