November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kuwajengea uwezo wanaume kutambua umuhimu wa wanawake

Na George Mwigulu, Timesmajira Online,Katavi

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe Mkoa wa Katavi, Shamimu Mwariko amesema serikali inaendelea kuwajengea uwezo wanaume kutambua umuhimu wa wanawake na wasichana kushirikishwa kwenye masuala ya uchumi ili kufikia lengo la usawa wa kijisia kwenye uchumi.

Hayo yamesema October 25 mwaka huu kwenye maonesho ya Wiki ya Mwanakatavi katika viwanja vya CCM Azimio Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi wakati Mkurugenzi huyo akizungumzia mipango ya serikali inayofanya ya kutengeneza mazingira wezeshezi ya kumwinua mwanamke na msichana.

Shamimu amesema kuwa kuanzia ngazi ya familia wanaume wanatakiwa kugatua mamlaka yao na kuyahamisha kwa wanawake ili kuwapa uwezo wa kujiamini kupigania familia zao kiuchumi hususani kuwa na uwezo wa kuendesha mitambo ya teknolojia kwenye sekta ya kilimo ambapo ni nguzo kwenye ustawi wa uchumi wa kisasa.

“Wiki iliyopita tulikuwa na wiki ya Wanawake vijijini ambayo ililenga kujenga uelewa na uwezo wa wanawake kutambua fursa zilizopo kwenye maeneo yao,kuweka mazigira wezeshi kwa wanawake kutambua fursa zilizopo za umilki wa ardhi pamoja na uwezo wa kuendesha mitambo ya teknolojia bali kumilki teknolojia hizo,”amesema

Ameeleza kuwa halmashauri hiyo ina mchanganyiko wa makabila mengi yenye mila na desturi mbalimbali ambapo wanatumia nguvu ya ziada kuhakikisha wanaelewa na kuvunja vikwazo vya kitamaduni ili mwanamke aweze kumilki ardhi.

“Mwanamke wa kijijini ni muhimu sana katika suala la ardhi aweze na yeye kuhudumia familia yake na ikitokea mwenza wake amefariki dunia au kuachana asipate tabu,”.

Amefafanua kuwa nchi imetoka kwenye umasikini na iko kwenye uchumi wa kati ambapo katika jitihada za kuongeza uzalishaji mali na mwanamke asibaki nyuma bali anapaswa kushiriki.

“Tunatambua kwa sasa serikali inafanya maboresha kadhaa kwenye mikopo ya asilimia kumi ya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu yatakapo kamilika makundi haya yanafahamika na sisi tutahamasisha wanawake wakuchukue mitaji mikubwa kwani tunawafuatilia kuhakikisha kwamba wanaweza kuanzisha viwanda vidogo,” amesisitiza Mkurugenzi huyo.

Aidha ametoa wito kwa wanawake na wasichana wa vijijini ambao wako nyuma licha ya hamasa mbalimbali kupatiwa na mazingira wezeshi wanapaswa kuamka kwenye kutafuta fursa na jamii iko tayari kuwapokea na kuwatia moyo kuinua uchumi wao.

Mrisho Kabwe,Mkazi wa Kijiji cha Kibaoni amesema kuwa jamii kwa kiasi kikubwa imeondokana na tabia ya kukandamiza mwanamke kiuchumi baada ya kutambua kuwa ni mwaminifu kwenye usimamizi wa uchumi.

Ametoa wito kwa jamii ya Mkoa wa Katavi kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo kwenye maonesha ya wiki ya Mwanakatavi ili waweze kuwa na uwezo mkubwa wa uchumi.