November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wahitimu st mary’s waahidi makubwa kidato cha nne

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online DSM

CHUO cha Elimu ya Biashara (CBE) kimeahidi kuiunganisha shule ya St Mary’s Mbezi Beach na Maktaba Kuu ya Taifa ili wanafunzi wa shule hiyo wapate fursa ya kusoma vitabu mbalimbali kwa namna rahisi.

Ahadi hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Kampasi ya Mwanza, Dk Robert Mashenene, wakati akizungumza kwenye mahafali ya 22 ya shule ya sekondari St Mary’s.

Amesema vitabu ni nyenzo muhimu kwa wanafunzi hivyo atafanya jitihada ili ndani ya muda mfupi shule hiyo iwe imeunganishwa na maktaba kuu ya taifa na kuanza kunufaika na vitabu vinavyopatikana ndani ya maktaba zake.

“Na katika kuwaunganisha kuna gharama huwa zinahitajika nawaahidi kwamba hizo gharama nitatoa mimi kwasababu nataka wanafunzi wetu wanufaike na fursa ya vitabu vinavyopatikana pale,” amesema

Kadhalika, amezitaka shule nchini kuwekeza kwenye Tekmolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na maabara za kisasa ili kulisaidia taifa kupata wataalamu wengi kufanyakazi kwenye sekta ya uhandisi.

“Dunia inakwenda kasi sana kwa hiyo tunavyozidi kuingia kwenye dijitali watahitajika wataalamu wengi sana wa TEHAMA wekezeni katika maabara zenye zana zote za kisasa tuongeze idadi ya wahandisi watakaotumika kwenye miradi mikubwa ya ujenzi,” amesema

“Lazima mjitofautishe na wengine kwa kuwa na maabara za kisasa ambazo zitasaidia kupata wanasayansi wazuri ambao wanahitajika kwenye dunia ya kidijitali,” amesema

Amewataka walimu na watumishi wote wa shule hiyo washikamane kwani mafanikio waliyopata ni matokeo ya mshikamano na kufanyakazi kama timu moja.

Amewataka wahitimu wasidhani kuwa kumaliza kidato cha nne ndiyo mwisho wa masomo na badala yake waone kwamba safari ndiyo kwanza imeanza na waendelee kufanya vizuri kwenye masomo.

“Kuna watakaoenda kidato cha tano na wengine vyuoni lakini cha msingi ni nidhamu kokote mtakapokuwa kwasababu nidhamu ni jambo la msingi maishani, nimefarijika sana kuona kuna walimu wanaofundisha maadili na dini,” amesema

Amewaka wazazi nao kuwahimiza watoto wao kwenda kwenye nyumba za ibada ambako watajengwa kuishi maisha yenye maadili.

Amesema wazazi wanawajibu wa kufuatilia nyendo za watoto kuanzia mavazi na makundi wanayokuwa nayo kwani wanaweza kupoteza mwelekeo wasipodhibitiwa kuwa na mwenendo mwema.

Amewataka pia watumie simu kufanya mambo ya msingi badala ya kuitumia kwa mambo machafu na yasiyofaa ambayo yamekuwa chanzo cha mmomonyoko wa maadili.

Amewataka pia kuweka utaratibu wa kuwatafuta wahitimu wa miaka ya nyuma na kuwaalika kwenye mahafali ya shule hiyo kama njia ya kuwahamasisha wanafunzi hao kusoma.

“Kuna wahitimu wenu wengi wanafanyakazi kwenye mashirika makubwa waleteni hapa ili wanafunzi waone kwamba hawako hapa kwa bahati mbaya wafanye vizuri kwenye masomo ili waje kuwa watu wakubwa,” amesema

Mkuu wa shule hiyo, Ntipoo Reca amesema mbali na kuwaandaa vizuri kitaaluma wahitimu hao, wamejitahidi kuwalea kwa maadili na anatarajia kuwa watakuwa watu wema wanakoenda.

“Tuliwapokea hapa mwaka 2020 tumewafundisha na wamekuwa wakifanya vizuri sana kwenye mitihani na tunatarajia kwenye mitihani yao ya mwisho watapata daraja la kwanza na daraja la pili,” amesema