-Hakuna atakayepoteza ajra, awatoa hofu wafanyabiashara wanaofanyakazi bandarni
Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema mikataba mitatu muhimu inayohusu
uendelezaji wa Bandari ya Dar es Salaam kati ya Mamlaka ya Bandari
Tanzania (TPA) kwa niaba ya Serikali na Kampuni ya DP World ya Dubai
imezingatia maoni yote yaliyotolewa, pamoja sheria na taratibu, zote
kwa maslahi mapana ya nchi yetu.
Aidha, amesisitiza kuwa hakuna mfanyakazi atakayepoteza kazi, awe
mwajiriwa wa bandari au wale wanaofanyakazi zao bandarini, wakiwemo
wafanyabiashara.
Rais Samia, ametoa kauli hiyo Ikulu ya Chamwino, jijini Dodoma
alipokuwa akizungumza mara baada ya kushuhudiwa kusainiwa kwa Mikataba
hiyo mitatu.
Kusainiwa kwa mikataba hiyo pia kulishuhudiwa na viongozi mbalimbali
kutoka Serikalini, Kampuni ya DP World na Umoja wa Falme za Kiarabu.
“Napenda niwahakikishie Watanzania maoni yote yaliyotplewa
yamezingatia pamoja sheria na taratibu, zote kwa maslahi mapana ya
nchi yetu.
Kinachofanyika ni kuhakikisha bandari yetu inafanyakazi kwenye viwango
vinavyokubalika duniani, kukuza biashara na hatimaye mapato ya nchi
yetu,” amesema Rais Samia.
Amesema Serikali kwa upande wake ilisikiliza michango na maoni
mbalimbali iliyotolewa na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), vyama
vya siasa, asasi, wanaharakati huru, vyombo vya habari na pia
waliangalia maoni katika mitandao ya kijamii.
“Tumewasikiliza viongozi wetu wa dini na baadhi ya viongozi wetu wastaafu.
Tumefuatilia kwa karibu sana hoja za wabunge wakati wa kujadili na
kupitisha Azimia la Bunge la Kuridhia Makubaliano ya Awali ya
Ushirikiano katika Uendelezaji wa Bandari kati ya Serikali ya Tanzania
na Mamlaka ya Dubai,” amesema Rais Samia na kuongeza;
“Na tulipokea ushauri wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM, kwa
uhakika naweza kusema hakuna sauti au kundi ambalo halikusikilizwa ama
ilipuuzwa,”
Amesema Serikali iliunda jopo la wataalam , lakini pia wanasiasa na
wanasheria waangalie hoja zote zilizotolewa wawaambie ni ipi iigie
kwenye mikataba na ipi haina mishiko kwenye mikataba.
Rais Samia amesema kazi hiyo ilifanywa vizuri na baadhi waliopedwa
kazi ya uchambuzi kutoka sekta binafsi wale wabobezi wa mambo ya kodi,
sheria nao waliingizwa kwenye timu ya majadiliano.
“Kwa hiyo tulifanya uchambuzi wa kina na kwa ujumla na kwa kipekee
nashukuru Watanzania wote waliojitokeza kutoa maoni yao juu ya
mchakato huo na kutuwezisha kupata nyenzo na miongozo ya kuzingatiwa
kwa makini katika majadiliano,” amesema Rais Samia.
Amesema linapokuja jambo geni lazima kutakuwa na maoni tofauti na ni
haki yetu na ndiyo demokrasia, watu watoe maoni yao.
Kwa mujibu wa Rais Samia inakuwa ni kazi ya Serikali kubeba maoni na
kuyafanyia kazi na wao ndicho walichokifanya.
“Mikataba hii iliyosainiwa imezaliwa kutoka kwenye makubaliano ya
awali ya lile dude lililoleta maneno mengi, ndilo lililotoa mikataba
hii mitatu kama ambavyo iliridhiwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania,” amesema Rais Samia na kuongeza;
Rais Samia, amesema ni lazima kukuza ufanisi wa bandari, iweze
kusafirisha mizigo mingi ya biashara. Alisema kwa kuzingatia ukweli
huo, busara ziliwaelekeza tupate mwekezaji ambaye tutashirikiana naye
kuongeza ufanisi.
Amesema walizingatia kuwa wao sio mlango bahari pekee Mashariki na
Kusini mwa Afrika. Kwa hiyo Rais Samia alisema maboresho yoyote ya
kiutendaji yanayokwenda kufanywa kupitia uwekezaji huo yanaenda
kukuzwa biashara ndani na nje na kuwezesha shughuli za kiuchumi za
nchi jirani.
Kwa mujibu wa Rais Samia, kuna bandari zingine mbali na ya kwetu,
hivyo wale wanaotaka mizigo yao ifike haraka wanaweza kuchagua
Bandari yoyote mizingo yao ipite na wakaitumia.
Amesema kinachotupa turufu dhidi ya washindani wetu ni mlango wetu wa
bahari kuwa na masafa mafupi kuingia kwenye nchi za jirani na
tunafikika na nchi nyingi kwa kupitia mpaka mmoja, ikilinganishwa na
nchi nyingine na mlango Bahari mingine.
Hata hivyo, amesema ukaribu sio sababu peke yake, kwa sababu tumekuwa
nao siku zote, lazima tufanyekazi ya kuongeza ufanisi kwenye bandari
yetu, kwani wafanyabiashara uangalia gharama.
Amesema kwenye mazungumzo yote Watanzania wanakubalia ipo changamoto
pale bandarini, tunatofautiana kwenye kuzitatua.
Amesema wapo wanaoamini sisi wenyewe bila mbia tunaweza kuiendeleza.
Rais Samia alisema hayo ni mawazo mazuri ya kimapinduzi, lakini yapo
mbali na uhalisi na njia hiyo itatuchukua muda mrefu kufika, wakati
dunia inaenda mbili.
Ameshukuru Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushauri wao
makini na kuridhia Azimio la makubaliano ya Awali ya Ushirikiano ya
Uendeshaji wa Bandari Juni 10, 2023.”
Aidha, amemshukuru Baraza la Mawaziri kwa kubariki mikataba hiyo
mitatu iliyosainiwa kwa mazingatio ya Kifungu cha Pili cha Sheria ya
Ubia No: 6 ya mwaka 2023 na Kifungu cha Pili cha Sheria ya Ununuzi wa
Umma No: 5 2023.
Amempongeza Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa na wajumbe wa
Kamati ya Majadiliano iliyoongozwa na Amza Johari kwa kazi kubwa
ambayo wamefanya na wengine.
Amepongeza uongozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu na uongozi wa DP World
ya Dubai kwa kushiriki bila kuchoka kwenye majadiliano yaliyotufikisha
kwenye makubaliano hayo yanayohusu uendelezaji katika bandari ya Dar
es Salaam.
Amesema wanawashukuru kwa uelewa wao na umakini waliouonesha katika
kipindi chote cha majadiliano.
“Tunafarijika kuwa wameridhia mahitaji na matakwa yetu kama
yalivyobainishwa, ambayo yamezingatia matamanio ya wananchi ya
Watanzania na maslahi mapana ya nchi yetu,” amesema Rais Samia.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa