November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bajaji,pikipiki kurahisisha utendaji kazi Dar es Salaam

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online, Dar es Salaam

HALMASHAURI ya Jiji la Dar es Salaam imendelea kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato ambapo imeweza kukusanya zaidi ya bilioni 30 huku awali ilikuwa ikikusanya chini ya bilioni 20 katika kipindi cha miezi mitatu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, leo Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, wakati akikabidhi pikipiki za magurudumu matatu (Bajaji) 35 na pikipiki za magurudumu mawili ” (bodaboda) 7, zenye thamani zaidi ya milioni 300 kwa ajili ya kusaidia utendaji kazi wa shughuli mbalimbali katika Kanda saba za kutoa huduma katika halmashauri ya Jiji hilo.

Mpogolo amesema vyombo hivyo vitaenda kurahisisha utendaji kazi katika kanda hizo ikiwa ni pamoja na kuongeza ukusanyaji wa mapato katika Wilaya ya Ilala na Jiji la Dar es Salaam kwa ujumla.

“Ukusanywaji mzuri wa mapato katika Jiji letu la Dar es Salaam leo hii umewezesha kununua bajaji hizi 35 na pikipiki 7, ambazo kila kanda itakuwa na bajaji tano na pikipiki moja, lengo ni kuwarahisishia watendaji wanapo timiza majukumu ya kikazi ikiwepo na ukusanywaji wa mapato,”.

Amesema Jiji hilo pamoja na Wilaya ya Ilala, wakazi wake ni wafanyabiashara hivyo bajaji na pikipiki hizo zitaenda kurahisha ukusanyaji wa mapato kwa na shughuli zingine.

Pia amesema kuwa, katika upande wa ukusanyaji wa mapato kwa wafanyabiashara, Jiji la Dar es Salaam litakuwa na makusanyo makubwa na matumizi bora kuliko halmashauri zote nchini, huku akidai kuwa hivi sasa halmashauri hiyo imejiwekea malengo ya ukusanyaji wa zaidi ya bilioni 100.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Jomaary Satura, amesema kuwa, lengo ya halmashauri hiyo ni kutoa huduma bora kwa wananchi wake ikiwa pamoja na kuwasogezea huduma karibu na makazi yao.

Nae Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Omary Kumbilamoto, amesema kutokana na Kanda hizo kupata vitendea kazi itaenda kusaidia kuzalisha ajira mpya kwa madereva wa bajaji na pikipiki hizo.