Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Jeshi la Polisi,maofisa uvuvi pamoja na taasisi nyingine zinazohusika na ulinzi wa rasilimali za Ziwa Victoria zimeombwa kutoa elimu ya athari ya uvuvi haramu kwa wavuvi ili kuongeza samaki pamoja na kulinda rasilimali zilizopo ndani ya ziwa hilo.
Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri uvuvi endelevu Ziwa Victoria Hasani Muhenga akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa mara baada ya kufunguliwa kwa kikao maalum kilichowakutanisha makamanda wa Polisi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwemo Kagera,Mara,Simiyu, Geita,Mwanza na Shinyanga na wadau wa sekta ya uvuvi kuzunguka ziwa hilo.
Kikao hicho kilichofanyika jijini Mwanza Oktoba 18,2023 huku kikiwa na malengo ya kufanya tathimini na kuweka mpango mkakati utakaowezesha kuzuia matukio ya uhalifu ndani ya ziwa hilo.
Ambapo ameeleza kuwa maofisa hao wanapofika kwa wavuvi watoe elimu ya uvuvi haramu kisha ndio waje na operesheni ya uvuvi haramu lakini mara nyingi wanakuja kwa ajili ya operesheni hivyo wavuvi wamekuwa wakimbia hivyo kukosa elimu ya kuwajenga kimsingi ya kuweza kuwahamasisha wajue nini athari za uvuvi haramu.
Muhenga amesema kuwa wanashauri maofisa uvuvi na wote wanaohusika na ulinzi wa rasilimali wa Ziwa Victoria wanapoenda katika maeneo ya mialo watoe elimu ya athari za uvuvi haramu kwa wavuvi vinginevyo rasilimali ya ziwa itapotea huku akisisitiza kutokutegemea kuwa watapata samaki wa kufuga.
“Samaki wa kufuga anatakiwa awe ziada lakini tumlinde samaki wa asili asitoweke kwa sababu ndio anayetutangaza Ziwa Victoria,elimu itolewe maofisa uvuvi wawe wanazunguka mara kwa mara kwa wavuvi kufikisha elimu hiyo kwani elimu ni ndogo haifiki kwa walengwa kule ziwani tunahitaji elimu itufikie,”ameeleza Muhenga.
Sanjari na hayo ameeleza kuwa wamefanya kikao cha tano na Jeshi la Polisi juu ya Ulinzi wa rasilimali za ziwa na watu na mali zao ziwani na tangu kuanza kwa vikao hivyo hadi kufikia siki ya leo uhalifu ziwani wa ujambazi wa kunyang’anywa mashine umebaki historia hivyo wanalishukuru jeshi hilo.
“Kuna uhalifu uliozuka wa ndani kwa ndani wa sisi kwa sisi tunanyang’anyana mali jeshi la Polisi bado halijaweza kudhibiti,wavuvi kwa wavuvi,tajiri kwa tajiri,mvuvi wa dagaa na mvuvi wa sangara tunafanyiana uhalifu kunyang’anyana nyavu,taa za kuvulia ndio tatizo linalotusumbua,ila uhalifu mkubwa wa kutumia bunduki na kupoteza uhai ndani ya Ziwa Victoria haupo mali zako zikipotea kutoka kwenye mwalo zikaenda sehemu nyingine utazikuta”ameeleza Muhenga.
Naye mmoja wa Mvuvi Ziwa Victoria Augustino Gimasa ameeleza kuwa suala la uvuvi haramu ni tatizo kubwa na unaendelea kutokana na elimu duni ya wavuvi kuweza kujitambua pamoja na mapungufu yaliopo katika sekta ya uvuvi za kutokuwa na doria za mara kwa mara pamoja na kutotekeleza majukumu yao ya kutokomeza uvuvi huo.
“Elimu ya kutekeleza uvuvi haramu itamjengea uwezo mvuvi kuweza kutambua athari za uvuvi haramu na faida atakazozipata pindi atakapo acha kufanya uvuvi haramu na pindi uvuvi endelevu utakapo pewa nafasi kwa maana atanufaika zaidi na kujiingizia kipato cha kutosha,” ameeleza Gisama.
Kwa upande wake Mkuu wa usimamizi wa Vikosi maalum vya Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Ferdinand Mtui kutoka kamisheni ya Opereseheni na mafunzo, makao makuu ya Polisi Dodoma, ameeleza kuwa hali ya usalama ndani ya Ziwa Victoria kwa sasa ni shwari kutokana na tathmini ya vikao vitano vilivyopita vimeweza kuchangia kupunguza uhalifu ziwani.
Haya hivyo Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi,Mkuu wa operesheni za Jeshi la Polisi Nchini Mihayo Msikhela, ameeleza kuwa kati ya mwaka 2019-2020 kuliibuka uhalifu mkubwa ndani ya Ziwa Victoria ikiwemo mauaji,unyanganyi wa kutumia silaha,uporaji wa nyavu,samaki na boti za injini na hasa kutoa majeruhi ya wavuvi na baadhi ya wafanyabiashara ziwani lakini kwa sasa matukio hayo yamepungua.
“Jeshi la Polisi Nchini lipo imara,tupo tayari kushirikiana na wadau wote wa uvuvi wa nchini kwetu dhidi ya uhalifu wowote wa nadni na nje ya mipaka yetu ,wale ambao wanavua kwa makusudi huku wakijua kuwa wamevuka na wapo kwenye maeneo yetu wawe tayari kupambana na moto wa jeshi letu na tukiwapata tutawashughulikia kwaujibu wa sheria,”ameeleza Msikhela.
Ameeleza sheria za nchi hii zipo wazi mtu akiingia nchini bila ya kuwa na kibali cha kusafiria watamkamata na kumfikisha mahakamani huku akiwasisitiza wavuvi wa Tanzania wasivuke mipaka ya Ziwa kwenda katika eneo la nchi jirani za Kenya na Uganda kwani watakamatwa na kushughulikia kwa mujibu wa sheria za nchi husika na wakirundi nchini tutawashughulikia vilevile kwa kwenda nje ya nchi bila ya kuwa na vibali vya kusafiria.
Akifungua kikao hicho Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi akimwamilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Amos Makala,ameeleza kuwa sekta ya uvuvi inachangia kwa asilimia 7 pato la mkoa.
Ambapo Mkoa umedhamiria kutekeleza mpango wa maendeleo wa miaka mitano katika sekta ya uvuvi ya kuifanya Mwanza kuwa na uchumi wa bluu kwa kuanzisha miradi mbalimbali kupitia ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba.
“Ni sekta pekee ya uvuvi ambayo mtu anaweza kuwa na kiwango kidogo cha fedha na akafanikiwa hivyo samaki wasipokuwepo ziwani ata uchumi wa Mkoa unashuka,”.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi