Na Agnes Alcardo,Timesmajira Online, Chalinze.
SERIKALI imeahidi kushughulikia changamoto ya umeme iliyopo nchini kwa kasi kubwa, ili tatizo hilo liweze kuisha katika kipindi kifupi kuanzia sasa.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko katika mkutano mkuu maalum wa Jimbo la Chalinze wa kupokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM (2020-2025) Wilaya ya Chalinze Mkoa wa Pwani.
Dkt. Biteko amesema kuwa, katika kipindi cha miezi sita inayokuja ukosefu wa umeme nchini utaisha, baada ya Serikali kuweka mikakati madhubuti ya kumaliza tatizo hilo na kudai kuwa hivi sasa watendaji wanafanya kazi ili watanzania wapate umeme wa kutosha.
Sanjari na hayo Dkt. Biteko ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kupeleka umeme katika shule ya Sekondari ya Moreto ili shule hiyo iunganishwe na huduma ya Nishati hiyo mapema huku akichangia kompyuta 10 kwenye shule hiyo kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi katika matumizi ya TEHAMA.
Kuhusu Halmashauri ya wilaya ya Chalinze Dkt. Biteko ametumia nafasi hiyo kupongeza juhudi zinazofanywa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii, ikiwemo ujenzi wa madarasa, zahanati na miundombinu muhimu na pia kufanya vizuri katika makusanyo ya mwaka ambapo wilaya hiyo imekusanya kiasi cha bilioni 15.
Kwa upande wake Rais wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatoa msukumo mkubwa kwenye maendeleo na fedha hizo zinaelekezwa katika miradi mbalimbali ili kukuza uchumi wa nchi.
Pia Dkt. Kikwete amempongeza Dkt. Biteko kwa kuteuliwa na Rais kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati hapa nchini na kumsisitiza awe msaada mkubwa katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya serikali na kufanya kazi kwa bidii.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema kuwa mkoa huo unaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa shule, madaraja, vituo vya afya ili ukue kiuchumi na hatimaye kuboresha maisha ya wananchi wake.
Naye Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete amesema, katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais Samia, Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze imefanikiwa kutekeleza kwa kiwango kikubwa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020/25.
“Wananchi wamewezeshwa kiuchumi, hali ya uzalishaji katika kilimo, uvuvi, umwagiliaji, viwanda na biashara imeongezeka, miundombinu ya shule, zahanati, vituo vya afya na hospitali ya wilaya imekamilika kwa asilimia kubwa na kwenye baadhi ya vijiji na kata ujenzi unaendelea,”amesema Ridhiwani.
Hata hivyo Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Halima Okash amesema, katika kipindi cha miaka wameshuhudia mabadiliko makubwa ya kimaendeleo ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze na Mbunge anaonesha ushirikiano.
More Stories
Prof. Mwakalila asisitiza uadilifu, uzalendo kwa wanafunzi wapya chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere
Benki ya Equity Tanzania yasaini mkataba wa kuwawezesha wanawake kiuchumi
Rais Samia alivyoguswa kifo cha msanii Grace Mapunda