November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Masache:Milioni 800 zimetengwa ununuzi vifaa tiba zahanati ya Nkwangu

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Chunya

MBUNGE wa Jimbo la Lupa wilayani Chunya mkoani Mbeya Masache Kasaka amesema kuwa Serikali imetenga kiasi cha zaidi ya milioni 800 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba kwa mwaka huu wa fedha 2023/2024 kwa ajili ya zahanati ya kijiji cha Nkwangu

Mbunge Kasaka amesema hayo leo wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Nkwangu kwa kuwapa mrejeso kuhusu Bunge la bajeti na kueleza shughuli mbalimbali zilizofanyika na ambazo zinaendelea kufanyika pamoja na kusikiliza kero za wananchi.

Ambapo amesema kuwa zahanati hiyo itakuwa ni moja kati ya wanufaika wa vifaa hivyo ili wananchi waendelee kupata huduma.

Aidha amewataka viongozi kuwapa mrejesho wananchi kuhusu fedha za maendeleo zinazoletwa na hata michango ya wananchi pamoja na kusoma taarifa za mapato na matumizi za fedha hizo.

Pamoja na hayo Mbunge Kasaka amewataka wananchi wa Jimbo hilo kuendelea kuiamini serikali kwani mpaka sasa imeendelea kutekeleza ahadi zote zilizoahidiwa mwaka 2020 na bado inaendelea kutekeleza.

“Hakikisheni wananchi wanapata taarifa ya fedha za serikali zinazoletwa kujenga miradi mbalimbali pamoja na fedha zinazotokana na michango yao ili kuepuka usumbufu kwani wamekuwa wakilalamika kwamba wanachaga fedha lakini hawaoni kilichofanyika lakini ukifuatilia unakuta fedha hizo zimefanya mambo mazuri lakini hawajui,”amesema.

Diwani wa Kata ya Upendo ,Richard Itelekelo amemshukuru Mbunge huyo kwa kuendelea kuwa mstari wa Mbele kuwapigania wananchi wa wilaya ya Chunya hasa kata ya Upendo kwani miradi mbalimbali kama vile uchimbaji wa visima, ujenzi wa shule ya sekondari, ujenzi wa zahanati na mingine mengi inatekelezwa katika kata hiyo kwa fedha kutoka serikalini

Awali akisoma taarifa kwa niaba ya wananchi , Mtendaji wa kijiji cha Nkwangu , Andrew Msoya amesema kijiji kinakabiliwa na chagamoto mbalimbali ikiwemo barabara, kukosekana kwa mawasiliano,nyumba za watumishi waliopo katika kijiji hicho, vifaa tiba katika zahanati hiyo pamoja,vitanda na jokofu la kutunzia chanjo kwa ajili ya watoto jambo ambalo husababisha watoto wanaostahili kupata chanjo kukosa chanjo hiyo hivyo kuhatarisha maisha yao.

Mbunge Kasaka yupo katika ziara yake ya kawaida kuwatembelea wananchi ili kuwapa mrejeso wa Bunge la Bajeti lililotamatika mwezi juni, kusikiliza kero za wananchi na kutafuta suluhu na kueleza namna ambavyo serikali inaendelea kutekeleza majukumu yake ili kuleta maendeleo kwa wanachunya wakiwemo wananchi wa kijiji cha Nkwangu. Ziara hiyo itaendelea leo Septemba 8 kwa Kata ya Upendo