Judith Ferdinand, Timesmajira Online,Mwanza
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Masala ameiagiza Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kuhakikisha inamalizia miradi yote iliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi ili kutowavunja moyo huku akisisitiza shughuli za usafi katika maeneo yote ya wilayani humo.
Pia ametumia fursa hiyo kuwapongeza wananchi wa Kata ya Nyasaka kwa juhudi zao za kuchangia ujenzi wa ofisi za Serikali za mitaa na Kata.
Masala ametoa agizo hilo pamoja na pongezi hizo wakati wa muendelezo wa ziara yake ya kusikiliza kero za wananchi na kukagua miradi ya maendeleo katika Kata zote za Wilaya ya Ilemela.
Ambapo mbali na kuitaka halmashauri hiyo kumalizia miradi hiyo amechangia mifuko ishirini ya saruji kama ishara ya kuunga mkono jitihada za wananchi wa Kata ya Nyasaka za ujenzi wa ofisi hizo.
Hivyo amewahimiza wananchi hao kuendelea na moyo huo katika miradi mingine ya maendeleo inayotekelezwa katika eneo lao.
“Niwapongeze kwenye mambo ya ujenzi wa ofisi zenu za mitaa, Kwakweli mnafanya vizuri hata ukiangalia mitaa yenu yote karibu ina ofisi,”amesema Masala.
Kaimu Mtendaji Kata ya Nyasaka Bashite Peter amesema kuwa ujenzi wa ofisi ya kata umefikia hatua ya renta ukihusisha nguvu za wananchi, mchango wa Mbunge Dkt.Angeline Mabula pamoja na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela hivyo kufanya jumla ya thamani ya kiasi cha shilingi milioni 10.68(10,680,000) huku akiiomba Halmashauri kusaidia ukamilishaji wa jengo hilo la ofisi.
Diwani wa Kata ya Nyasaka Abdulrahman Simba,amesema kuwa kata yake imetekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa ofisi tano za mitaa na ujenzi wa barabara tatu Kwa viwango vya changarawe.
Mhandisi Uswege Jacob kutoka Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) amesema kuwa kata ya Nyasaka imefanikiwa kujengewa barabara yenye urefu wa Km 1.2 kwa kiasi cha milioni 241 na Mkandarasi Kones Construction kwa kipindi cha miezi 2 huku serikali inao mpango wa kuendelea kurekebisha miundombinu katika mitaa mbalimbali ya kata hiyo.
More Stories
Rais Samia kuzindua mfuko wa kuendeleza kazi za wabunifu
Makalla ampongeza Lissu kukiri CHADEMA haina wagombea Serikali za Mitaa
Chande azindua misheni ya uangalizi uchaguzi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika