Na Mwandishi Maalumu, Timesmajira Online
SERIKALI kupitia Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), imeendelea na juhudi za kuwafungulia fursa mabaharia wa nchini hapa kimataifa na mpaka sasa imesajili vyeti 17,689 vya mabaharia.
Ambapo TASAC ilisaini Hati ya Makubaliano (MOU) na nchi ya Barbados,kwa niaba ya serikali ili nchi hizo mbili ziweze kutambua vyeti vya mabaharia wa kila upande.
Akizungumza mara baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo jijini London, Uingereza, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC ambaye pia ni Msajili wa Mabaharia na Meli nchini, Kaimu Abdi Mkeyenge amesema hadi sasa Tanzania imeanzisha mawasiliano na majadiliano na nchi 34 kwa ajili ya makubaliano ya kutambulika kwa vyeti vya mabaharia wa pande hizo.
Amesema hatua hiyo ni fursa nzuri ya ajira za kimataifa kwa mabaharia wa Tanzania pia itasaidia kuondoa usumbufu wa kushushwa kwa mabaharia wa kitanzania katika meli mbalimbali ambazo zimesajiliwa na nchi ambazo Tanzania haina mkataba nazo.
Barbados ni nchi ya Kisiwani katika Bahari ya Karibi takriban kilomita 430 Kaskazini-Mashariki mwa Venezuela, mpaka sasa ina usajili wa wazi na masharti nafuu (open registry) wa meli 400.
Nchi jirani za karibu kuvukia bahari ni Saint Lucia na Saint Vincent upande wa Magharibi, Trinidad na Tobago upande wa Kusini na Grenada upande wa Kusini-Magharibi.
“Barbados ni moja ya nchi ambazo tulikuwa tumeanzisha mazungumzo kuhusu, tunashukuru leo hii tumefanikiwa kusaini Hati ya Makubaliano ya kutambuliana vyeti vya mabaharia, hivyo basi nidhahiri kuwa sisi tunatambua mabaharia wa Barbados na wao wanatambua mabaharia wetu,”amesema Mkeyenge.
Nchi nyingine ambazo Tanzania imeshaanzisha mawasiliano na majadiliano ni pamoja na Bahamas, Algeria, Korea ya Kusini, China, Comoros, Cyprus, Misri, Ufaransa, Ghana, India, Iran, Kenya, Liberia, Malta, Marshall Islands, Mongolia, Oman, Palau, Panama, Peru, Qatar, Saudi Arabia, Singapore, Africa Kusini, Shelisheli, Uturuki, Umoja wa Falme za Kiarabu, Vanuatu, Vietnam na nchi za Umoja wa Ulaya.
Â
More Stories
Mwalimu adaiwa kumfanyia ukatili mwanafunziÂ
NAOT watakiwa kuendana na viwango vya ukaguzi
Rais Samia kuzindua mfuko wa kuendeleza kazi za wabunifu