November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Hatua madhubutu zahitajika kudhibiti taka plastic fukwe za maziwa makuu

Judith Ferdinand

Utupaji wa taka hususani za plastiki ndani ya maziwa na bahari nchini bado ni changamoto huku hali hiyo ikielezwa kuwa hatua za makusudi zisipo chukuliwa za kudhibiti taka hizo kuingia katika fukwe itachangia kupunguza samaki ifikapo mwaka 2050.

Hii ni kutokana na tafiti zilizofanywa kupitia kampeni ya Fukwe Safi yenye lengo la kukusanya taarifa na takwimu za taka katika mialo ya maziwa makuu (Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa). Kampeni hiyo inatekelezwa kwa kushirikiana kati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (SOAF-UDSM), EMEDO, Halmashauri ya Jiji la Mwanza na ARENA RECYCLING kwa ufadhili wa shirika la NORCE kutoka nchini Norway.

Muonekano wa taka za plastiki ambazo zinaelea katika Ziwa(picha kwa msaada wa mtandao)

Endapo hatua hazitachukuliwa kufikia miaka hiyo taka zitakuwa nyingi zaidi kuliko samaki hali itakayochangia kushindwa kufikia adhima ya serikali ya kuwa na uchumi wa bluu ambayo imetenga kiasi cha bilioni 7 kwa ajili ya kuwezesha vijana katika ufugaji wa samaki ambao unategemea maziwa na bahari.

Akizungumza na Timesmajira Online mara baada ya kumalizika kwa kikao kazi cha kuwasilisha matokeo/mrejesho wa kampeni ya Fukwe Safi maziwa makuu yenye lengo la kukusanya taarifa na takwimu za taka katika mialo ya maziwa makuu (Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa) Mhadhiri Msaidizi Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam shule Kuu ya Sayansi na Teknolojia ya Uvuvi Dkt.Bahati Mayoma, anaeleza kuwa lengo la kampeni hiyo ni kuhakikisha wanatoa elimu kwa jamii ili kudhibiti taka ngumu zinazotokana na plastiki.

“Tusipochukua hatua mapema maana yake tunatengeneza janga kubwa zaidi na adhima njema ya serikali ya uchumi wa bluu haita fikiwa kwa sababu uchumi wa bluu siyo samaki tu, kuna sekta kama utalii,viumbe kuzaliana kama unataka samaki lakini mazingira yake siyo mazuri hauwezi kumpata samaki na hata ukimpata hawawezi kuwa bora,”anaeleza Dkt.Mayoma.

Mwanzilishi wa Arena Recycling Industry Zagalo Emanuel, akionesha tofali lililotengenezwa na taka za plastiki

Anaeleza kuwa kampeni yao ilianza Februari 28 mwaka huu,ilizinduliwa jijini Mwanza na baadae ikaendelea kufanyika katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Wilaya ya Nyamagana, Ukerewe,Kigoma Ujiji kwa upande wa Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa walikuwa Kyela.

“Awamu ya kwanza ilifanyika vizuri tulikamilisha maeneo yote na kiwango cha taka kilikuwa kikubwa,awamu ya pili tulianza Agosti hadi Septemba na tukaongeza maeneo mawili mapya ya Mkoa wa Mara na Simiyu,” anaeleza Dkt.Mayoma.

Anaeleza kuwa kiwango cha taka za plastiki kipo na ni kikubwa nchini katika vyanzo vya maji kama zilivyo nchi nyingine duniani huku chanzo kikuu ni matumizi yasiyo endelevu yanayotokana na jamii yenyewe kutozingatia taratibu zilizowekwa na serikali za kutochafua mazingira.

“Mimi pamoja na timu ya watafiti wengine mwaka 2014,2015 tulianza utafiti wa taka za plastiki Ziwa Victoria na tukagundua tatizo hilo lipo nchini na mwaka 2018 serikali ilipitisha sheria ya kudhibiti matumizi yasiyo endelevu ya mifuko ya plastiki,”anaeleza Dkt.Mayoma na kuongeza kuwa

“Tukaendelea kufanya tatifi nyingine 2019,2020 tukaona tatizo hili bado lipo hivyo tukaona njia rahisi kwa sisi watafiti ni kurudi kwenye jamii na kuishirikisha kuwa mabalozi wa kudhibiti taka kwani serikali pekee yake haiwezi kwani taka zinatokana na mtu mmoja mmoja ndio sababu ya kuja na hii kampeni,”.

Pia anaeleza kuwa katika taka walizokusanya nyingi ni chupa za plastiki ambazo zinatumika kama vifungashio vya bidhaa mbalimbali ndio zinaongoaza kwa wingi ndani ya maziwa hayo.

Huku mifuko ya plastiki ikifuata kwa wingi na kwa bahati mbaya kwenye baadhi ya maeneo bado mifuko ile ambayo serikali imezuia inaendelea kuonekana.

“Hii ni ishara kuwa kuna wachache ambao wanakiuka taratibu ambazo serikali imeweka katika kuhakikisha inadhibiti taka za plastiki hususani mifuko,”anasema Dkt.Mayoma.

Sanjari na hayo anaeleza kuwa kitu kingine walicho kibaini na cha kushangaza ni kuwa ata taka zinazotokana shughuli za uvuvi kama nyavu zilizotekelezwa na vigungashio mbalimbali vinavyotumika katika sekta hiyo vimeibuka miongoni mwa taka tano zinazopatikana kwa wingi katika kampeni hiyo.

Vilevile anaeleza kuwa tafiti duniani kote zinaonesha kuwa taka za plastiki zinaweza kuathiri viumbe hai wa majini kwa namna mbalimbali ikiwemo kuzonga samaki hivyo kusababisha kufa.

Pia anaeleza kuwa pamoja na kipande cha plastiki kumezwa na samaki ambacho hakiwezi kumengenywa hivyo wanakufa kimya kimya hali hiyo ni changamoto ambayo inahitaji kushughulikiwa.

“Tusipochukua hatua sasa maana yake ndoto ya uchumi wa bluu ya serikali inaweza isifikiwe kwani samaki watapungua au kupotea kabisa,ili kufikia adhima hiyo lazima kitu chochote kinachofanya uchumi wa bluu iwe mazingira,samaki wenyewe,maji lazima viwe na ubora unaokubalika kimataifa na kitaifa ndio maana tunasema tuchukue hatua sasa kunusuru viumbe vyetu,”anasema Dkt. Mayoma.

Huku anaeleza kuwa hayo ni matokeo ya awali wanaendelea kuweka takwimu vizuri ili waweze kutoa kitu kilicho kamilika ingawa maziwa yote matatu yalio fikiwa na kampeni hiyo yote yana changamoto ya uchafuzi wa taka za plastiki kama zilivyo nchi nyingine.

Msaidizi wa utafiti kutoka Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam Happiness Beda,anaeleza kuwa kampeni hiyo imelenga kupunguza taka za plastiki kwenye maziwa makuu pamoja na kushirikiana na jamii husika inayozunguka maeneoa hayo ikiwemo wanafunzi.

Beda anaelea kuwa wanatoa elimu kwa jamii jinsi gani wanavyoweza kupambana na taka za plastiki kwani kuziepuka kabisa inaweza kuwa ni changamoto lakini kufanya urejerezaji kama wanavyofanya Arena Recycling Industry kutumia taka hizo kutengeneza tofali na vigae.Pia kuacha matumizi ya mara moja ya plastiki(single use plastic),bali itumike zaidi ya mara moja mfano chupa za plastiki EMEDO wanatumia kutengenezea banda,heleni na hiyo yote ni kuepusha taka hizo zisiingie ziwani.

“Tulienda shule ya msingi Mwembeni mkoani Mara tukawakuta wananfunzi mbalimbali wa mahitaji maalumu wanatengeza vitu mbalimbali kwa kutumia taka za plastiki,”anaeleza Beda.

Bidhaa zilizotengenezwa na taka za plastiki ikiwemo heleni,kamba za kuanikia nguo

Sanjari na hayo anaeleza kuwa wakipata takwimu halisi watashirikiana na mamlaka husika kama Ofisi ya Taifa ya Takwimu(NBS) kutengeneza sera ambazo zitasaidia kudhibiti uchafuzi wa taka za plastiki.

“Kwa kiasi chake tumefanikiwa kufikia shule 21 na kukusanya taka, tuendelee kushirikiana na jamii kwa sababu ndio wanao kaa kwenye maeneo hayo na wanajua changamoto zilizopo kwa kuwapa elimu ili waweze kutatua changamoto ya taka za plastiki, hatujafika sehemu zote tunahitajika miradi mingine kama hii tumefikia Ziwa Victoria upande wa Magharibi pia kuna upande mwingine nao unatakiwa ufikiwe,”anaeleza Beda.

Nini chanzo cha utupaji taka za plastiki

Beda anaeleza kuwa changamoto ni uelewa mdogo wa jamii kwani hawana elimu kuhusu taka za plastiki maana ukiwaambia zikiendelea kuwa nyingi ikifika 2050 hatutaweza kupata samaki kwani taka zitakuwa nyingi zaidi hawaelewi.

“Tuwape elimu na madhara yake ya utupaji wa taka hususani za plastiki ili mtu alielewe tatizo lazima hajue madhara yanayotokana na tatizo hilo ili haweze kulibeba kwa ukubwa wake,” anaeleza Beda.

Wadau wanavyoweza kubadili taka kuwa bidhaa

Naye Mwanzilishi wa Arena Recycling Industry Zagalo Emanuel, ameeleza kuwa wanatengeneza bidhaa zinazotokana na taka za plastiki ambazo ni rafiki kwa mazingira.Zagalo anaeleza kuwa katika kampeni hiyo wameshiriki kwa namna kuu mbili kwanza ni kudhibiti taka zote rejerezi na zisizo rejerezi ambazo zimekusanywa kutoka kwenye fukwe takribani 68,ambazo wamezifanyia usafi katika maziwa makuu matatu.

Anaeleza kuwa kwa taka ambazo siyo rejerezi wamekuwa wakizipeleka kwenye madampo na zile taka rejerezi wametafuta namna ambayo zinakwenda kutumika kwa mara nyingine.

“Tunatengeneza bidhaa kwa kutumia taka za plastiki ambazo ni marafiki kwa mazingira ikiwemo tofali ambazo zinatengenezwa bila kutumia saruji kadhalika katika ujenzi pia utumii kwan zinajengwa kwa kupachika hali ambayo inarahisha na kupunguza gharama za ujenzi,”anaeleza Zagalo.

Pia anaeleza kuwa bidhaa hiyo ya tofali zinazotokana na taka za plastiki mbali na kuokoa mazingira pia ni nafuu hata kwa wananchi menye kipato cha chini na kati ambayo bei yake ni nafuu ukilinganisha na tofali nyingine za saruji na udongo.Ubora wa tofali za plastiki.

Zagalo anaeleza kuwa wamefanya vipimo katika Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam kitivo cha Ardhi pamoja na kupeleka nchini Ujerumani ambapo vipimo vimeonesha kuwa tofali hizo ni imara mara mbili ya zile za kawaida zilizo zoeleka.

“Ni tofali ambazo ni ngumu mara mbili ya nyingine,haziathiriwi na maji hivyo zinaweza kutumika hata katika mazingira ya maji ambapo tofali nyingine zinapata ‘fangasi’(ukungu) kwa hizi huwezi kuona changamoto kama hizo,zinatunza joto takribani nyuzi joto 120 karibu na tofali za kawaida,” anaeleza.

Anaeleza kuwa kwa sasa soko la tofali hizi bado change kwa wateja ni wachache lakini wameweza kufanya kazi na mashirika yanayofanya ujenzi wa majengo kama Wilaya ya Temeke wamejenga kwa kutumia tofali hizo katika shule tatu.

Wito kwa vijana waweze kushiriki katika kutatua tatizo la taka za plastiki kama kujihusisha moja kwa moja kufanya urejezaji aidha kwa kukusanya plastiki au kugeuza taka za plastiki kutengeneza bidhaa mbalimbali ambazo ni rafiki kwa mazingira.

Kwa upande wake Adventina Edson kutoka shirika la EMEDO linalo jishughulisha na uhifadhi na utunzaji wa mazingira,anaeleza kuwa wamekuwa wakifanya na klabu za mazingira shuleni ambao wamekutana na watoto wenye uhitaji maalumu ikiwemo viziwi ambao wameweza kutumia vizibo vya chupa za plastiki kutengenezea ndala(malapa).

Pia wametengeneza mikoba,kamba za kuanikia nguo,kofia,mikebe kwa ajili ya kutunzia mafuta kwa kutumia taka za plastiki.

“Lengo au dhima ya kampeni hii tunatamani kutokomeza taka za plastiki katika Ziwa Victoria au kupunguza maana zina athari katika ziwa letu,”anaeleza Advetina.

Sanjari na hayo anaeleza kuwa shirika lao wanatoa elimu kwa jamii ili iweze kuhifadhi mazingira lakini pia kupunguza matumizi ya plastiki .

“EMEDO tuna bustani za mboga ambazo zimetokana na taka za plastiki na tumezitoa katika mazingila lakini pia unaweza kutengeneza bustani nzuri nyumbani kwako ukapata mbogamboga kwa ajili ya matumizi ya familia au biashara,”anaeleza.

Pia anaeleza kuwa kawa kutumia taka za plastiki wanatengeneza banda ambalo lanaweza kutumika kwa ajili ya mikutano,mama ntilie(mama lishe),’grocery’ au banda kwa ajili ya kufugia mifugo.

“Banda hili limetokana na chupa za plastiki ambazo tumeziokota mtaani lengo kutunza mazingira pamoja na kuhakikisha tunadhibiti plastiki aiingii katika Ziwa Victoria,hivyo tunaipa matumizi mengine,” anaeleza na kuongeza kuwa

“Pia itamsaidia mama kujiongezea kipato badala ya kutupa taka hizo atatumia kutengeneza kitu kingine hivyo kufanya mazingira kuwa safi na kujiingizia kipato pamoja na kuwalinda viumbe wa majini wasiweze kuathirika,” anaeleza Adventina.

Wadau wa uvuvi wanena

Mwenyekiti wa Taasisi ya Muungano wa Wavuvi(FUO),Juvenary Matangili anaeleza kuwa katika kukabiliana na uchafuzi wa maziwa ni kuweka sheria kuwa mtu au mvuvi kwenye kambi yake akibanika ana chupa za plastiki au taka zozote za plastiki zinaelea katika kambi achukuliwe hatua ikiwa ni pamoja na kufutiwa leseni ya uvuvi.

Katika kambi za uvuvi zinakofanyika shughuli za uvuvi kuwe na eneo moja la kukusanyia taka ikiwemo za plastiki.Ili ata kama kuna ambazo zimeingia katika fukwe watu waeneo husika waziondoe na kuziweka katika kitu cha kukusanyia taka kisha wahusika wa mazingira watakuja kuchukua na kuzipeleka mahali panapo stahili hali hii itasaidia kuondoa au kupunguza changamoto ya taka za plastiki katika maziwa makuu.

“Tunatakiwa taka za plastiki pamoja na nyavu zote zikusanywe sehemu moja pia ziwekwe sheria zikikutwa taka hizo kwenye kambi yako unafutiwa leseni nani hatakubali kuacha taka hizo zielee ovyo, seriakali ikaze kabisa katika jambo hilo kwani ukipita katika visiwa vyote ndani ya ziwa Victoria unao taka za plastiki zinavyoelea,” anaeleza Matangili na kuongeza kuwa

“Nimeanza uvuvi mwaka 1964 daaga zinaingia Ziwa Victoria mwaka 1966 ndio tumeanza kuvua dagaa na mimi ni miongoni mwa watu wa mwanzo kuvua dagaa,taka za plastiki kwa sasa ziangaliwe kwa jicho jingine ili kudhibiti upotevu wa samaki,”.

Pia anaeleza kuwa kwa sasa asilimia 95 ya uvuvi ndani ya ziwa Victoria unatumia betri ambazo zinafungwa na kamba za plastiki(nailoni) ambapo mawimbi yakija betri zinadondoka ndani ya ziwa.

“Sasa hili hatulioni tumeona vyuma,nyavu lakini sasa hivi kuna wimbi la betri kudumbukia ndani ya ziwa Victoria hili nalo ni la kufanyia kazi katika kuhakikisha tunaokoa viumbe maji na ikolojia ya ziwa kuwa salama,”anaeleza Matangili.

Sanjari na hayo elimu inapaswa kuendelea kutolewa zaidi kwani kuna baadhi ya watu wanafikra potofu huku akitolea mfano kuwa wanaenda katika mialo na kuwakusanya BMU ili kufanya usafi wengine wanajibu kuwa nyinyi mmeisha kula fedha hivyo fikra zao zipo kwenye fedha kitu ambacho ni uongo badala ya kuangalia namna ya kulinda rasirimali hiyo ya ziwa.

Muonekano wa bustani ya mboga ambayo imetengenezwa kwa taka za plastiki lengo ni kudhibiti uchaguzi wa mazingira hususani katika maeneo ya maziwa makuu

Hatua ambazo serikali imechukua katika kudhibiti taka za plastiki

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Emily Kasagara,wakati akifungua kikao kazi cha kuwasilisha matokeo/mrejesho wa kampeni ya fukwe safi maziwa makuu kilichofanyika jijini Mwanza anaeleza kuwa serikali imechukua hatua mbalimbali za kukabiliana na changamoto hiyo ikiwemo kupiga marufuku uzalishwaji wa mifuko ya plastiki.

Marufuku hiyo ambayo imemsaidia kupunguza tatizo na itaendelea kusimamia kupitia Wizara husika kuhakikisha taka hizo zinadhibitiwa.

Anaeleza kuwa licha ya jitihada za serikali katika kudhibiti taka ngumu ikiwemo za plastiki lakini zimekuwa zikiongezeka kila siku kutokana na shughuli za kila siku ikiwemo kijamii, kiuchumi, usafirishaji na nakadhalika.

“Tafiti zinaonesha kuwa kama hali hii itaendelea bila kudhibiti taka hizi za plastiki kuingia katika maziwa na bahari,tusipo chukua hatua za makusudi kufikia 2050 basi ndani ya ziwa na bahari tutakuwa na taka nyingi kuliko samaki hivyo uchumi wetu wa bluu utakuwa umeathiriwa na adhima ya serikali kushindwa kufikiwa.