November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RAS Mara awataka walimu kuboresha elimu msingi

Na Raphael Okello, Timesmajira Online,Bunda.

KATIBU Tawala Mkoa wa Mara, Msalika Makungu amewaasa walimu wakuu kusaidia kuboresha elimu ya msingi nchini.

Makungu ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Walimu Wakuu wa shule za msingi kutoka halmshauri tano za Mkoa wa Mara yanayofanyika katika chuo cha Ualimu Bunda.

Katibu tawala wa mkoa wa Mara, Msalika Robert akifungua mafunzo hayo katika chuo cha Ualimu Bunda mkoani Mara

Mafunzo hayo ambayo ni moja ya mradi wa BOOST unalenga kuboresha utendaji kazi, uongozi na usimamizi katika miradi ya elimu kwa kuacha kufanyakazi Kwa mazoea.

“Ukiiona uongozi ni kazi rahisi basi wewe utakuwa hufanyi kinachotakiwa kufanyika, uongozi ni dhamana na mafunzo haya yawasaidie katika kuboresha utendaji, usimamizi na uongozi wenu katika shule zenu tuone mabadiliko,”amesisitiza Makungu.

Ameeleza kuwa endapo Walimu Wakuu watatimiza wajibu wao vizuri ni dhairi kuwa maboresho katika elimu yataonekana wazi na watu watajua kuwa shule zinaongozwa na viongozi walioiva vizuri.

Ameongeza kuwa walimu wakuu wataweza kusimamia vizuri ufundishaji, watumishi wenzao, rasilimali na miradi ya maendeleo katika shule wanazosimamia

Ameeleza kuwa serikali imeboresha miundombinu, idadi ya walimu na watumishi, mishahara na madai mbalimbali yamelipwa vizuri na kwamba kikubwa ni Walimu Wakuu kuonesha mfano katika kusimamia maneno yao ili nchi inufaike na uwekezaji mkubwa katika sekta ya elimu.

Kaimu Katibu Tawala msaidizi Elimu wa Mkoa wa Mara , Judith Mrimi akisema jambo kwa washiriki ambao ni Walimu wakuu walihudhuria mafunzo hayo ya BOOST katika chuo cha Ualimu Bunda .

Aidha, amewataka Walimu Wakuu kutoa taarifa kwa viongozi wa Halmashauri na Mkoa pale wanapoona wanaingiliwa na watu wengine kutoka nje ya mfumo wa elimu katika manunuzi ya vifaa na utendaji wao wa kila siku.

Kaimu Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Elimu , Judith Mrimi amesema mafunzo hayo ni utekelezaji wa hatua namba nne ya mradi wa BOOST ambayo unalenga kuboresha uongozi na usimamizi katika elimu.

Amesema lengo kuu la mafunzo hayo ni kuboresha uongozi, usimamizi na uendeshaji wa shule za msingi katika Mkoa wa Mara ambapo amewaomba walimu kujifunza na baadaye kuyafanyia kazi mafunzo waliyopewa.

Mafunzo hayo kwa Walimu Wakuu wa shule za msingi yametolewa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia mradi wa BOOST na kutolewa na wakufunzi kutoka Chuo cha Uongozi wa Elimu, Bagamoyo (ADEM) na Maofisa Elimu Taaluma wa Halmashauri zilizohusika.

Mafunzo hayo ya siku tatu kwa awamu ya kwanza yamewahusisha Walimu Wakuu 415 kutoka shule za msingi za Halmashauri tano za Mkoa wa Mara.

Baadhi ya Walimu Wakuu wakifuatilia jambo katika mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo wa usimamizi wa shule uliofadhiliwa na benki ya Dunia kupitia mradi wa BOOST

Halmashauri hizo ni halmashauri ya Mji wa Bunda, Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, Halmashauri ya Wilaya ya Musoma na Manispaa ya Musoma.

Kwa awamu ya pili mafunzo kama hayo yatafanyika katika Mji wa Tarime na kuhusisha walimu Wakuu kutoka shule za msingi za Halmashauri za Tarime Mji, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti na Halmashauri ya Wilaya ya Rorya.