November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TARURA kuunganisha Iringa, Morogoro kupitia Kilolo       

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeanza kazi ya kuunganisha mkoa wa Morogoro na Iringa kupitia Wilaya ya Kilolo baada ya kufungua Barabara ya Mhanga–Mgeta yenye urefu wa kilomita 17.5 ili kuwezesha wananchi kusafiri kwa urahisi na kufikisha mazao yao sokoni.

Meneja wa TARURA Mkoa wa Iringa, Mhandisi Makori Kisare  alisema kuwa lengo la kufungua barabara hiyo ni kuunganisha Mkoa wa Morogoro na Iringa ambapo hapo awali ilikuwa haipitiki kutokana na milima mikali na imegharimu kiasi cha shilingi milioni 282 ambapo  kwa sasa magari yameanza kupita na ujenzi wa vivuko  unaendelea sehemu zenye mito.

“Tumeweza kufungua barabara hii baada ya maombi ya wananchi wakiongozwa na mbunge wao wa jimbo la Kilolo, Justine Nyamoga , eneo hili ni wazalishaji wakubwa wa ndizi, maharage na mazao mengine pia wazalishaji wakubwa wa hewa ukaa hivyo kukosekana kwa barabara hii wananchi walikuwa wanapata shida, barabara hii ikikamilika itakuwa kiungo muhimu kwani sasa wananchi wanatembea takribani km 40 ili waweze kufika eneo la Morogoro”, alisema Mhandisi Makori.

 Claston Kikoti Mkazi wa kijiji cha Mwanga aliishukuru Serikali kupitia TARURA kwa ujenzi wa barabara hiyo kwani itawasaidia kusafirisha mazao kwenda mjini na kupata urahisi wa usafiri kwenda Morogoro hadi Dar es Salaam.

“Sisi wakazi wa huku usafiri wetu rahisi wa kwenda Dar es Salaam ni kwa kutumia treni hivyo barabara hii ikikamilika itarahisisha usafiri wa kwenda mjini kufanya biashara kwani biashara zetu hazitaishia Mgeta tu”, alisema Claston.

Wilaya ya Kilolo inatarajia kutumia takribani Shilingi Bilioni 2.7 kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kufanya matengenezo ya barabara ili kuwezesha wananchi kufika kusiko fikika.