Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amewataka
viongozi wa ngazi mbalimbali nchini kwenda kwenye maeneo ya wananchi
kwa ajili ya kutoa huduma, kusikiliza kero zao na kuzitatua.
Amesema hayo tarehe 28 Septemba, 2023 katika Kijiji cha Nyakanazi
Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera akiwa njiani kuelekea wilayani
Ngara kuwasha umeme vijijini pamoja na kuhudhuria Mkutano wa Mawaziri
wa Nishati kutoka nchi za Tanzania, Burundi na Rwanda wanaohusika na
Mradi wa umeme wa Rusumo utakaozalisha megawati 80.
“Viongozi wenzangu tutoke maofisini na tuwafuate wananchi walipo,
haina maana yoyote kama kuna kiongozi hapa na kuna shida ipo na
haijawahi kutatuliwa, Mhe, Rais anachotaka ni wananchi hawa
kusikilizwa na kama kuna kero sisi tuzimalize kabla yeye hajaja,
wananchi wakisema kuna shida sisi tuzimalize, yeye kazi yake kubwa ni
kutafuta fedha kwa ajili ya maendeleo.” Amesema Dkt.Biteko
Aidha, Dkt.Biteko ameendelea kusisitiza kuhusu matumizi sahihi ya
fedha za Serikali ili wananchi wapate huduma stahiki na hivyo
kuwapunguzia kero wanazopata wakati wakijiletea maendeleo.
Katika hatua nyingine, Dkt.Doto Biteko ameagiza Wakala wa Nishati
Vijijini (REA) kupeleka umeme kwenye eneo la Kabulaishoke katika
kijiji cha Nyakanazi baada ya viongozi wa eneo hilo kumweleza kuwa
bado halina umeme; ambapo Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan
Saidy amemuahidi Naibu Waziri Mkuu kuwa, mkandarasi, kampuni ya
Nakuroi ataanza kazi katika eneo hilo ndani ya mwezi mmoja.
Aidha, Dkt.Doto Biteko ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO),
kuwa na mpango maalum wa kusambaza umeme kwenye eneo hilo la Nyakanazi
kutokana na kupitiwa na miundombinu ya umeme kutoka kituo kikubwa cha
umeme cha Nyakanazi ambacho kinasambaza kwenye maeneo mengine ya nchi.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Mkuu, amekagua kituo cha umeme cha
Nyakanazi ambacho kitapokea umeme kutoka mradi wa wa umeme wa Rusumo
kupitia njia ya msongo wa kV 220 na kusambaza kwenye maeneo mbalimbali
ya nchi.
Akiwa kituoni hapo, Dkt.Biteko amezungumza na vijana wa
kitanzania wanaoendelea na ujenzi wa eneo kutakapowekwa mtambo wa
kupoza umeme kabla ya kuwasambazia wananchi ambapo amewaeleza vijana
hao kuwa, kazi wanayofanya ni kwa ajili ya heshima ya nchi kwani umeme
kutoka kituo hicho utahudumia wananchi.
Ameongeza kuwa, Serikali inathamini nguvu kazi wanayotumia kwani umeme
kutoka kituo hicho utaenda kwenye maeneo mbalimbali ya nchi ikiwemo
Biharamulo, Geita ,Shinyanga na Kigoma ili kupunguza changamoto ya
kukatika kwa umeme mara kwa mara.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi