November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jokate: ujenzi wa shule mpya umewarudisha wanafunzi shuleni

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online, Korogwe

MKUU wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga Jokate Mwegelo amesema miradi ya shule mpya kwa msingi na sekondari, imesaidia kuwarudisha shule wanafunzi waliokata tamaa kwenda shule kutokana na umbali mrefu.

Ameeleza kuwa wanafunzi kutoka Kata ya Foroforo iliwalazimu kutembea kilomita 22 kila siku ili kwenda shule ya sekondari Magoma na kurudi nyumbani, jambo lililofanya baadhi yao kuacha shule na wengine kukosa ari ya kusoma na kujiendeleza kielimu.

Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Jokate Mwegelo akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua ujenzi wa shule mpya ya sekondari Kata ya Foroforo Septemba 26, 2023

Joketi ameyasema hayo Septemba 26, 2023 baada ya kufika shule mpya ya sekondari Kata ya Foroforo ambapo amesema Serikali imetoa milioni 584.2 kwa ajili ya kuanzisha shule mpya ya sekondari ambayo wanajengwa vyumba 8 vya madarasa na jengo la utawala.

Vingine ni maabara tatu za kemia, fizikia na baiolojia, chumba cha TEHAMA, maktaba, vyoo matundu 10, kichomea taka pamoja na shimo la ardhini kwa ajili ya kujenga kisima cha maji ya kunywa.

“Wengine waliacha shule, sababu nimeelezwa kutoka kwenye baadhi ya vijiji (Kwenkeyu na Lutindi) hadi kufika Sekondari ya Magoma ni kilomita 11, hivyo kwenda na kurudi ni kilomita 22,”ameeleza Joketi.

Mabweni mapya Shule ya Sekondari Mnyuzi

Joketi ambaye alitembelea miradi ya elimu Tarafa ya Magoma ili waweze kukamilisha miradi hiyo Septemba 30, mwaka huu, amesema hataki kusikia fedha zimeisha na mradi umebaki.

Anataka kuona fedha zilizopelekwa kwa ajili ya miradi ya shule na afya inamalizika kwa fedha zilizopangwa sababu miradi mingi ndani yake kuna nguvu za wananchi.

“Miradi imalizike kwa fedha zilizopo, sitaki fedha zimalizike mradi bado,fedha hizi zinakuja kwa muongozo mahususi, hivyo sitaki kuona zinatumiwa nje ya malengo yaliyokusudiwa au kubadilisha matumizi yake” amesema Joketi.

Vyumba vipya vya madarasa Shule ya Sekondari Mnyuzi

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza ziara hiyo, Joketi amesema ameridhika na ujenzi wa miradi kwenye wilaya hiyo hasa ya elimu na afya, ameweza kupambana kuona miradi viporo inakamilika na hataki tena kuona Korogwe inakuwa na miradi isiyoisha.

Akizungumza na mwandishi wa habari, Diwani wa Kata ya Foroforo Ernest Kulangwa amesema hadi sasa mradi huo wa shule unakwenda vizuri ambapo baadhi ya majengo yanasubiri kupauliwa, mengine yapo kwenye linta na mengine msingi, lakini tayari vifaa vyake vipo.

Moja ya mabweni mapya Shule ya Sekondari Magoma

Joketi pia alitembelea shule ya sekondari Mnyuzi kuona ujenzi wa mabweni na vyumba vya madarasa,kuangalia ujenzi wa shule ya msingi mpya iliyopo Kitongoji cha Magunga, Kijiji cha Makumba, Kata ya Makumba, ambayo serikali imetoa milioni 348.5, na imeshapauliwa, na sasa inawekwa madirisha.