Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
MAMLAKA ya MajiSafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA) imepata zaidi ya bilioni 15 kutoka Tume ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) kwa ajili kutengeneza mfumo mzuri wa uondoshaji maji taka kwa wakazi wa maeneo ya milimani jijini hapa.
Hayo yamebainishwa Septemba 26, mwaka huu katika ziara ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Stephen Byabato jijini Mwanza.
Ziara hiyo ambayo imejikita kwenye ukaguzi wa miradi mbalimbali inayotekelezwa kwa ushirikiano wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ukiwemo mradi wa usafi wa mazingira unaofadhiliwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania, Serikali ya Ujerumani kupitia Benki yake ya Maendeleo ya KfW na Umoja wa Ulaya (EU) chini ya uratibu wa LVBC kupitia programu ya pamoja ya usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji katika Bonde la Ziwa Victoria (LVB-IWRM).
Byabato amesema kuunganishiwa kwa huduma za mfumo huo wa uondoaji wa maji taka milimani zitafanywa bure kwa wananchi katika maeneo ambayo mradi huo utapita na mwananchi atapaswa kuwa akilipia gharama za uendeshaji wake.
“Kwa kaya ambazo hawajavuta maji watapatiwa huduma ya kuunganishiwa kwa sh 21000 ili kuwawezesha kuwa na urahisi wa kuondosha maji taka”alisema Byabato.
Akiwa katika ziara ya kukagua mradi wa uondoshaji maji taka Pasiansi uliogharimu kiasi cha bilioni 3.8 ambao umewezesha kaya 830 kuunganishiwa mfumo huo kwa urefu wa kilomita 26 amesema jumuiya hiyo imetoa tena fedha kwa ajili hiyo.
Sanjari na hayo Byabato amesema kuwa nchi zote za ukanda huo wa Afrika Mashariki zimejizatiti kuhakikisha zinafanya jitihada za dhati katika utunzaji wa mazingira pamoja na Ziwa Victoria.
Kaimu Mkurugenzi wa MWAUWASA Mhandisi Robert Lupoja amesema kutokana na Jiji la Mwanza kuwa na miamba na kufanya vyoo kuchimbwa kwa kina kifupi hivyo kuwa na mfumo wa kuondosha maji taka ni muhimu.
Amesema jitihada za kuondosha maji taka milimani zilianza mwaka 2013,mpaka sasa baada ya utekelezaji wake hakuna changamoto yoyote iliyojitokeza.
Mhandisi Lupoja amesema kuwa miji iliyopo milimani nyakati za mvua walikuwa wakifungulia vyoo hivyo vinyesi kuteremka chini hali ilio sababisha tishio la afya kwa watu.
Pia amesema katika awamu inayoanza kaya 1600 zitapangwa kwenye mfumo huo ambapo maeneo yaliyonufaika na yayakayonufaika na mradi huo ni Pasiansi, Kilimahewa, Mabatini, Kitangiri na Igogo.
Naye mmoja wa wanufaika wa mradi huo William Mchomvu kutoka Pasiansi ameishukuru serikali kwa kuwezesha kupatikana kwa mradi huo kwani umeondoa changamoto ya madhara ya kiafya kwa watu.
More Stories
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili