November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Majaliwa awasimamisha kazi watumushi wanne forodha ya Mtukula

Ashura Jumapili Timesmajira Online,Missenyi

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi watumishi 4 katika kituo cha forodha cha pamoja Mtukula mpakani mwa Tanzania na Uganda.

Majaliwa ,amesema kuanzia leo Msimamizi wa kituo hicho kinachotumika kukusanya mapato kupelekwa makao makuu mara moja ili kupisha uchunguzi wa masuala ya ukusanyaji kodi.

Waliosimamisha kazi ni pamoja na Ofisa Mfawidhi wa kituo cha Forodha cha Mtukula Faisary Nasoro na wenzake Gerald Mabula, George Mwakitalu na Emanuel Mabula wote ni Maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika kituo hicho.

Anasema uamuzi huo unatokana na watumishi hao kuvidharau vyombo vya ulinzi na usalama vya Mkoa wa Kagera na Wilaya ya Missenyi pale wanapohojiwa kuhusu mifumo inayotumika kukusanya mapato pamoja kutoweka fedha za mapato zinazokusanywa katika mfuko mkuu wa mapato badala yake wanatumia mpaka huo kujinufaisha wenyewe .

Amesema kuwa serikali imekuwa ikiweka utaratibu wa kukusanya fedha katika mfuko wa pamoja ili fedha hizo kufanya maendeleo lakini Mkuu wa kituo hicho cha Forodha amekuwa haweki fedha katika mfuko huo badala yake anaweka fedha nyingine zinazokusanywa katika mfuko wake.

Pia amesema mapumgufu mengine ni kero na vilio kwa wafanyabiasha wanaotumia mpaka huo wa Uganda na Tanzania kuwa baadhi yao wanalipia ushuru kwa asilimia 100 na baadhi wanalipa mapato kwa asilimia 2 tu hivyo mapato yanalipwa kwa ubaguzi mkubwa.

Aidha amesema kuwa uchunguzi wa kamati ya ulinzi na usalama ulibaini kuwa mykuu wa kituo cha Forodha Mtukula alikuwa akitoza ushuru kwa maboksi ya bidhaa zilizopita maboksi matatu kati ya maboksi 120,huku maroli yakipita kwa makubaliano ya kulipa kidogo serikalini na kumpa fedha ya mfukoni.

Vilevile Waziri Mkuu huyo amesema watumushi wengine wa kituo cha Forodha wamekuwa wakisuka mipango ya kupitisha bidhaa na kugawana fedha ,mamlaka zilipojitokeza kuchunguza walizuiliwa na kuwekewa vikwazo pamoja na kufanyiwa dharau.

Ambapo amesema watumishi hao hawafai kuwa watumishi wa umma na watachunguzwa na mamlaka za nidhamu na kuchukuliwa hatua Kali.

“Watumishi mmekosa uadilifu,mnakusanya mapato kwa maslahi yenu na maamuzi yenu bila kufuata sheria ,mmepoteza uadilifu wa utumishi,mnataka kujinufaisha bila kujali masilahi ya wananchi ,vyombo vya ulinzi na salama vinadharauliwa hakuna atakaye vumilia hilo lazima watumishi wafanye kazi kwa miongozo na sheria za utumishi,naomba niseme serikali itaendelea kuwashughulikia,”amesema Majaliwa.

Changamoto nyingine ambayo Waziri Mkuu huyo ametaka ishughulikiwe ni uwepo wa scana ya kukagua mizigo inayovuka mpaka wa Mtukula kwani wafanyabiasha wanaopitisha mizigo hulazimika kushusha mizigo ili ikaguliwe na kupakiwa tena jambo ambalo linapoteza muda mrefu wa kibiashara na linakwamisha uchumi.

Aidha amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Kagera kwa kuchukua hatua kwa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi wanaohusika na ukusanyaji wa mapato ambapo watumishi watatu kutoka kitengo cha mapato,Ofisa Misitu,Ofisa Wanyamapori ambao walikuwa wakichukua mapato ambayo wanayoyakusanya bila kuyafikisha katika halmashauri hiyo hivyo amewaagiza viongozi wa mkoa kuchukua hatua kali ya sheria

Sanjari na hayo ameagiza kusimamimishwa kazi kwa wakusanya ushuru 6 wa Mnada wa Bunazi ambao wamekuwa wakileta elfu 30 kilawanapokusanya ushuru katika soko la Bunazi na kuwataka kurejesha fedha za Julai na Agosti mara moja.

Huku ameagiza kuwa hakuna mtumishi kuhamishiwa katika vituo vingine vya kazi na fedha zote zirejeshwe katika Halmashauri.

“Soko la Bunazi ni kubwa sana mtumushi aliyeaminiwa anaenda kukusanya ushuru asubuhi hadi jioni na kuleta shilingi elfu 30 katika Halmashauri wakati vyombo vya ulinzi na usalama wakisimamia kwa siku wanakusanya milioni mbili hii ni aibu kubwa sana lazima tujishangae na tuone aibu ,sijui mnakwama wapi niseme hivi hakuna atakayedanganya na akabaki,”amesema