Na. Mwandishi wetu Jeshi la Polisi
Jeshi la Polisi limetembelea Hifadhi ya Taifa ya Arusha lengo likiwa ni kujionea vivutio vinavyopatikana katika hifadhi hiyo ambayo inapatikana ndani ya Mkoa huo sambamba na kuhamasisha watu kutembelea vivutio hivyo.
Akiongoza zoezi hilo kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi hilo, CP Awadh Haji amesema wameona fahari kutembelea hifadhi hiyo yenye vivutio mbalimbali ikiwa ni kuunga juhudi za Rais Samia za kuutangaza utalii wa nchi.
CP Awadh alibainisha kuwa ziara hiyo itachangia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha uhusiano, kutatua changamoto za kiusalama baina ya jeshi hilo na wadau wengine wanaohusika moja kwa moja kuhudumia watalii.
Amesema jeshi hilo limeingia mkataba wa ushirikiano na Chuo cha Taifa cha Utalii ili kuwajengea uwezo wa kiutendaji Maofisa, Wakaguzi na Askari ili kuhakikisha wanakwenda kutoa huduma bora kwa watalii na wageni wote wanaofika nchini.
‘’Dhamira ya Rais na Amiri Jeshi Mkuu ni kukuza Utalii wa nchi yetu kwa kuongeza idadi ya watalii nchini,sisi Jeshi la Polisi tutahakikisha tunaenda kutoa huduma bora kwa watalii na wageni wanaofika nchini sambamba na kuimarisha usalama wao,”amesisitiza CP Awadh.
Kwa upande wake Mhifadhi wa hifadhi hiyo ACC Yusta Kiwango amesema wamekua na uhusiano mzuri na jeshi la Polisi ambapo mara nyingi hufanya operesheni za pamoja hali ambayo inasaidia watalii wanaotembelea hifadhi hiyo kufurahia mandhari bila ya uwepo wa changamoto za kiusalama.
Aidha ametoa wito kwa taasisi nyingine za serikali na za binafsi kutembelea hifadhi hiyo ili kujionea vivutio vilivyopo sambamba na kuutangaza utalii wa nchi.
Ziara hiyo imekuja mara baada ya Jeshi hilo kuingia mkatabata wa ushirikiano na Chuo cha Taifa cha Utalii jana jijini Arusha ambapo maafisa wa Jeshi hilo watajengewa uwezo wa kiutendaji wa namna bora ya kuwahudumia watalii.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi