Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Lushoto
MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga Mwantumu Zodo amesema Serikali ya itaendelea kuunga mkono juhudi za wananchi ili kuboresha huduma za jamii baada ya kuona wananchi wa Wilaya ya Lushoto wanajitoa sana kwenye shughuli za maendeleo hasa kwenye kujenga miundombinu ya elimu, afya na barabara.
Akizungumza kwa nyakati tofauti kwenye Kata za Mwangoi na Hemtoye katika Jimbo la Mlalo wilayani Lushoto, amesema wananchi hao wameonesha kupenda maendeleo, hivyo Serikali ya itaendelea kuunga mkono jitihada hizo.
Zodo amesema kwa miradi ambayo wananchi hawawezi kuchangia kama umeme, maji na barabara,Serikali itafanya juhudi miradi hiyo iweze kuwafikia kwa kupeleka miundombinu vijijini huku ile miradi ya elimu na afya ambayo wananchi wamejitolea sana halmashauri na Serikali Kuu wataboresha huduma.
“Nimeona wananchi wa Lushoto ni watu wanaojituma kwenye kujenga miundombinu hasa ya afya na elimu,tangu nimeanza ziara yangu nimekuta wamejenga vyumba vya madarasa na zahanati kwenye maeneo yao,”amesema Zodo.
Kufuatia jitihada walizoonesha wananchi Mbunge huyo amewaunga mkono kwa kutoa mifuko ya saruji 50 kwa Shule ya Msingi Kwefivi iliopo kijiji cha Mwangoi na Zahanati ya Mangika Kata ya Hemtoye mifuko ya saruji 50.
Zodo amesema kwa upande wa umeme, Serikali imepeleka umeme kwenye vijiji vyote viwili vya Kata ya Mwangoi, Kijiji cha Majulai na Mwangoi.
Pia amesema umeme umefika kwenye baadhi ya vitongoji ambapo kati ya vitongoji 23 vya Kata ya Mwangoi, vitongoji 14 vina umeme huku tisa bado havijapata umeme.
“Nchi hii ni kubwa na mipango ya Serikali ilikuwa ni kwanza kuweka umeme kwenye vijiji takribani 12,000 nchi nzima halafu ndiyo ihamie kuweka kwenye vitongoji, lakini ninyi mmepata bahati mpaka vitongoji vina umeme wakati sehemu nyingine vijiji havijafikiwa na umeme,” amesema Zodo.
Akiwa Kijiji cha Mangika Kata ya Hemtoye, Zodo amesema ipo haja ya fedha kutoka Serikali Kuu zikamaliza ujenzi wa zahanati ya Mangika ilioanza ujenzi wake mwaka 2015 ambapo wananchi walichangia kiasi cha milioni 15 na nguvu zao hivyo ameiomba TAMISEMI ikamilishe.
Ambapo amemueleza Kaimu Mkurugenzi Mtendaji pamoja na Kaimu Mganga Mkuu, hawatendei haki wananchi hao ambao wameonesha jitihada kwa kuchangia kiasi hicho cha fedha lakini mpaka sasa ni miaka minane zahanati haijakamilika na ikizingatiwa Jiografia ya eneo hilo ilivyo ni milima hivyo mjamzito anaweza kujifungulia njiani.
“Mpaka sasa, zahanati hii imeshatumia milioni 15 za wananchi na milioni nne za Mfuko wa Jimbo ndizo zikaezeka haya mabati, lakini bado haitoshi ili kukamilisha zahanati na vifaa vyake zinahitajika milioni 80, jengo pekee yake linahitajika kiasi cha milioni 50, hivyo tunaomba fedha hizi ziweze kutafutwa na kumaliza hili tatizo,” amesema Zodo.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Meshack Ikera amesema zahanati ya Mangika ipo kwenye mpango wa kuombewa kiasi cha milioni 50 kutoka TAMISEMI huku jumla ya zahanati tano wameziombea fedha.
Naye Mbunge wa Jimbo la Mlalo Rashid Shangazi amesema mradi wa maji wa Kata nne za Mlalo, Mwangoi, Dule B na Kwemshasha zitamaliza kiu ya maji kwa eneo hilo huku milima ambayo haina maji, watachimba maji ardhini.
More Stories
Mwanasheria Mkuu apiga kura uchaguzi wa serikali za mitaa
CHADEMA yasikitishwa mawakala wao kuzuiliwa
Rais Samia amlilia Dkt. Ndugulile