November 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya KCB yaadhimisha Mara Day

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

BENKI ya KCB Tanzania, imeshiriki katika Siku ya Mara Day iliyoandaliwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ili kuendeleza uhifadhi wa Bonde la Mto Mara ambapo Jumla ya miti 6, 000 ilipandwa.

Akizungumza na waandishi wa Habari Mkoani Mara, Naibu Waziri wa Maji-Eng.Maryprisca Mahundi aliipongeza Benki hiyo kwa kushiriki katika maadhimisho hayo na kuonyesha juhudi kubwa za utunzaji mazingira.

“Kwenye miradi yetu ambayo Rais Samia anatoa fedha nyingi kutekeleza miundombinu mbalimbali tunahitaji sana vyanzo vya maji”

“Sisi urafiki wetu ni kwa yule aliyeshiriki kuona namna utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji unawezeshwa”

Aidha aliiomba Benki ya KCB kuwapa wanawake mikopo rafiki ili waweze kuendelea kuizalisha katika maeneo mbalimbali ya kimaendeleo.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi na Biashara KCB Bank, Abdul Juma alisema KCB wamekuwa na mahusiano mazuri na wenzao kutoka Afrika Mashariki ambapo wameshirikiana nao katika upandaji miti ili kuendelea kutunza mazingira katika mto Mara.

“Sisi kama wadau wao leo tunawaunga mkono kwenye kupanda miti ili kutunza mazingira katika mto Mara”

Maadhimisho hayo hufanyika kila mwaka ili kuwakusanya wadau mbalimbali katika shughuli za uhifadhi wa mazingira pamoja na taasisi binafsi.