Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula ameishauri Mamlaka ya MajiSafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA) kuja na mkakati wa kuboresha miundombinu ya maji iliopo ardhini(mtandao wa mabomba ya usambazaji maji) ili iendane na kasi ya maji yanayozalishwa sasa na kudhibiti upotevu wa maji.
Dkt Angeline alitoa ushauri huo wakati akitoa salamu za Jimbo la Ilemela katika hafla ya majaribio ya awali ya mradi wa chanzo kipya cha maji Butimba ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 96,uliofanyika kwenye chanzo hicho jijini Mwanza.
Ambapo ameeleza kuwa baada ya kupata vyanzo vya maji waone mkakati mkubwa wa miundombinu iliopo ardhini iende sambamba na kasi ya maji yanayozalishwa sasa kwani mabomba mengi yamekuwa yakipasuka.
“Pamoja najitihada hizi inawezekana miundombinu iliopo ardhini na uzalishaji wa maji ambao upo pamoja na uboreshaji mnaofanya haujaweza kwenda sambamba mbali na miundombinu tunayoweka ya matanki,chanzo kuna haja sasa ya kuifumua mifumo na kuangalia mabomba yanayosambaza maji kama kweli yanaweza kukidhi mahitaji ndio maana mengi yamekuwa yakipasuka na nikushukuru Kaimu Mkurugenzi wa MWAUWASA kwa mfumo ulioweka mkipata taarifa mara moja mnaenda kushughulikia,”ameeleza Dkt.Angeline.
Sanjari na hayo ameeleza kuwa kulikuwa na changamoto na kilio cha maji katika Wilaya hizi mbili za Ilemela na Nyamagana lakini Ilemela ni zaidi kwa sababu ya changamoto nyingi zilizopo hivyo serikali ya awamu ya sita imekuwa ikitoa ahadi nyingi na ikatekeleza kwa awamu kama hivyo ambavyo wameona.
“Kwa taarifa ambayo ameitoa Kaimu Mkurugenzi wa MWAUWASA na namna ambavyo tumekuwa na changamoto tunahitaji sasa kuona kasi inakwenda kwa haraka katika kutekeleza yale yaliosemwa,”amesema Dkt.Angelina.
Aidha ameeleza kuwa chanzo cha maji walichokuwa wanakitumia cha Capripoint kilianza muda mrefu wakiwa na watu wasiofika laki tatu kwa Wilaya zote mbili Ilemela na Nyamagana walikuwa watu 221,209 lakini sasa wanaongele watu zaidi ya milioni 1 na chanzo ni kilekile.
“Na uzalishaji wake ulikuwa chini ya kiwango kwa mahitaji ya lita milioni 165, uzalishaji ulikuwa ni milioni 90 ni wazi lazima kilio kungekuwa kikubwa zaidi lakini kwa namna ambavyo tunaendelea na ongezeko lililopo ukiangalia watu 221,209 na watu zaidi ya milioni 1, kuna ongezeko la watu asilimia 399.3 lakini chanzo ni kile kile lazima kilio kilikuwa kikubwa,nafarijika kushuhudia majaribio ya mitambo haikuwa rahisi kuwaeleza wananchi waishio kando ya Ziwa Victoria kukosa maji wakati yanafika hadi Shinyanga,Tabora na maeneo mengine,”ameeleza Dkt.Angeline.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa MWAUWASA Neli Msuya, ameeleza kuwa wamepeleka andiko la chanzo kipya cha maji Kabanganja kitakachozalisha lita milioni 200 kwa siku kitakachojengwa kwa awamu mbili.
Pia wanaendelea na miradi ya haraka ya uboreshaji mifumo ya maji itakayogharimu kiasi cha bilioni 4.3,itakapokamilika yote itakidhi mahitaji ya wananchi.
“MWAUWASA imejipanga kufanya marekebisho kwa mabomba ya zamani ili kupunguza upotevu wa maji na kuendelea kuondoa mabomba madogo madogo ili kupunguza athari zinazotokana na kuongezeka kwa msukumo wa maji,”ameeleza Neli.
Naye mmoja wa wananchi Said Abdallah ameeleza kuwa kukamilika kwa mradi wa chanzo kipya cha maji Butimba unakwenda kutatua kero za maji kwa wananchi wa Nyamagana na kuifungua Mwanza kwa sababu utasaidia Usagara,Kisesa na baadhi ya Kata ya Ilemela.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â