November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Walimu 12 CBE wasomea akili bandia na usalama wa mtandao

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

CHUO cha Elimu ya Biashara (CBE), kimeingia makubaliano na Taasisi ya Teknolojia ya Habari JR Institute of Information and Technology ambao utakiwezesha chuo hicho kutoa mafunzo ya akili bandia na usalama wa mtandao.

Makubaliano hayo yalisainiwa jana kwenye chuo cha CBE baina ya Mku wa chuo hicho, Profesa Tandi Lwoga na Meneja wa JR Institute, Isack Marandu.

Akizungumza kwenye tukio hilo, Profesa Lwoga amesema ushirikiano huo utakuwa na manufaa makubwa kwa chuo hicho kwani taasisi ya teknolojia ya JR ambayo inafadhiliwa na taasisi ya Punjani Charitable Trust, imebobea kwa kiwango kikubwa kwenye eneo la teknolojia.

“Wamechukua walimu wetu 12 kwenye Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano TEHAMA ambao watawapa mafunzo yatajayotusaidia nasisi kuanza kufundisha masomo hayo kwenye mwaka wa masomo kuanzia mwakani,” amesema Profesa Tandi

Amesema walimu wa chuo hicho wanasoma masomo hayo kwa njia ya mtandao na wamekuwa wakisoma kozi tofauti tofauti ikiwemo ya akili bandia ambayo imekuwa hitaji kubwa kwenye sehemu mbali mbali duniani.

“Walimu wetu wanafanya Stashahada ya Juu ya intelijensia ya jamii, watatu wamekwenda kusoma stashahada ya juu ya usalama mitandao, wawili wanasoma Stashahada ya Juu ya uchambuzi wa taarifa na sayansi na mmoja anafanya Stashahada ya Juu ya intelijensia ya bishara,” amesema

Aidha, amesema walimu hao wa CBE watasoma kwa njia ya mtandao kwa muda wa miezi 12 na wakimaliza watakuja kuanzisha program hizo walizosomea kwajili ya kuanza kuwafundisha wanafunzi hao.

Amesema baada ya mafunzo hayo anatarajia CBE itaanza kutoa mafunzo yanayoendana sana na sayansi na teknolojia kwani dunia ya sasa inaendeshwa na teknolojia mbalimbali za kisasa ikiwemo ile ya akili bandia.

“Tunashukuru sana kwaajili ya huu ushirikiano ambao utajengea walimu wetu uwezo kwaajili ya kuanza kutoa mafunzo mafupi mafupi, kufanya tafiti mbalimbali na kutoa ushauri wa kitaalamu nasisi wakimaliza tutaanza kutoa mafunzo kama hayo hayo,” amesema Profesa Lwoga

Mkuu wa Idara ya Hesabu na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT), wa CBE, Dk. Ahmed Kijazi, ameushukuru uongozi wa chuo kwa juhudi za kuona umuhimu wa idara hiyo kwenda mbele katika teknolojia hiyo ya kisasa kama akili bandia na usalama mitandaoni.

Amesema wataalamu wa fani hizo ni wachache na kwamba anaminani uhusiano wa CBE na JR kutaboresha ufundishaji na kupata wahitimu wengi wa fani hiyo maeneo mengi nchini.

“Si kwamba hawa walimu wakihitimu watakuwa na manufaa hapa CBE tu, watakuwa na msaada nchini kwa ujumla kwasababu wataalamu ni wachache sana kwa hiyo watafundisha watu wengi na hatimaye tutapata wataalamu wengi wenye ujuzi wa aina hii,” amesema

Naye Meneja wa JR Institute, Isack Marandu amesema walimu wa CBE wanaendelea kupata mafunzo kwenye chuo hicho na kwamba wanatengeneza walimu ambao watakuwa msaada kwenye teknolojia ya kisasa kama ya akili bandia na usalama mitandao.