Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
WANAFUNZI waliohitimu kozi mbalimbali katika Chuo Cha Maendeleo ya Jamii Wilayani Kaliua Mkoani Tabora wamepongezwa kwa kuonesha weledi na nidhamu katika kutumikia wananchi kwenye nafasi za ajira walizopata.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI na Mbunge wa Jimbo la Mikumi Denice Lazaro alipokuwa akiongea na walimu, wanafunzi, wazazi na walezi katika mahafali ya 5 ya Chuo hicho.
Alisema mafunzo na malezi mazuri wanayopata chuoni hapo yamekuwa chachu kubwa kwa wahitimu wa chuo hicho kuwa mfano wa kuigwa mahali popote wanapopata fursa ya kuajiriwa.
‘Nimepata taarifa kuwa baadhi ya wahitimu wa chuo hiki waliopata ajira katika maeneo mbalimbali wanafanya vizuri sana na wana nidhamu ya hali ya juu, katika hili nawapongeza sana, endeleeni hivyo hivyo, msiige tabia mbaya’, alisema.
Londo alibainisha kuwa serikali imekuwa ikisisitiza watumishi wa umma kuwa na nidhamu katika utumishi wao lakini kama hawakufundwa vizuri walipokuwa chuoni ni vigumu kubadilika.
Aidha aliongeza kuwa Chuo hicho kina mchango mkubwa sana kwa maendeleo ya jamii kutokana na aina ya kozi zinazofundishwa ambazo huwapa ujuzi na fursa ya kujiajiri na kuajiriwa katika maeneo mbalimbali.
Kwa kutambua mchango mkubwa wa wahitimu wa mafunzo hayo, aliahidi kuwa wataendelea kuishauri serikali ya Rais Samia Suluhu kutoa kipaumbele cha ajira kwa wanafunzi wanaohitimu chuoni hapo na vyuo vingine ili wakasaidie jamii.
Awali akitoa taarifa kwenye mahafali hayo, Mkuu wa Chuo hicho Abdallah Hamis alisema jumla ya wanafunzi 195 wamehitimu na kufuzu katika fani mbalimbali hivyo kupata sifa na vigezo vya kutunukiwa stashahada ya chuo hicho.
Alitaja kozi zilizotolewa kuwa ni pamoja na Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii, Mipango, Rasilimali Watu, Ufundi Umeme wa Majumbani, Ufundi Bomba, TEHAMA na Ualimu wa Malezi ya Watoto.
Alibainisha kuwa kuanzishwa kwa chuo hicho kumechangia kuinua uchumi na kuongeza kipato kwa wananchi hususani wafanyabiashara na kukifanya kuwa tegemeo miongoni mwa jamii katika halmashauri hiyo, Mkoa na maeneo jirani.
Abdallah alifafanua kuwa chuo hicho kimekuwa mstari wa mbele kutekeleza ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kupambana na ujinga, maradi na umaskini kupitia elimu ya stadi za maisha wanayowapa vijana.
Naye Mbunge wa Jimbo la Kaliua Aloyce Kwezi alishukuru serikali ya awamu ya 6 kwa kutoa fursa kwa taasisi za elimu ya kati kuendelea kutoa mafunzo ya stadi mbalimbali kwa vijana ili kuwapa ujuzi utakaowasaidia kujikwamua kimaisha.
Alibainisha kuwa uwepo wa chuo hicho na fursa lukuki za utekelezaji miradi ya maendeleo inayoletwa na serikali ya awamu ya 6 unaifanya halmashauri hiyo kwenda mwendo wa 5G kimaendeleo.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi