November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TTCL yafanya mabadiliko makubwa utoaji wa huduma

Na Penina Malundo

SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL ) imesema
kwa sasa imefanya mabadiliko makubwa katika Kuboresha utoaji wa huduma zake ambapo imehakikisha miundombinu ya Mawasiliano ya simu kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) umeboreshwa ipasavyo.

Aidha imesema katika uboreshaji huo wa miundombinu yake, tayari kwa sasa inapakana kwa nchi takribani nane ikiwemo nchi ya Kenya, Congo, Rwanda,Burundi, Malawi na Uganda.

Akizungumza jana na Waandishi wa habari Mkurugenzi wa Biashara wa TTCL,Vedastus Mwita katika Kongamano la siku mbili la Connect 2 Connect (C2C) Visiwani Zanzibar, lililokutanisha wadau zaidi ya 250 wa Tehama ili kuelezana Ukuaji wa Teknolojia, fursa mbalimbali za Kibiashara pamoja na Ushirikano wa Kibiashara.

Amesema miongoni mwa uboreshaji huo wa miundombinu ni kuhakikisha huduma ya intaneti imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na uwepo wa Miundombinu imara inayotolewa na TTCL pamoja na kuhakikisha uhifadhi data kwa kutoa suluhisho na vifaa vya kutunza Data kwa kupitia kituo cha kutunza data Kimtandao (NIDC) kilichoidhinishwa na ISO.

“Kwa sasa sisi TTCL tunahakikisha tunakuwa ndio lango la huduma za E-serikali kwa kukaribisha miundombinu na huduma muhimu za ICT n pia lango la usalama wa kitaifa wa kielektroniki kwa kuimarisha usalama wa sekta ya mawasiliano,”amesema na kuongeza

“TTCL inaenda kuwa kama kitovu cha Mawasiliano nchini na itahakikisha huduma ya intaneti inapatikana katika kiwango cha juu katika kongamano hili la Kimataifa ili kuwawezesha wadau wa Kongamano kuweza kuperuzi kwa uharaka na urahisi zaidi,”amesema

Amesema, TTCL si tu mtoa huduma za mawasiliano ya simu bali ni mhusika Mkuu aliyepewa mamlaka ya kupanga, kujenga, kuendesha na kudumisha miundombinu ya kimkakati ya mawasiliano ya simu, ambayo inaweza kubadilika kulingana na mabadiliko ya kisasa ya kiteknolojia na miundombinu.