Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amesema Serikali za Afrika zinapaswa kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwapa wakulima wadogo pembejeo za bei nafuu, maarifa, ujuzi na mitaji ili kuongeza tija katika mnyororo wa thamani wa uzalishaji chakula.
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akifungua Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Barani Afrika kwa Mwaka 2023(AGRF) unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam. Amesema pamoja na mambo mengine Afrika inahitaji kutumia maarifa yaliyopo ya kisayansi ikiwa ni pamoja na teknolojia ya kiasili ili kuzalisha na kusindika chakula cha kutosha kwa ajili ya watu wake na masoko ya kimataifa.
Makamu wa Rais ameongeza kwamba ni muhimu kuendelea kufadhili tafiti za kisayansi, matumizi ya dijitali, kutambua mchango wa wanawake na vijana katika kilimo, pamoja na kuwavutia vijana kwa kuongeza matumizi ya teknolojia ya kisasa, upatikanaji rahisi wa ardhi, mitaji na masoko yanayolenga shughuli kama vile kilimo cha bustani ambacho kina matokeo ya haraka zaidi.
Pia Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa kuondoa ukandamizaji wa aina yeyote kwa wakulima ikiwemo kuhakikisha matumizi sahihi ya vipimo katika masoko ya mazao ya kilimo ili kuwalinda wakulima.
Makamu wa Rais amesema mageuzi katika mifumo ya chakula yanaenda sambamba na ukuaji wa sekta zingine ikiwemo usafirishaji wa bidhaa za chakula hivyo nchi za Afrika zinapaswa kuheshimu mipango ya biashara ya kikanda, hasa Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA), kwa kuzingatia itifaki za kibiashara na kuondoa vikwazo visivyo vya kiforodha.
Halikadhalika, Makamu wa Rais amesema ni muhimu mataifa ya Afrika na Dunia kwa ujumla kutumia njia za usuluhishi wa amani katika kukabiliana na migogoro mbalimbali kwa kuwa amani na usalama ni nguzo muhimu kwa mifumo ya chakula. Amesema idadi kubwa ya watu waliokimbia makazi yao sababu ya migogoro ambao ni pamoja na wakulima na wafugaji wametatizwa maisha yao na uwezo wao wa kuzalisha chakula.
Makamu wa Rais amesema Tanzania imechukua hatua mbalimbali za kuimarisha sekta ya kilimo ikiwemo kuongeza bajeti kwa asilimia 70 kutoka dola za marekani milioni 120 kwa mwaka wa fedha 2021/2022 hadi dola za marekani milioni 397 kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kwa lengo la kufanya Kilimo kuwa cha biashara na kuongeza ukuaji wa sekta ndogo ya mazao hadi asilimia 10 ifikapo mwaka 2030 kutoka kiwango cha sasa cha asilimia 5.4. Pia mpango huo unalenga kuboresha huduma za ugani na kuongeza uwekezaji katika sekta hiyo pamoja na kuhamasisha ushiriki wa vijana katika kilimo biashara kupitia kuanzisha kilimo cha umwagiliaji cha vitalu chini ya Programu maalum ya Jenga Kesho Iliyobora (BBT).
Vilevile Makamu wa Rais amesema Tanzania imeweka sera na mikakati ya kusaidia mifumo ya chakula na kutokana na utekelezaji wa sera na mikakati hiyo, Tanzania imekuwa na uwiano wa kujitosheleza kwa chakula wa asilimia 100 kwa zaidi ya miongo miwili. Ameongeza kwamba serikali ya Tanzania imeanzisha ufadhili wa gharama nafuu na wa muda mrefu wa kilimo kwa sekta binafsi ikiwa ni pamoja na kuanzisha kituo katika Benki Kuu ambacho kinaziwezesha benki za biashara kukopa kwa ajili ya kuendelea kuwakopesha wakulima kwa riba ya chini ya asilimia kumi.
Kwa upande wake Rais wa Jumuiya ya Mapinduzi ya Kijani Barani Afrika (AGRA) Dkt. Agnes Kalibata amesema Mkutano huo utajikita zaidi katika kujadili namna ya kujikwamua kutoka katika changamoto mbalimbali zinazokabili mifumo ya chakula, kuimarisha upya mifumo ya chakula pamoja na kuangazia hatua za kuchukua katika kukabiliana na changamoto za sekta ya kilimo Barani Afrika.
Aidha Dkt. Kalibata amemshukuru na kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada mbalimbali anazofanya kuhakikisha Afrika inatambua uwezo wa Tanzania katika mageuzi ya mifumo ya chakula pamoja na jitihada za nchi katika kuimarisha usalama wa chakula Barani Afrika.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa