November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

zaidi ya watu 4000 kushirki mkutano wa Jukwaa la mifumo ya chakula afrika.

Na David John,Timesmajira Online

WATU zaidi ya 4,000 kutoka sehemu mbalimbali Afrika wanatarajia kushiriki Mkutano wa Mifumo ya Chakula jijini Dar es salaam katika ukumbi wa kimataifa wa Julius Nyerere.

Mkutano huo wa 13 ambao unaaza septemba 5-8 mwaka huu ukiongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, utatoa fursa kwa viongozi, wataalam, wabunifu na wadau mbalimbali kujadili masuala tofauti yanayohusu sera, changamoto, mafanikio na ubunifu utakaoboresha sekta ya kilimo, mifumo na chakula.

Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam Septemba 3, 2023, Waziri wa Kilimo wa Tanzania, Hussein Mohamed Bashe, amewakaribisha wageni kutoka ndani na nje ya nchi, kuhudhuria mkutano huo wa siku nne.

Waziri Bashe Amesema mkutano huo ni hatua muhimu katika kuhakikisha bara zima la Afrika linakuwa na mifumo ya chakula endelevu na jumuishi.

“Mkutano wa mwaka huu unahimiza uwezeshaji wa wanawake na vijana, pamoja na kutambua umuhimu wao katika uzalishaji chakula barani Afrika,” amesema.

Pia Waziri Bashe aligusia jinsi serikali ya Tanzania inavyochukua hatua katika kuhakikisha upatikanaji wa chakula na kutengeneza ajira kupitia mpango wake wa BBT-YIA “Building a Better Tomorrow: Youth Initiative for Agribusiness (BBT-YIA)” ambao unalenga kutoa mafunzo kwa vijana 200,000 na kusaidia biashara za kilimo zipatazo 15,000 zinazofanywa na vijana, katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

“Mkutano huu utajadili namna ya kuongeza ajira za vijana kwenye mifumo ya chakula Afrika na kuonyesha biashara za kibunifu kwenye kilimo ambazo zinasimamiwa na wajasiriamali vijana.

Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF)ambalo limeandaa mkutano huo, Amath Pathe Sene, amesisisitiza umuhimu wa kushughulikia changamoto za mifumo ya chakula.

“Ni muhimu sauti zetu zisikike, tutoe masuluhisho yanayozingatia mazingira yetu na tutoe kipau mbele katika kuwawezesha wanawake na vijana katika mchakato wa kuboresha mifumo ya chakula,” amesema.

Mkutano huo pia unaandaa mjadala wa mifumo ya chakula kuelekea mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi (COP 28), utakaofanyika Dubai.

Mambo muhimu yatakayojiri katika mkutano huo ni pamoja na majadiliano ya wataalam, mkutano wa mawaziri zaidi ya 40, mkutano wa Wakuu wa Nchi ambao watatoa matamko yao kuhusu kuboresha mifumo ya chakula Afrika.

Mwisho.