Na Hamisi Miraji, Timesmajira Online
Unapozungumzia Ukataji wa miti ni mojawapo ya masuala ya kijamii na kimazingira yanayotisha zaidi wakati huu.
Kitendo cha kukata miti kinaitwa ukataji wa miti. Miti ni moja ya vipengele muhimu zaidi vya asili. Inachukua jukumu muhimu katika kudumisha usawa wa ikolojia.
Kwa sasa miti iko katika kundi la watu katili na idadi ya miti inapungua katika mazingira. Kama matokeo ya ukataji miti, tunaelekea kwenye hatari kubwa.
Ukataji wa miti ni changamoto katika jitihada za kulinda misitu hasa nchi zinazoendelea kwa sababu ya watu kukata miti kwa ajili ya mkaa, kuni pamoja na mbao .
Athari za ukataji miti ni nyingi na katika hatua za kukomesha ukataji miti haramu, Serikali ikiwemo ya Tanzania inachukua hatua ili kudhibiti hali hiyo ambayo inasababisha uharibifu wa mazingira unaopelekea upotevu wa bioanuai.
Hata hivyo inaelezwa kwamba, misitu inaangamia na kuteketea kutokana na umaskini ambapo hakuna namna misitu inaweza ikapona kutokana na kukithiri kwa ukataji miti kwa ajili ya mkaa ambao mahitaji yake ni makubwa hasa katika mkoa wa pwani ambako watu wamekuwa wakikata miti bila kufuata utaratibu.
Licha ya mahitaji hayo makubwa ya mkaa hakuna Sera ya Taifa inayotoa maelekezo ya namna gani mahitaji haya yaweze kufikiwa kwa njia endelevu bila kuathiri ikolojia na uchumi.
Umoja wa Mataifa unaendelea kuzihimiza nchi wanachama kuchukua hatua ili kukabiliana na athari za uharibifu wa mazingira ikiwa ni pamoja na kuacha ukataji miti hovyo kwa ajili ya uchomaji mkaa, kuharibiwa kwa vyanzo vya maji na uharibifu mwingine.
KWA NCHI YA TANZANIA
Kwa hali ilivyo nchini Tanzania takriban hekari 469,420 za misitu zinatazamiwa kupotea kila mwaka kutokana na ukataji wa miti ambao unaochochewa na shughuli za binadamu kutokana na matumizi ya kuni na mkaa.
Ripoti ya Tatu ya Hali ya Mazingira nchini ya mwaka 2019, inaonesha kuwa kasi ya uharibifu wa misitu ni kubwa na kila mwaka zaidi ya hekta 469,420 huharibiwa kutokana na ukataji wa miti kwa ajili ya matumizi ya kuni na mkaa.
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo inakadiriwa kuwa asilimia 16 ya ardhi imeharibika na inakabiliwa na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame kutokana na watu wengi kufanya shughuli zisizo endelevu, ikiwemo kutumia nishati ya kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia, kutokana na nishati hiyo kupatikana kwa urahisi na watu wengi wanaweza kumudu gharama yake.
Tathmini hiyo imedhihirisha wazi kwamba matumizi ya mkaa na kuni ndio chanzo kikubwa cha ukataji miti na hivyo hatua za haraka zichukuliwe kukabiliana na tatizo hilo.
Kwa hili muarubaini wa changamoto hiyo ni matumizi ya nishati mbadala, ikiwa ni agenda ambayo itaokoa raslimali za misitu na kimsingi ni muokozi wa maisha ya watanzania .
Nchini Tanzania kati ya hekari milioni moja ya miti inayokatwa, asilimia 70 ya miti hutumika kwa uzalishaji wa mkaa na hupelekea nchi yetu kuwa jangwa kwa asilimia 61.
TAKWIMU ZA WHO
Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), zinasema takribani watu milioni nne hufariki kila mwaka kabla ya wakati kutokana na matumizi ya moto na nishati ngumu katika kupikia.
”Matumizi ya mkaa majumbani na viwandani yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku kadri idadi ya watu inavyoongezeka, hali inayofanya athari yake katika mazingira kuonekana dhahiri.”
Uharibifu wa mazingira kwa kiasi kikubwa unaotokana na matumizi ya mkaa, ambao unatumiwa na karibu kila kaya .
Pamoja na uvumbuzi wa nishati mbadala kwa matumizi ya nyumbani, bado matumizi ya mkaa yanatarajiwa kuendelea kuongezeka katika miongo ijayo, hasa Barani Afrika kutokana na ongezeko la watu, ukuaji wa miji na bei za nishati mbadala kuwa juu. Pia uwezo duni wa kiuchumi wa wananchi katika mataifa yanayoendelea.
Hadi kufikia 2015, uzalishaji wa mkaa duniani ulikadiriwa kuwa tani milioni 52 kwa mwaka, na kati ya hizo asilimia huzalishwa Barani Afrika wakati Amerika ni asilimia 19.6.
Kati ya tani milioni 32.4 zinazozalishwa Afrika, asilimia 42 zinazalishwa katika ukanda wa Afrika Mashariki unaohusisha nchi za Tanzania, Uganda, Kenya, Rwanda na Burundi. Afrika Magharibi inazalisha asilimia 32, Afrika ya Kati (12.2), Kaskazini (9.8) na Kusini mwa Afrika ni asilimia 3.4.
Mikakati ya Serikali
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Alhaj Dkt. Suleiman Jafo anasema Tanzania inaendelea kuweka mikakati na sera endelevu za uhifadhi na usimamizi endelevu wa mazingira ikiwemo kuhamasisha zoezi la upandaji miti ili kukabiliana na athari za uharibifu wa mazingira mabadiliko ya tabia nchi.
Anasema, ajenda ya mazingira ni miongoni mwa vipaumbele muhimu vinavyoendelea kupewa msukumo na Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ikiwemo uhamasishaji wa kampeni za usafi wa mazingira na upandaji miti.
Kwa mujibu wa Waziri Jafo, hivi karibuni Tanzania imeshuhudia athari kubwa za mabadiliko ya tabia nchi ambazo ziliathiri sekta za uchumi na uzalishaji mali na kushuhudiwa kuongezeka kwa bei za bidhaa za mazao ya chakula, hali iliyotokana na ongezeko kubwa la ukame katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Sote ni mashahidi, tumeshuhudia mvua zisizo na wastani mzuri zikinyesha katika baadhi ya maeneo ambazo zilileta athari ikiwemo vifo.
Pamoja na hayo, ukame mkali katika wilaya ya Simanjiro, Longido na Kiteto hali iliyosababisha vifo vingi vya wanyama na kusababisha hali ya umaskini wa kipato kwa wafugaji” anafafanua Jafo.
Katika hatua nyingine, anaeleza Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imezitaka Taasisi zote za Umma na Binafsi Tanzania Bara zinazoandaa chakula na kulisha watu zaidi ya 100 kwa siku kusitisha matumizi ya kuni na mkaa ifikapo Januari 31, 2024.
Vilevile imezielekeza Taasisi zinazoandaa chakula na kulisha watu zaidi ya 300 kwa siku kusitisha matumizi ya kuni na mkaa ifikapo Januari 31, 2025.
Jafo anafafanua, watumiaji wakubwa wa nishati za kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia ni Taasisi za umma na binafsi, hivyo kutokana na athari zake kimazingira, kiafya, kijamii na kiuchumi, Serikali imeandaa Dira ya Taifa ya matumizi ya nishati safi ya kupikia na Mpango Mkakati wa Utekelezaji wa Dira hiyo kwa kipindi cha miaka kumi hadi kufikia 2033.
WIZARA YA NISHATI
Inakadiriwa kuwa, mahitaji ya mkaa bila ugavi na afua za mahitaji yataongezeka maradufu ifikapo mwaka 2030, kutoka takriban tani milioni 2.3 za mkaa mwaka 2012.
Ni dhahiri kwamba kuendelea kwa matumizi ya kuni na mkaa bila kuingilia kati kwa kiasi kikubwa kunahatarisha mazingira yetu.
Waziri wa Nishati January Makamba anangeza kusema, utekelezaji wa Nishati Safi ya Kupikia imezingatia miongozo mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa kama Sera ya Taifa ya Nishati ya mwaka 2015, pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia (SDGs-2030). Ambapo lengo namba 7 linazungumzia masuala ya upatikanaji wa nishati safi na bei nafuu.
Makamba anasisitiza, Dira hii inakataza matumizi ya mkaa wa asili ambao una athari kwa afya na mazingira, hivyo uwekezaji katika mkaa mbadala wenye viwango vinavyotakiwa uendelee.
WAFANYABIASHARA YA MKAA
Wakati Serikali ikipiga vita ukataji wa miti hovyo usiozingatia sheria, baadhi ya vijana wanaojishughulisha na biashara ya kubeba mkaa kwa kutumia bodaboda maarufu ( WAKUBETI ), Kibaha Vijijini, Mkoani Pwani, wananena kwamba, biashara hiyo ndio inayowaweka Mjini na kuhudumia familia zao.
Wanaeleza, biashara hiyo ni kimbilio lao, kwakuwa hawana ajira, inabidi wajitafutie kipato kujiendeleza kimaisha.
Kwakuwa wameshajidhihirishia biashara hiyo, wanajitetea na kulalama wakihitaji mapunguzo ya tozo zinazowakabili jambo linalosababisha kukwepa ushuru kwa kupita njia za panya.
Hatua hiyo huwa inasababisha )vijana hao, kuingia kwenye msuguano baina yao na doria za wakala wa misitu( TFS) na kuamua kukwepa ushuru.
Hosea Paulo na Yasin Rajabu ni miongoni mwa wafanyabiashara wa kubeba mkaa maarufu wakijiita (WAKUBETI) wanaeleza, biashara hiyo inawalipa licha ya changamoto ambazo huwa zikijitokeza hasa kwenye ushuru.
“Ushuru haueleweki 12,500 kipindi kingine tunapandishiwa, tukikaidi sheria inatubana, pikipiki zetu zinachukuliwa na kulipishwa faini tukienda kuzichukua, tozo tunaona ni nyingi zinatuzidia tunajikuta tunapata faida sh.18,000 kwa kiroba kitu ambacho hakikidhi hali ya maisha na wengine tuna familia “anasema Hosea.
Yasini anaweka bayana kuwa, kuna bei ya shamba ambayo nayo ni kubwa 90,000 wakati zamani walilipia 60,000 .
“Mimi ni mwanaume, familia yangu inahitaji huduma nzuri, huwezi amini ushuru na tozo mbalimbali tunazolipa sisi ni zaidi ya 160,000 hadi kufikisha mzigo sokoni, kwa hali hii ya utitiri wa ushuru hatuwezi kutoboa, tunashindwa na inabidi kufanya vurugu ili kuweza kumudu maisha.”
HALMASHAURI YA KIBAHA /TFS
Meneja wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) Kibaha, Mkoani Pwani, Aslam Juma anaeleza, hawana kikundi Chochote ambacho wamekisajili Wala bodaboda kuruhusu kubeba mkaa bila kufuata sheria na miongozo iliyopo.
“Hatuna kikundi tulichokisajili, hakuna bodaboda tunayoitoza ushuru, kifupi sisi hatuna geti”
Anasema, kwa mujibu wa sheria ya misitu na.14 ya mwaka 2002 na kanuni zake mfanyabiashara wa mkaa anatakiwa kulipa sh.250 kwa kila kilo ya mkaa au 12,500 kwa gunia lenye kilo 50.
Ameeleza, kwa mwaka huu bado hana takwimu sahihi ya tathmini ya makusanyo na hana idadi sahihi ya wavunaji mkaa hadi hapo watakapokaa kwenye kikao cha wavunaji.
Aslam, anawaasa wafanyabiashara wa mazao ya misitu kutimiza masharti ikiwemo kuwa na hati ya usajili, hati ya usafirishaji wa mazao ya misitu, leseni ya kuvuna mazao ya misitu, leseni ya biashara ikiwa ni pamoja na TIN namba na kulipia ushuru wa Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kisheria.
Anataadharisha atakayevunja masharti hayo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Upande wa Halmashauri, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kibaha, Erasto Makala anaeleza, tatizo la ukataji miti ni kubwa, hali ni mbaya hasa maeneo ya Kimaramisale Kata ya Dutumi na Kwala .
Anaeleza, vijana walio wengi wanatoka maeneo mbalimbali ikiwemo Kisarawe, Mlandizi, Dar es Salaam kujihusisha na biashara ya ubebaji mkaa bila kufuata sheria.
Makala anaeleza, Kimaramisale, Dutumi miti mingi inakatwa lakini jitihada kubwa zinafanyika kukabiliana na ukataji miti na kuhakikisha kunarejeshwa uoto wa asili.
Makala anaeleza, kama Serikali inavyoagiza, Halmashauri inashirikiana na wakala wa misitu TFS kutoa elimu ya kufuata sheria na kufanya doria za mara kwa mara.
“Tunashukuru kwa jitihada tunaendelea nazo kwani wapo waliokuwa wakataji miti na kutengeneza mkaa lakini Sasa wameacha na wameamua kuingia kwenye kilimo na kufanya shughuli nyingine za kijamii,”anasema Makala.
Makala anaeleza ipo mikakati inayofanyika ikiwemo kupanda miti maeneo yaliyoathirika zaidi, kufanya doria maeneo yanayokatwa ili yawe salama.
Anasema, eneo jingine ambalo wanahimiza ni matumizi ya nishati safi ambapo wanahamasisha akinamama lishe, vijana wajasiriamali wa chips, wauza samaki kutumia gesi badala ya kuni na mkaa.
“Mikakati hiyo inaenda pamoja na Taasisi za Umma kuanza matumizi ya nishati safi, ambapo kwa sisi ni miongoni mwa Halmashauri ambayo tumeanza na Shule ya Sekondari ya wasichana Ruvu ambayo inatumia nishati safi kwa ajili ya jiko la shule, ikiwa ni kutii agizo la Serikali la kuzitaka Taasisi zote za Umma na Binafsi Tanzania Bara zinazoandaa chakula na kulisha watu zaidi ya 100 kwa siku kusitisha matumizi ya kuni na mkaa ifikapo Januari 31, 2024″anaeleza Makala.
MWONGOZO WA UVUNAJI ENDELEVU MAZAO YA MISITU
Kasi kubwa ya uvunaji wa miti kwa ajili ya magogo, mbao, nguzo na mkaa nchini, inaashiria uharibifu mkubwa wa mazingira na kupungua thamani kwa rasilimali ya misitu, hivyo kupoteza faida zitokanazo na kuwepo kwa rasilimali hiyo.
Takwimu zinaonyesha kuwa ongezeko la ujazo wa miti kwa mwaka katika misitu ni meta za ujazo milioni 84, ambazo ndizo zinazoruhusiwa kuvunwa kutoka misitu ya uzalishaji.
Matumizi ya miti katika mwaka 2013 yalikadiriwa kufikia meta za ujazo milioni 103.5, hivyo kuwa na upungufu wa meta za ujazo milioni 19.5.
Upungufu huu wa mahitaji au uvunaji wa ziadi ya kinachoruhusiwa kuvunwa kwa mwaka ni kichochezi cha uharibifu katika misitu iliyohifadhiwa.
Kutokana na changamoto mbalimbali ambazo zilijitokeza kwenye shughuli za uvunaji na biashara ya mazao ya misitu, Wizara ya Maliasili na Utalii ilidhibiti uvunaji wa baadhi ya miti au baadhi ya mazao ya misitu katika vipindi tofauti kwenye miaka kati ya 1995 na 2000 kwa lengo la kutathmini rasilimali iliyopo.
Vile vile kutokana na tathmini hizo, Mwongozo wa Uvunaji endelevu na Biashara ya Mazao ya Misitu wa kwanza uliandaliwa mwaka 2007.
Wananchi na wadau kwa jumla wanatakiwa kutoa ushirikiano wa dhati ili kufanikisha utekelezaji wa mwongozo huu ambao umetolewa kwa madhumuni ya kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali zetu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
MKOA WA PWANI
Mkoa wa Pwani ni miongoni mwa mikoa minne ambayo imeathirika kwa kiasi kikubwa na uharibifu wa mazingira lakini baada ya kupata maelekezo kutoka kwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan ya kutaka mikoa iweke mipango ya kukabiliana na hali hiyo, mkoa huo umejiongeza kwa kuwa na kampeni hiyo.
Mkoa huo kwa kushirikiana na Taifa Gas na Taasisi ya kifedha NMB umekuja na mkakati kabambe wa kuanza kampeni ya upandaji miti ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira.
Kampeni hiyo itasaidia kutunza mazingira na kutangaza teknolojia mbadala ya matumizi ya nishati mbadala baada ya kupunguza matumizi ya miti kama nishati kwa ajili ya kupikia na matumizi mengine ya binadamu ya kila siku.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Alhaj Abubakar Kunenge, anaeleza kuwa mkoa umeweka mikakati mbalimbali ili kutunza mazingira ikiwa ni pamoja na kupanda miti million 13.5 lakini hadi sasa wameshapanda miti milioni 9.7 ikiwa ni zaidi ya asilimia 70 ya malengo ili kurejesha uoto wa asili.
Kunenge anaeleza, kati ya mikakati hiyo wanadhibiti matumizi ya mkaa ambao asilimia 70 ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wanatumia mkaa kutoka Pwani ambapo vijana wengi wamejiajiri kupitia biashara ya mkaa na mazao ya miti.
Anaeleza kwasasa, mkakati mkubwa ni kupunguza vibali kwa asilimia 50 ya matumizi ya miti ili kupunguza ukataji miti kiholela.
Kunenge anafafanua, mikakati mingine ni usimamizi wa mazingira, upandaji wa miti, matumizi ya nishati mbadala na uchumi mbadala ambapo matumizi ya gesi yanapunguza asilimia 40 ya gharama ya fedha ikilinganishwa na mkaa na kutoa ajira kwa vijana 5,000 viwandani .
Kuhusu udhibiti ukataji miti na kuchoma mkaa ovyo Kunenge anaeleza kuwa mkoa umeazimia kudhibiti vyombo vya usafiri (pikipiki) vinavyobeba mkaa kwa kuvisajili na kuvifuatilia kujua wanakotoa mkaa .
“Tumejipanga kuja na mpango wa kudhibiti uvunaji wa mkaa kwa kupunguza utoaji vibali vya mkaa na hili litahamasisha matumizi ya nishati Safi ya gesi,” anasisitiza Kunenge.
Mkuu huyo wa mkoa anaagiza, wavunaji holela wa mazao ya misitu, ambao wanavuna bila kufuata sheria kwenye hifadhi za misitu na vyanzo vya maji waondoke katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Kunenge anakemea, wafanyabiashara wa mkaa, wanaokata miti, kuni na fito, muenendo huu haukubariki hata kidogo.
“Kuna uvunaji holela na misitu kwenye maeneo ya vijiji, vyanzo maji, misitu ya hifadhi kinyume cha sheria, kwasababu tunafahamu misitu hii ni maliasili ya Taifa na inavunwa na kutunzwa kisheria”
Kufuatia kampeni hiyo, dkt.Seleman Jafo anaupongeza mkoa wa Pwani pamoja na wadau mbalimbali wakiwemo Taifa Gas na NMB, kwa jicho lao la tatu kukabiliana na changamoto ya ukataji miti hovyo na matumizi ya mkaa.
MWENGE UNAVYOANGAZA NISHATI SAFI
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa( 2023), Abdallah Shaib Kaim yeye anahimiza wananchi kuongeza matumizi ya Nishati Mbadala (gesi), badala ya kutumia mkaa na kuni ambao huchochea ongezeko la ukataji miti kiholela.
Anaitaka Jamii, kushirikiana na Serikali kupambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Shaib anazisisitiza, Sekretariet za Mikoa na Halmashauri za wilaya, kusimamia sheria, kanuni na miongozo inayotolewa na Serikali kuhusu Uhifadhi wa Mazingira, Misitu na Raslimali zake, vyanzo vya maji na maeneo tengefu.
Anaelezea, kwa zaidi ya asilimia 95 matendo ya shughuli za kijamii yanapelekea kuharibu mazingira hali ambayo inaenda kuharibu ikolojia ya viumbe hai na uchumi wa Taifa.
“Ukataji wa miti usiozingatia utunzaji wa mazingira, hupelekea upotevu wa bioanuai ikiwemo wanyama na mimea, ardhi kupoteza rutuba kupungua kwa pato la Taifa linalotokana na utalii, kupungua kwa kipato cha kaya zinazotegemea raslimali za misitu kupungua kwa raslimali zitokanazo na misitu na kuongezeka kwa athari za mabadiliko ya tabia nchi,” anabainisha Shaib.
JIOGRAFIA YA NCHI
Tanzania ina eneo la kilomita za mraba 94,500 sawa na hekta milioni 94.5. Kati ya hizo, takriban hekta milioni 481 ni misitu na misitu matajiwazi.
Kati ya hekta milioni 48., hekta milioni 28.0 ni hifadhi ya maji, ardhi na bioanuai wakati hekta milioni 20 zilizobaki ni misitu na matajiwazi ambayo uvunaji unaruhusiwa kisheria.
Misitu hii inajumuisha misitu iliyohifadhiwa kwa ajili ya uvunaji na iliyopo kwenye maeneo ambayo hayajahifadhiwa kisheria.
Rasilimali ya misitu ina umuhimu mkubwa katika suala la uhifadhi wa mazingira na inakadiriwa kuchangia asilimia 2 hadi 3 kwenye pato la Taifa.
Pamoja na umuhimu wake katika kuchangia pato la taifa na uhifadhi wa mazingira, baadhi ya misitu iliyohifadhiwa na isiyohifadhiwa inaendelea kuvamiwa kwa ajili uvunaji holela wa mazao mbalimbali, usiojali hifadhi ya mazingira na uchomaji moto.
More Stories
Boost ilivyoboresha miundombinu ya elimu Ilemela
Samia apongeza walimu 5,000 kupatiwa mitungi ya gesi, majiko kutoka Oryx
Uwekezaji kwenye kilimo utatimiza ndoto ya Samia ya nchi kuwa ghala la chakula Afrika