November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bilioni 1.29 kutekeleza miradi ya Tafiti

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online

SERIKALI kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imetoa bilioni 1.29 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi saba ya kitafiti kutoka katika taasisi mbalimbali hapa nchini.
 
Akizungumza wakati wa kuhitimisha mafunzo na utoaji ufadhili huo kwa watafiti wanufaika wa miradi hiyo Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema fedha hizo zinatokana na bajeti kuu ya serikali pamoja na michango ya washirika wa maendeleo ikiwemo Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Utafiti la Canada (IDRC) na Shirika la Maendeleo la Taifa la Norway (NORAD).


 
Amesema serikali imeendelea kuongeza rasilimali fedha, kuweka mazingira rafiki na wezeshi ili kuvutia wadau wengine ndani na nje ya nchi kuwekeza katika shughuli za utafiti na ubunifu nchini.
 
“Mazingira rafiki yamewezesha Serikali katika kipindi cha miaka mitano (2019-2022), kugharamia jumla ya miradi 49 ya utafiti, iliyojumuisha zaidi ya watafiti 235 kutoka Taasisi za Elimu ya Juu na zile za Utafiti na Maendeleo nchini,” amesema Prof. Nombo.


Ameongeza kuwa taasisi 11 za elimu ya juu na utafiti zimewezeshwa kukarabati na kununua vifaa vya maabara za utafiti na miundombinu mingine katika kipindi husika kiasi cha bilioni 9.04 kimetumika katika kutekeleza matokeo hayo.
 
Akizungumzia matokeo ya utafiti utakaofanyika kupitia ufadhili uliotolewa Prof. Nombo amesema inatarajiwa kuimarisha ufaulu katika somo la hisabati kwa shule za msingi na sekondari na kuongeza matumizi ya teknolojia zinazoibukia  hususani matumizi ya akili bandia katika kuchagiza maendeleo ya sekta za kilimo,uvuvi, afya,elimu na manunuzi serikalini.


“Nimefarijika kuona tafiti zimejikita katika maeneo muhimu ya jamii na yanashirikisha sekta husika, kipekee niwapongeze TAKUKURU ambao mmeshirikiana na vyuo kuingia katika ushindani na kushinda kupata ufadhili,nasisitiza watafiti kuhusisha wadau wa sekta husika na tafiti mnazofanya na kuzingatia vipaumbele vya tafiti kitaifa( National Reserch Agenda)”, amesema Nombo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Costech, Dkt. Amos Nungu amesema kupitia ushirikiano uliopo COSTECH imefanikiwa kuleta fedha za utafiti nchini hapa zenye thamani takribani bilioni 9 kwa kipindi cha miaka minne.


Ametaja  baadhi ya maeneo yaliyonufaika na fedha hizo ni pamoja na uanzishwaji wa vigoda viwili vya utafiti katika chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Afrika ya Nelson Mandela (NM-AIST) Arusha na Tathmini ya madhara ya COVID19 kupitia MUHAS, UDOM.


 
“Nitoe wito kwa taasisi za utafiti na vyuo vikuu kuleta Tungo zao (proposals) kwenye eneo la usalama wa chakula. Mwisho wa kuwasilisha ni tarehe 10.09.2023 na kiasi cha fedha za kitanzania shilingi milion 650 zitatumika kufadhili miradi ya utafiti itakayoshinda,”amesema Dkt. Nungu