Na Lubango Mleka, TimesMajiraOnline Igunga.
Wafanyabiashara wa soko la kati wilayani Igunga mkoani Tabora wamemlalamikia msimamizi anayekusanya ushuru wa vyoo vya soko hilo Madete Sinas kwa kuvifunga vyoo hivyo kwa siku nne na kusababisha wao kupata usumbufu mkubwa hali ambayo imechangia kushindwa kufanya shughuli zao za biashara.
Wakizungumza katika soko hilo, Lucia Samson, amesema kitendo kilichofanywa na msimamizi huyo kimewasikitisha sana kwani kukosekana kwa huduma hiyo kumechangia pia wao kuathirika ikiwa pamoja na Halmashauri kukosa mapato.
“Mimi nimuombe Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga kuchukua hatua kali dhidi ya msimamizi huyo pamoja na wahasibu wa Halmashauri ambao wameshindwa kufuatilia tatizo hili ikiwa ni pamoja na kutokuhakiki mapato kwani hapa hatupatiwi risiti tunapo pata huduma ya choo, kwani huwa tunalipa shilingi 300,”amesema Magdalena Andrea,
Huku, Bakari Kimwaga amesema kuwa vyoo hivyo siyo visafi na vinatoa harufu mbaya, hali ambayo inaweza kusababisha mlipuko wa magonjwa hapa sokoni.
Msimamizi wa vyoo hivyo vya soko la Kati mjini Igunga Madete Sinas alipoulizwa na mwandishi wa habari hizi juu ya kuvifunga vyoo amesema kuwa “naomba usiniulize mimi wewe waambie hao wafanyabiashara waandamane wakawaulize Halmashauri,”.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Kati ambapo lipo soko hilo Mhoja Masanja amesema yeye alipigiwa simu siku ya Jumapili akijulishwa na wafanyabiashara kuwa vyoo vimefungwa na mhusika hayupo.
Amesema alikwenda mpaka eneo la soko hilo na kukuta milango ya vyoo ikiwa imefungwa makufuli na kuongeza kuwa hali hiyo ilimsikitisha sana kwa kuwa wafanyabiashara hao wamekuwa wakilipa ushuru pasipo kuwa na shida yoyote.
“kwa kweli mambo kama haya ya kufunga vyoo hayajinipendeza kwani Serikali imekuwa ikisisitiza kutokuwafungia wananchi wake kufanya biashara lakini wao huwafungia wanapochelewa kulipa kodi sasa kama wafanyabiashara wanalipa ushuru iweje wafungiwe vyoo sio jambo la hekima wala busara kuwafanyia hivi wafanyabiashara hawa,” amesema Muhoja.
Naye Katibu wa soko hilo Marco Gideon amesema yeye alikwenda kujiisaidia katika vyoo hivyo lakini alikuta milango imefungwa na makufuli yapo na kuongeza kuwa kufungwa kwa vyoo hivyo kumeathiri wafanyabiashara kwani soko hilo linahudumia wananchi zaidi ya 3000 kwa siku.
Hata hivyo amebainisha kuwa usimamizi wa mtu huyo aliyewekwa ni mbovu na amekuwa hatoi risiti licha ya wafanyabiashara kulipa sh 300, pia amekuwa hafanyi usafi wa vyoo na kusababisha kuwa vichafu.
Sambamba na hayo amemuomba Mkurugenzi kuongeza matundu ya vyoo kwani yaliyopo ni machache ambapo upande wa wanawake kuna milango miwili na wanaume milango miwili hali ambayo imekuwa ikileta usumbufu mkubwa wa kupanga foleni wanapokwenda kupata huduma.
Hata hivyo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga Joseph Sambo amethibitisha kufungwa kwa vyoo hivyo.
“ni kweli mimi nimefika hapa soko na kukuta milango ya vyoo ikiwa imefungwa na nimetoa maelekezo vyoo vyote vifunguliwe na kuanza kufanya kazi,” amesema Sambo.
Amesema msimamizi aliyekuwepo Madete Sinas amejiondoa mwenyewe na tayari wameweka mtu mwingine ambaye ni Mashaka Lutonja na amemtaka kufanya kazi kwa umakini kwa kutoa risiti huku akimtaka pia kutoa taarifa pindi anapokumbana na changamoto yoyote.
More Stories
Kamati ya Mfuko wa Jimbo Musoma Vijijini yagawa vifaa vya ujenzi
Hatma mrithi wa Kinana kupatikana
Mrithi wa Kinana CCM kujulikana katika Mkutano Mkuu wa Jan 18/19