November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mha.Mahundi:Rais Samia ameupendelea Mkoa wa Mbeya sekta ya Afya

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

NAIBU Waziri wa Maji Mhandisi , Maryprisca Mahundi amesema kuwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ameupendelea mkoa wa Mbeya kwa kuwekeza miundombinu ya majengo ya kisasa katika sekta ya afya hususani vifaa tiba vya kutosha.

Imautaja uwekezaji huo umesaidia jamii kutolazimika kusafiri na kutotumia gharama kubwa ya kutafuta matibabu Jijini Dar es Salaam kutokana na huduma zote muhimu kupatikana Jijini Mbeya.

“Zamani ilikuwa lazima upande basi kuzifuata huduma za matibabu ambazo ni muhimu lakini kwa sasa huduma hizo zinapatikana kirahisi hapa hapa mkoanibeya,”amesema.

Mha.Mahundi amesema hayo wakati wa ufunguzi kambi ya matibabu ya upasuaji mtoto jicho katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mbeya ambapo kambi hiyo itadumu kwa siku saba.

Aidha Mha.Mahundi amesema kwamba baada ya kuona mwitikio mkubwa wa tatizo la fistula alipata simu nyingi hivyo akaona ni bora familia zote zije kupata matibabu kwa pamoja na kupata wazo la matibabu ya macho.

“Kwasababu tulimkomboa mwanamke wanasema ukimkomboa mwanamke umekimbia familia,maana tulichukulia lile tatizo linalotukumba sisi akina mama la misamba, fistula,kutokwa hewa chafu bila kujiandaa mwenyewe kwa hiyari yako mwisho wa siku akina mama na akina baba wakaomba kama kuna lingine tunaomba utufikie,”amesema.

Ameeleza zaidi kuwa huduma hiyo ya bure ya macho mpaka Agosti 21,kuna watu 30 wamehudumiwa na watu 8 walikutwa na shida ya macho na tayari watu wanne wameshafanyiwa upasuaji wa mtoto jicho.

Hata hivyo amewataka wananchi mkoani Mbeya kuwaombea madaktari bingwa kutoka nchini Ujerumani ambao wamesafiri umbali mrefu pamoja na madaktari wenyeji wa mkoa wa mbeya ambao ndo wenyeji wa madaktari bingwa kutoka Ujerumani.

“Unapokuwa kiongozi hupaswi kuwa wewe ndiyo bosi uongozi ni uwajibikaji unapokuwa kiongozi wewe ni mtumwa,hutakiwi kukaa kwenye kiti mara unazunguka,mara umekunywa bia,aaa huo sio uongozi,tunapoomba kuwa wawakilishi wenu maana yake tunapaswa kusimama mstari wa mbele katafute fursa kawaletee wenzio kwasababu unapokuwa mwakilishi maana yake lile kundi kubwa linakuangalia wewe”amesema Mha.Mahundi.

Akizungumza katika ufunguzi huo Mganga mfawidhi wa hospitali Rufaa ya mkoa wa Mbeya,Dkt.Abdallah Mbaga amesema kambi hiyo watakuwa na madaktari bingwa kutoka nchini Ujerumani na watakuwa hospitalini hapo kwa siku Saba mpaka Agosti 29 mwaka huu .

Amesema kuwa matibabu hayo kwa gharama kawaida ni dola 95 na kwa fedha kitanzania ni Shilingi 218,000 kwa mgonjwa mmoja.