Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online DSM
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hashim Komba, amempongeza Mkurugenzi wa shule za St Anne Marie, Dk. Jasson Rweikiza kwa uwekezaji mkubwa alioufanya kwenye elimu na kutengeneza nafasi za ajira.
Ametoa pongezi hizo mwishoni mwa wiki shuleni hapo wakati wa mahafali ya 19 ya kidato cha nne yaliyofanyika shuleni hapo Mbezi Kimara kwa Msuguri jijini Dar es Salaam.
Amesema Dk. Rweikiza ameisaidia Serikali kwa kiasi kikubwa kuwasaidia watanzania kupata elimu bora tena ya gharama nafuu.
Amesema uwekezaji huo umesaidia kuongeza ajira kwa watanzania na kuwapongeza wazazi/walezi wa wanafunzi wa kidato channe kwa kutimiza wajibu wao wa kuwalipia ada ili wapate elimu bora katika shule hiyo.
Ameupongeza uongozi wa shule kwa usimamizi mzuri wa shule nakwamba hali hiyo imesababisha ifanye vizuri sana kitaaluma kwa kupata matokeo mazuri katika mitihani ya kitaifa.
Amewapongeza pia kwa kuhakikisha huduma zote muhimu kwa wanafunzi zinapatikana na kujitosheleza kama vile maji ya kutosha kwa ajili ya kupikia, kufua, kumwagilia mashamba, bustani za maua na mboga, maji safi na salama ya kunywa, Uwepo wa magari ya kusambaza maji wakati wa dharura ya maji ya DAWASA yanapokatika.
Amesema amefurahi kusikia shule ina mradi wa ufugaji wa ng’ombe na kuku kwa ajili ya nyama na mayai ya wanafunzi.
“Wakati naingia hapa shuleni leo, nimeshuhudia magari mengi sana ya shule, hii ni dhahiri kwamba shule ina magari ya kutosha kwa ajili ya usafiri wa wanafunzi wa kutwa na shughuli nyingine za shule,” amesema.
“Pia nimeshuhudia maabara tano kubwa zenye vifaa vya sayansi kwa vitendo, maktaba mbili kubwa zilizosheheni vitabu vya kila aina na mazingira mazuri ya wanafunzi kujisomea,” amesema
Amesema hiyo ni mara yake ya kwanza kuona maktaba ya shule ya msingi yenye viyoyozi huku akishauri ada iwe himilivu.
“Mheshimiwa Dk. Jasson Rweikiza, Mwenyekiti na Mkurugenzi wa shule hizi ili wazazi wapate fursa ya kuwaleta watoto wao wapate elimu bora hapa, nashauri ada ya shule iwe himilivu isiwe kubwa ya kuwashinda watanzania wenye vipato vya kati,” amesema .
Aidha, amesema ada ikiwa himilivu itatoa fursa kwa watanzania wengi kumudu kuwalipia ada watoto wao na hivyo watakuja kusoma hapo ili wapate elimu bora inayotolewa shuleni hapo.
“Shule hii imezungukwa na jamii, shule itoe misaada/ishiriki kwenye maendeleo ya jamii kama vile barabara, zahanati, shule, miundombinu ya maji, ulinzi, usafiri . Hii itasaidia kudumisha uhusiano chanya kati ya shule na jamii,” amesema.
Amewapongeza Maafisa wote wa Elimu wa wilaya ya Ubungo na wasaidizi wao kwa kusimamia vizuri sana elimu ndani ya Wilaya hiyo ya Ubungo.
Amesema usimamizi mzuri wa viongozi hao unachangia sana shule hiyo kuendelea kufanya vizuri kitaaluma.
Amesema serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inatambua mchango mkubwa wa shule ya St. Anne Marie Academy pamoja na shule nyingine za binafsi na kwamba itaendelea kuweka mazingira rafiki ili kupata shule nyingi ziweze kuwekeza kwenye elimu na kutoa huduma zilizotukuka kama za St. Anne
Amesema mafanikio hayo makubwa ya shule yametokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya wafanyakazi wa shule, kujituma, kufanya kazi kwa bidii na uwekezaji mkubwa uliofanywa na uongozi wa shule.
“Naomba msirudi nyuma endeleeni kufanya kazi zenu kwa bidii ili shule hii iendelee kupaa siku hadi siku,” amesema .
Amezitaka shule kuweka mifumo imara ya ulinzi ya namna ya kupambana na majanga ya moto kama kuweka vifaa vya kisasa vya kuzimia moto kama vya St Anne Marie.
Amesema ametembelea shule hiyo na kujionea uzio eneo lote la shule na askari wa kutosha wenye mafunzo na uwezo wa kutumia silaha za moto, wakiwemo mbwa wakali kwa ajili ya ulinzi wa shule.
“Usalama wa watoto inatakiwa kuwa kipaumbele cha kwanza kwa hiyo ni vyema shule zingine nazo zikaiga mfano huu kwa kweli mmejidhatiti na hata likitokea lolote mnaweza kukabiliana nalo,” amesema
Amempongeza Mkurugenzi wa shule hizo, Dk. Jasson Rweikiza kwa uwekezaji alioufanya kwamba ameisaidia Serikali kwa kiasi kikubwa kuwapa watanzania elimu bora tena ya gharama nafuu.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa