November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakazi Ulyankulu waaswa kuhifadhi mazingira

Na Allan Vicent, Timesmajira Online, Kaliua

WAKAZI wa Kata za Ilege na Kona Nne katika Tarafa ya Kashishi Jimbo la Ulyankulu wilayani Kaliua mkoani Tabora wametakiwa kuhifadhi vizuri mazingira wanayoishi ili kulinda uoto wa asili.

Wito huo umetolewa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Halima Mamuya alipokuwa akizungumza na wakazi wa kata hizo katika ziara yake ya siku moja wilayani humo.

Amesema vitendo vya uharibifu wa mazingira ni adui mkubwa wa maendeleo ya wananchi hivyo amewasisitiza wakazi wa kata hizo kupanda miti ya kutosha katika maeneo yao ili kulinda na kuboresha mazingira yanayowazunguka.

Alibainisha kuwa ukataji miti ovyo husababisha jangqa n ukosefu wa mvua katika maeneo mengi ikiwemo kusababisha jangwa.

Mamuya aliwataka wakazi wa kata hizo kuboresha mazingira ya shule zao mpya za sekondari zinazoendelea kujengwa kwa kupanda miti ili kuepusha upepo kuezua mapaa ya vyumba vya madarasa na nyumba za walimu zinazoendelea kujengwa kwa mabilioni ya fedha.

Alisisitiza kuwa serikali ya awamu ya sita inawajali sana wananchi wake wakiwemo wakazi wa kata hizo hivyo akawaomba kutunza vizuri miradi yote inayotekelezwa na serikali ili kuwanufaisha zaidi..

Aidha aliwataka kuunga mkono juhudi za maendeleo zinazoendelea kufanywa na serikali kupitia halmashauri hiyo huku akiwakumbusha madiwani na watendaji wa vijiji na kata kujenga utamaduni wa kutembelea wananchi.

Sanjari na hayo Mamuya alipongeza kazi nzuri inayofanywa na Mwenyekiti wa halmashauri hiyo ikiwemo kuwezesha vikundi vya wanawake wa CCM.

Naye Diwani wa Kata ya Ilege ambaye ndiye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Japhael Lufungija alipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kuwaletea zaidi ya bilioni 12 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kimkakati katika sekta ya elimu, afya, maji na miundombinu ya barabara.

Aliwahakikishia kuwa serikali ya Rais Samia imedhamiria kumaliza kero zote zinazokabili wananchi katika sekta zote.