November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

UWT yawataka wananchi Igunga kupuuza wapotoshaji mkataba wa bandari

Na Lubango Mleka, Timesmajira Online,Igunga.

UMOJA wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi Taifa (UWT) umewataka Wananchi wa Jimbo la Igunga mkoani Tabora kuwapuuza viongozi wa vyama vya upinzani na watu wote ambao wanapotosha ukweli juu ya mkataba wa uendeshaji wa bandari ya Dar-es-Salaam kati ya Tanzania na kampuni ya DP World ya nchini Dubai.

Hayo yamesemwa na Makamu Mwenyekiti UWT Taifa,MNEC Zainab Shomari katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya kumbukumbu ya Sokoine Mjini Igunga baada ya kumaliza ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo katika Kata za Bukoko, Nguvumoja, Lugubu, Mwamakona, Mwamashiga, Nanga na Igunga zilizopo jimbo humo ambapo ameridhishwa na ujenzi wa miradi hiyo.

“Wanaigunga kuna watu wameibuka wanapita sehemu mbalimbali za nchi wakipotosha nia njema ya Serikali yetu kuuingia ubia wa maendeleo ya uboreshaji usimamizi na uendeshaji wa bandari yetu ya Dar-es-Salaam na miundombinu yake, ninawaomba muwapuuze kwani ni waongo Serikali haijauza bandari yetu bali imeingia makubaliano ya kushirikiana kuendeleza na kuiboresha na si vinginevyo,” amesema Shomari na kuongeza kuwa

“Walikuwa wanapiga kelele kuwa hapa hakuna hospitali,zahanati,vituo vya afya , sasa hivi kuna vituo vya afya na zahanati nchi nzima na bahati nzuri kuna mitambo ya Ultrasound zamani ulikuwa hauzipati mpaka hospitali ya Mkoa,vyumba vya kujifungulia vipo, vya upasuaji vipo leo katika ziara yangu nimejionea mafanikio yote haya katika Jimbo la Igunga na Manonga,”.

MNEC Shomari, amebainisha kuwa wapinzani wameishiwa hoja hivyo wameona kwa sasa kukimbilia katika hoja ya bandari kwa kupotosha wananchi kwani bandari ipo salama na Rais Samia ni mwaminifu na ameisha fanya miradi mingi mikubwa ndani ya kipindi cha miaka miwili hivyo waendelee kuiamini CCM.

Katika hatua nyingine MNEC Shomari amewaasa wananchi kupinga vitendo vyote vilivyo kinyume na maadili ya kitanzani na kidini ikiwemo vya mapenzi ya jinsia moja, ukatili wa kijinsia kwa kuwakemea watu wote ambao watawabaini kujihusisha au kufadhili vitendo hivyo.

“Hivi karibuni limeibuka wimbi la vijana wetu kujihusisha na masuala ya ndoa za jinsia moja tena cha kusikitisha kiongozi mmoja wa upinzani alikimbia nchi yetu sasa yeye ndiye amekuwa kinara wa kuunga mkono vitendo hivi, wakina mama na kina baba hatuwalei watoto wetu kama tulivyolelewa sisi na wazee wetu, tuwafundishe makuzi mazuri kwa kuwapatia elimu bora ya malezi,” amesema Shomari.

Aidha, amewataka wanawake, vijana na walemavu kuzitumia vyema fedha ambazo wanapatiwa za asilimia 10 kutoka katika Halmashauri kwani zitawasaidia kujiinua kiuchumi.

Akifafanua kuhusu mkopo wa asilimia 10 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga Athumani Msabila amesema kuwa halmashauri hiyo ina jumla ya milioni 128 ambazo wanasubiri tu maelekezo kutoka Serikalini juu ya kuanza kuwapatia walengwa huku akivitaka vikundi ambavyo vinasuasaua kurejesha mikopo hiyo kurejesha kama wanavyotakiwa.