Na Esther Macha, Timesmajira Online,Mbarali
WANANCHI wilayani Mbarali mkoani Mbeya wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia huduma ya matibabu ya macho bila malipo ambayo imekuwa mkombozi kwa watu waliokosa matumaini ya kupona kabisa kutokana na kukata tamaa.
Hayo yamebainishwa leo na mmoja wa wagonjwa ambaye amefanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho, Sabina Sent (65) kupitia kambi ya siku saba ya Madaktari Bingwa wa upasuaji wa macho wilayani humo chini ya ufadhili wa Shirika la Kimataifa la Helen Killer.
Sabina amesema alifika hospitali hapo akiwa haoni lakini baada ya kufanyiwa upasuaji ameweza kwani kwa muda wa miaka miwili lakini baada ya kufika katika Hospitali ya Wilaya ya Mbarali na kufanyiwa uchunguzi kisha upasuaji anarudi kwake akiwa na tabasamu la kuona.
“Namshukuru Rais Samia kwa kutupatia matibabu ya macho bila malipo, nimekuja nikiwa sioni lakini sasa naweza kuona vizuri macho yangu yote”, amesema Sabina.
Kwa upande wake Mzee Richard Enock (59) amesema ameishi na tatizo la kutokuona kwa miaka 18 lakini leo baada ya kufanyiwa upasuaji na madaktari bingwa wa macho bila malipo anaweza kuona vizuri.
Mzee Enock ameeleza kuwa tatizo la kutokuona lilimuanza toka mwaka 2005 ambapo lilianza jicho moja na kila siku nguvu ya kuona ikawa inapungua mpaka macho yote yakawa hayaoni tena.
“Namshukuru sana Rais kwa juhudi zake za kutujali sisi wananchi kwa kutusogezea huduma za macho karibu sikuwa na uwezo wa kusafiri kufuata huduma hizi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya”, amesema Mzee Enock
Naye Mtoto wa mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho, Nassoro Atupele amesema kuwa amefarijika sana kuona baba yake anaona kwani amekuwa haoni tangu mwaka 2014 alipopata tatizo la mtoto wa jicho na kuacha kuona kabisa.
“Nitoe wito na shukrani zangu za dhati kwa serikali yetu naomba huduma hizi ziwe endelevu kwani sio kila Mtanzania ataweza kusafiri kufika Hospitali zinazotoa huduma hizi za upasuaji kama zilivyotufata hapa Mbarali”, amesisitiza Atupele
Aidha, kambi hiyo ya Madaktari Bingwa wa Macho mpaka sasa imefanya upasuaji wa mtoto wa jicho kwa watu 150 na ilianza Jumatatu ya Agosti 14 na inatarajia kumalizika Agosti 20 mwaka huu.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa