November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ATCL kuongeza safari Octoba

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Shirika la ndege Tanzania (ATCL) wanatarajia kuongeza idadi ya safari kutoka safari 4 hadi kufikia 5 kwa wiki ifikapo mwezi Octoba mwaka huu ili kukabiliana na ongezeko la abiria.

Mwaka 2019, Air Tanzania iliongeza mtandao wake wa safari kwa kuingia kwenye soko la Mumbai, India na walianza na safari moja kwa wiki kwa
kutumia ndege hizo za abiria kulihudumia soko hilo na sasa wanasafari nne (4)
kwa wiki.

Aidha Shirika hilo limesema kwa sasa litaendelea kutumia ndege zao kubwa mpya za kisasa Boeing 787- 8
Dreamliner ili kuendelea kukidhi matarajio yao.

Hayo aliyasema Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL Mhandisi Ladslaus Matindi wakati akizungumza na waandishi wa Habari Jana Jijini Dar es Salaam, kuhusu ziara ya kikazi aliyoifanya jijini Mumbai , China ambapo alifanikiwa kukutana na wadau mbalimbali wakiwemo Makampuni makubwa ya uzalishaji na usambazaji wa Madawa, Makampuni makubwa ya uuzaji wa tiketi , Makampuni makubwa ya Ndege
na Uongozi wa hospitali mbili (2) kubwa jijini Mumbai

Mhandisi Matindi alisema Kwa kutumia ndege zao za abiria walifanikiwa kumiliki asilimia 80 ya abiria wote wanaosafiri kati ya Tanzania na Mumbai sawa na wastani wa abiria Zaidi
ya elfu 66 kwa mwaka.

“Licha ya ukweli kwamba idadi hii ni ndogo sana ukilinganisha na abiria wote
wanaosafiri nje ya nchi hiyo kila mwaka hususan watalii, tulifanikiwa kumiliki
asilimia 80 ya abiria wote wanaosafiri kati ya Tanzania na Mumbai kutokana na
Ubora wa huduma, aina ya ndege Boeing 787- 8 Dreamliner (ndege za kisasa, zenye utulivu angani, nafasi kubwa na uwezo wa kuwafanya wasafiri wajisikie fahari
na maalum), Uwezo wa Kampuni katika kumudu soko naAbiria wanaosafiri na ndege zetu wameendelea kufurahia huduma ya mtandao “Wifi” angani, vyakula vya asili kwa wasafiri pamoja na
viburudisho.”

Kwa upande wa Ndege mpya ya kisasa ya mizigo Boeing 767- 300F kutoka shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Mhandisi Matindi alisema tayari imeanza safari zake na imeendelea kusafirisha mizigo ya aina mbalimbali ikiwemo Bidhaa zinazoharibika kwa muda mfupi, Bidhaa za kawaida na Bidhaa zenye uhitaji wa udhibiti wa hali ya hewa ya kiwango maalum kama vile madawa.

Mhandisi Matindi alisema Uwepo wa ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba tani 54 kwa mara moja imewezesha Kampuni ya Glenmark Pharmaceutical, mojawapo ya makampuni makubwa ya utengenezaji wa madawa ya binadamu nchini India, kukubali kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usambazaji wa madawa ya Kampuni hiyo barani Afrika kwa kutumia ndege zetu.

Aidha alisema hadi sasa kampuni kubwa zimekubali kuingia nao makubaliano lengo ikiwa ni kuendelea kuboresha utoaji wa huduma.

“MakeMyTrip inayohusika na uuzaji wa tiketi za ndege na uwezeshaji wa
safari za kitalii nchini humo. MakeMyTrip ambayo inatumia tovuti yake kuuza tiketi za Air Tanzania ndani na nje ya India pia imekubali kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania kupitia tovuti hiyo.”

Pia Matindi alisema wamefanikiwa pia kuanzisha mazungumzo ya mashirikiano ya
kibiashara ya kubebeana abiria (Interline Agreement) na Kampuni ya Ndege ya Vistara.

“Kampuni hii ina mtandao mkubwa kwa safari za ndani nchini India hivyo
itarahisisha uunganishaji wa safari za ndani kwa abiria wa ATCL
wanapofika jijini Mumbai.”

Alisema wameanzisha mazungumzo na hospitali mbili (2) zilizopo jijini
Mumbai kwa ajili ya kuingia makubaliano ya kibiashara ambapo makubaliano
hayo yatawezesha wagonjwa wanaotoka Tanzania kupata punguzo la gharama za matibabu wanapotumia ndege zetu.

“Tayari tuna mahusiano ya kibiashara na hospitali ya Kokilaben iliyoko
Mumbai ambapo wasafiri wanaotumia ndege zetu hupata punguzo la
gharama za matibabu wanapotibiwa katika hospitali hiyo.”

Kadhalika Mhandisi Matindi alisema
Katika ziara hiyo alifanikiwa kukutana na Balozi Anisa Mbega,
Balozi wa Tanzania nchini India, na kupongeza kwa juhudi anazozifanya
kutangaza fursa na vivutio vilivyopo Tanzania ikiwemo maonesho nchini India ambapo ATCL wameshiriki kwenye baadhi ya maonesho hayo.

Kuhusu utekelezaji wa Mpango Mkakati wa ATCL, Mhandisi Matindi alisema wameendelea kuboresha utoaji wa huduma, kununua ndege mpya za kisasa na kupanua mtandao wa safari ili kuendana na kasi ya mahitaji halisi ya soko la Anga.

Alisema Kwa sasa wana
ndege mpya Masafa ya mbali tatu (3) – Boeing 787-8 (2) na Boeing 767-300F (1),
Masafa ya kati nne (4) – Airbus 220-300 na Masafa mafupi sita (6) – Q400 (5).