Na Ashura Jumapili, Timesmajira Online, Bukoba
Baraza la Madiwani Halmashauri ya Manispaa Bukoba limekutana kwa dharura na kubadilisha matumizi ya kiasi cha bilioni 1, zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya ujenzi wa stendi mpya ya mabasi itakayojengwa eneo la Kyakailabwa.
Fedha hizo zimebadilishiwa matumizi ili zifanye ukarabati wa stendi ya sasa iliyojengwa wakati wa mkoloni kwa zaidi ya miaka 60 na haijawahi kufanyiwa ukarabati mkubwa.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ukarabati wa stendi kuu ya mabasi Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Hamid Njovu,amesema halmashauri hiyo inamiliki stendi inayotumika kwa sasa iliyopo katikati ya Mji Mtaa wa Uhuru kiwanja chenye hati Na.71712 kiwanja Na.164 kitalu (I )Kata Bilele ina ukubwa wa Mita za mraba (6620 ).
Njovu,amesema stendi hiyo ilijengwa wakati wa mkoloni na ina umri zaidi ya miaka 60 lakini haijawahi kufanyiwa ukarabati mkubwa hali inayoisababishia halmashauri gharama kubwa za usimamizi na maboresho ya mara kwa mara na imekuwa kero kwa watumiaji kwa sababu ya uchakavu wake.
Amesema katika kutataua kero za wananchi Mkuu wa Mkoa huo ,akiwa ameambatana na wajumbe wa sekretarieti ya Mkoa , Mstahiki Meya pamoja na wataalam wa halmashauri ya Manispaa ya Bukoba walitembelea stendi hiyo na kubaini changamoto kubwa.
“Ujumbe wa Mkuu wa Mkoa ulielekeza kwamba badala ya kutumia bilioni 1 kuanza ujenzi wa stendi mpya ya Kyakailabwa ambapo tayari anatafutwa mkandarasi mshauri badala yake itumike kufanya marekebisho makubwa ya stendi inayotumika sasa wakati taratibu za ujenzi wa stendi kubwa unaendelea ambapo ,halmashauri ilielekezwa kufanya tathimini na kutekeleza jambo hilo kwa mujibu wa sheria,”amesema Mkurugenzi.
Amesema tathimini ya awali ya ukarabati na ujenzi wa eneo hilo inaonesha eneo la kuegesha magari makubwa na madogo ni mita za mraba 3637 litakuwa na uwezo wa kuingiza mabasi makubwa (15-20) na madogo (20-30 )kwa wakati mmoja na litakuwa na jengo la abiria la ghorofa moja.
Pia amesema ghorofa ya chini itakuwa na maduka saba ,vyoo vya wanawake vitano,wanaume vitatu ,migahawa, jiko, stoo,vyumba 15 vya kukatia tiketi na sehemu ya abiria kusubiria usafiri au kupumzika.
Huku ghorofa ya juu itakuwa na kituo cha polisi,jengo la utawala na sehemu nyingine za ofisi kwa matumizi ambayo yatapangwa baadae.
Aidha amesema gharama za mradi zinaweza kuzidi bilioni moja zilizotolewa na Rais hivyo aliliomba Baraza la Madiwani kuridhia kubadili vifungu vya miradi ya maendeleo kwa kutumia mapato ya ndani ili ziweze kukamilisha stendi hiyo sanjari na kupeleka ombi maalumu la nyongeza ya gharama hizo kwa Rais Samia ili kukamilisha maboresho ya stendi hiyo ya zamani kwa ufanisi zaidi.
Diwani wa Kata Bilele ilipo stendi hiyo Tawfiq Sharif,amesema wamechelewa sana kutekeleza mradi huo wa ukarabati wa stendi hiyo ambayo imekuwa kero kwa wananchi kwa muda mrefu sasa wafanye kazi.
“Itoshe kusema kazi endelee maana changamoto zilizopo katika stendi hiyo zimekuwa kero kwa muda mrefu kwa wananchi ,leo nimefarijika sana kufikia hatua hii,”amesema Sharif.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Erasto Siima,amewashukuru Madiwani kwa kukubali kubadili matumiz ya fedha hizo kwa lugha moja ili kuboresha stendi iliyopo sasa.
Siima,amesema Wilaya ya Bukoba ilianza mwaka1961 lakini Manispaa ya Bukoba ilianza mwaka 2005 hadi leo hakuna kilichofanyika “sisi tunabishana tu hapa tunazidiwa na Singida na Kigoma zaidi ya miaka 60 stendi haijawahi kufanyiwa marekebisho yoyote,”amesema Siima.
“uchumi wa Bukoba na Mkoa Kagera hauwezi kuulinganisha na Singida mali zote zilizopo hapa tuazidiwa na Mkoa huo ambapo Bukoba hatuna stendi,sisi kama wasimamizi tutaendelea kuyasimamia na yakamilike kwa wakati na stendi hii inajengwa ili kukidhi mahitaji ya sasa ujenzi wa Kyakailabwa tutajipanga vizuri zaidi kwa ujenzi wa stendi ya kimataifa,tumshukuru Mkuu wa Mkoa ana asilimia kubwa katika kutekeleza hilo,”amesema mkuu wa Wilaya.
Naibu Waziri wa Nishati ambaye ni Mbunge wa jimbo la Bukoba Wakili Stephen Byabato,amesema ili wasikwame washirikiane kwani hakuna mlango ambao hauwezi kufunguliwa waombe ushauri waeleze uhalisia wa Bukoba waweze kusonga mbele.
Wakili Byabato,amesema kilichowafanya wapige kona hiyo nzuri ni kwa sababu kumekuwa na uhakika wa utekelezaji wa mradi wa ( TACTIC )”Tanzania Cities Transforming Infrastructure $ Competitiveness”.
Naye Mhandisi Mshauri wa mradi huo kutoka kampuni ya ( SAVANNA ENGINEERS )Aswile Kibona,amesema ukarabati huo umezingatia ubora kwa kujenga sakafu ya zege imara,mitaro ya maji yanayomwagika na mifumo ya maji taka.
Kibona amesema utajengwa uzio wa ukuta kwaajili ya kuona watu wanaoingia ndani ya stendi kupitia mlango unaonekana nakutoka sio kila mtu kuingia kwa njia ambayo anataka yeye wamezingatia mabasi yaweze kuingia kwa urahisi na kutoka.
Anasema pia wameweka mabango kwaajili ya matangazo ambayo watu wanataka kuingia stendi ambayo wataweza kuwaingizia halmashauri mapato.
More Stories
Prof. Mwakalila asisitiza uadilifu, uzalendo kwa wanafunzi wapya chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere
Benki ya Equity Tanzania yasaini mkataba wa kuwawezesha wanawake kiuchumi
Rais Samia alivyoguswa kifo cha msanii Grace Mapunda