November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NMB yatunikiwa cheti cha Superbrand

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

NMB imetunukiwa cheti cha kuwa ‘Superbrand’, na kuifanya kuwa benki pekee iliyopata hadhi hiyo nchini Tanzania kwa mwaka huu.

Hadhi hiyo ya ‘Superbrands’ inatunukiwa chapa bora zaidi katika uwanja wao kufuatia mchakato mkali wa uteuzi na baraza la Superbrands na watumiaji wa bidhaa na huduma kutoka Afrika Mashariki.

Akizungumza wakati wa hafla ya kupokea cheti hicho iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana, Mweka Hazina wa Benki ya NMB, Aziz Chacha amesema hadhi ya Superbrands ina maana kubwa kwa benki hiyo huku akisisitiza kuwa cheti hicho ni chachu ya kuifanya benki hiyo kuwa chaguo kwa wateja wake.

“Hili lisingewezekana bila imani iliyopo kwa wateja wetu ambao wamekuwa bega kwa bega nasi kwa miaka hii yote, tunafurahi kwamba wateja wetu wameweza kuamini chapa yetu na kuifanya kuwa miongoni mwa chapa bora Afrika Mashariki,”amesema.

Amebainisha kuwa benki hiyo imejipanga kuendelea kuongeza thamani kwa wadau wake wote wakiwemo wanahisa, wateja na jamii ambako benki hiyo inafanya kazi.

Pia ametoa shukrani kwa mamlaka zote za udhibiti zikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) kwa kufanya nao kazi kwa karibu ambapo miongozo ya mamlaka hizo imesaidia kujenga misingi imara kwa benki yao.

Awali Mkurugenzi wa Mradi wa Superbrands na Mchapishaji Jawad Jaffer,amesema kufikia hadhi ya Superbrands huimarisha nafasi ya chapa, huongeza heshima na kuwahakikishia watumiaji na wasambazaji kwamba wananunua chapa bora zaidi .

“Hadhi ya Superbrand inazipa faida kubwa kwa wanaoipata, inaongeza heshima kwa kampuni dhidi ya washindani wake na inadhihiririsha kuwa mlaji wa mwisho anapata bidha bora kabisa,”amebainisha.

Jaffer amesema katika awamu ya nane mwaka huu, kampuni yake imetoa hadhi ya Superbrand kwa kampuni nne nyingine mwaka huu zikiwemo GSM, Kilimanjaro Drinking Water, Dar Ceramic na Shirika la Bima la NIC Insurance.

“Kupokea hadhi ya Superbrand ni jambo moja. Kuitunza ni jambo lingine nazikumbusha kampuni zote ambazo zimepokea hadhi hii leo kufanya juu chini ili kuhakikisha kwamba zinaidumisha,”amesisitiza.

Amesema kampuni zote tano zilizopokea hadhi ya Superbrand zitatunukiwa tuzo wakati wa sherehe zilizopangwa kufanyika mwaka kesho.