November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mhandisi Mahundi atoa zaidi ya milioni 200 kuwawezesha wanawake kiuchumi

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya

MBUNGE wa Vitimaalum CCM Mkoa wa Mbeya na Naibu Waziri wa Maji ,Mhandisi Maryprisca Mahundi,ametoa kiasi cha zaidi ya milioni 200 kwa ajili ya kuwawezesha wanawake kutekeleza miradi mbalimbali katika Wilaya zote za Mkoa huo ili kuinika kiuchumi na kutokuwa tegemezi katika familia zao.

Mhandisi Mahundi amebainisha hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa miaka miwili ya Ubunge wake katika jijini hapa .

Amesema kuwa miradi inayotekelezwa katika Wilaya zote ni pamoja na ujenzi wa nyumba za biashara pamoja na kalasha lengo likiwa ni kuwakwamua wanawake kiuchumi.

‘Uwezeshaji huu kwa wanawake wa Mkoa Mbeya katika kipindi chote cha miaka miwili nimefanya kupitia taasisi yangu ya Women Empowerment Foundation (MWEF),nitazidi kuwainua zaidi na zaidi lengo ni kuona kila mwanamke anakuwa na uchumi wake ambao utamfanya asiwe tegemezi katika familia yake “amesema Mhandisi Mahundi.

Akizungumzia kuhusu ushirikiano Mhandisi Mahundi amesema katika kufikia maendeleo yeyote wanawake wanapaswa kuungana ili kuhakikisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anashinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu ujao.

Hata hivyo Mhandisi Mahundi amesema anatarajia kupita kila Wilaya na wawezeshaji kutoka SIDO ili waweze kutoa semina elekezi kwa wanawake ili wajue namna ya kutumia mashine mbalimbali pamoja na ujasiliamali wa kujiongezea kipato.

“Sisi wanawake ni jeshi kubwa hivyo hatuna budi kuwa kitu kimoja ili 2025 Rais wetu mpendwa Rais.Dkt.Samia Suluhu Hassan anapata kura za kishindo hasa sisi wanawake wa Mkoa Mbeya tupate kura za kumwagika”amesema Mhandisi Mahundi.

Akielezea zaidi Mhandisi Mahundi amesema kwamba kupitia Taasisi ya Maryprisca Women Empowerment Foundation (MWEF) anatarajia kujenga mabweni ya wasichana na kuwalipia mahitaji yote ya msingi.

Pia amesema matarajio yake ni kuandaa tamasha la Mama Ntilie(Mama Ntilie Festival 2023) katika wilaya zote za Mkoa wa Mbeya na atatoa majiko 100 ya gesi ili iwe chachu ya kutunza mazingira na kuhifadhi vyanzo vya maji katika maeneo yao wanayoishi ambayo yana vyanzo vya maji.

Akizungumza na Timesmajira mmoja wanawake waliowezeshwa na Mbunge huyo ,Zabibu Mohamed amesema kuwa fedha hizo zimeweza kumsaidia kwa kiasi kikubwa kwani mpaka sasa ana mradi mkubwa wa kupika chakula katika Wilaya ya Rujewa ambapo ameweza kuwapatia ajira wanawake wenzie na kuweza kuhudumia familia zao.

“Binafsi sijutii hizi nimefanya malengo makubwa sana huku kwenye chama tunaendelea na miradi yetu kama kawaida hatutaki kumwangusha Mbunge wetu Mhandisi Maryprisca Mahundi anafanya Kazi kubwa ya kuwakomboa wanawake wote wa wilaya zote za Mkoa wa Mbeya, “amesema.